RC PWANI AWATAKA WATAALAM WA HALMASHAURI KUWATUMIA WAKANDARASI WENYE SIFA NA UWEZO UJENZI WA MIRADI
Na Gustaphu Haule, Pwani
MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amewataka wataalam wa Halmashauri kuwatumia wakandarasi wenye sifa na uwezo katika ujenzi wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati pamoja na kuwepo kwa viwango vinavyotakiwa.
Kunenge ametoa wito huo Julai 2/2026 wakati akizungumza na viongozi mbalimbali wa Halmashauri na wadau wa maendeleo katika Warsha ya wadau wa Usimamizi na Utekelezaji wa miradi ya Maendeleo iliyokuwa imeandaliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Pwani.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akizungumza katika Warsha ya wadau wa Usimamizi na Utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyofanyika Julai 2,2026 chini Takukuru Mkoa wa Pwani.Kunenge amesema kuwa kuna tabia imejengeka kwa baadhi ya Halmashauri kwani utoa tenda ya ujenzi wa miradi ya maendeleo kwa kumpa mkandarasi ambaye hana uwezo lakini kibaya zaidi mkandarasi mmoja anapewa miradi 10 wakati mkandarasi huyo hana uwezo wa kuitekeleza .
Amesema kitendo cha kumpa mkandarasi mmoja miradi mingi kwa wakati mmoja ndicho kinasababisha miradi mingi kukwama kutokana na uwezo kuwa mdogo lakini hata ufuatiliaji wake unakuwa mgumu.
Kunenge ameagiza kuanzia sasa kuhakikisha mkandarasi anayepewa kazi ya kujenga mradi wa maendeleo afuatiliwe maeneo ambayo tayari alifanyakazi ili kuona na kujiridhisha juu uwezo na ubora wa kazi zake na ndipo mkataba usainiwe.
Wadau mbalimbali walioshiriki Warsha ya Wadau wa Usimamizi na Utekelezaji wa miradi ya Maendeleo iliyofanyika Julai 2,2026 kupitia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)Mkoa wa Pwani.Aidha,amesema kumpa mkandarasi mradi sio mwisho kwani wataalam wa Halmashauri husika nao wahakikishe wanaitembelea miradi hiyo na kufanya mikutano ( Site Meeting) ili kujiridhisha na kile ambacho kinafanyika kwani kama miradi haitembelewi ni rahisi kukwama.
"Hakuna sababu ya miradi kukwama na kwamba wasimamie kikamilifu miradi na kama kuna vifaa vipo nje ya mradi wavikatae kwani kukubali vifaa ambavyo havipo katika mkataba ni kuitia hasara Serikali,naamini miradi ikitumia vipimo sahihi na usimamizi mzuri hakuna mradi ambao utakwama ,"amesema Kunenge.
Amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan ameagiza kila linalofanyika liendane na dira ya 2020/2050 na katika kufikia malengo hayo lazima kwasasa kila mradi utekelezwe na wataalam wenye sifa zinazotakiwa,kuwepo kwa meneja wa mradi,uwazi na uwajibikaji.
Kunenge ameipongeza Takukuru Mkoa wa Pwani kwa kufanyakazi nzuri ya ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo huku akisema kazi yao inasaidia kwa kiwango kikubwa kuongeza uwajibikaji kwa wataalam wa usimamizi wa miradi.
Mkuu wa Taasisi ya kuzuia na Kupambana na Rushwa ( TAKUKURU) Mkoa wa Pwani Domina Mukama amesema Warsha hiyo imekuja kipindi hiki kwasababu kuna programu maalum ya ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo inayoitwa PETS .
Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Domina Mukama akizungumza na wadau mbalimbali katika Warsha ya wadau wa Usimamizi na Utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyofanyika Julai 2,2026 chini ya TAKUKURU mkoa wa Pwani.Mukama, amesema programu hiyo kazi yake kubwa ni kufuatilia miradi ya maendeleo ambayo inatekelezwa katika eneo husika na ndio maana Takukuru imefanya Warsha hiyo katika eneo lake la Mkoa.
Amesema programu hiyo ni ya muda mrefu na imefanyika nchi nzima na kwamba baada ya kufanyika kwa muda mrefu imefanyika tathmini kwa kuangalia maeneo ambayo kwa miradi ya nchi nzima yapi yanausumbufu na yapi hayajatekelezwa vizuri.
Amesema katika Warsha hiyo waliita wadau wote muhimu wakiwemo wakuu wa taasisi, Wakurugenzi wa Halmashauri,Wakuu wa idara,Wakuu wa Wilaya,wenyeviti wa Halmashauri, Makatibu Tawala wa Wilaya na wadau wengine kwakuwa wao ndio watekeleza wa miradi yote inayofanyika katika Halmashauri zao.
Washiriki wa Warsha ya wadau wa Usimamizi na Utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyofanyika Julai 2,2026 chini Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Pwani.Amesema jambo la msingi lilikuwa ni kutaka kuwapitisha katika miradi yao wanayoitekeleza na kuwaonyesha mapungufu ili wayafanyiekazi ili miradi hiyo iweze kukamilika na kutoa huduma bora kwa Wananchi kama ambavyo Serikali imekusudia.
"TAKUKURU inataka kuona kama hospitali majengo yanajengwa,vifaa vinakuwepo na madaktari wanakuwepo wa kutosha ili kupatikane huduma bora na vivyo hivyo katika miradi ya maji na hata miradi mingine ya maendeleo", amesema Mukama.
Mukama amesema katika Warsha hiyo walikuwa na Tarura, Tanroads, Tanesco, Dawasa, REA ili waone namna ya kusimamia miradi yao kwa viwango ambavyo Takukuru inaelekeza ili mwisho wa siku kila mradi uliopo ndani ya Mkoa utoe thamani halisi na Wananchi wapate huduma bora.
Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Hadija Nasri ameipongeza Takukuru Mkoa wa Pwani kupitia Mkuu wake Domina Mukama kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kusukuma gurudumu la maendeleo ndani ya Mkoa.
Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Hadija Nasri akichangia jambo katika Warsha ya wadau wa Usimamizi na Utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyofanyika Julai 2,2026 chini ya TAKUKURU Mkoa wa Pwani.Hata hivyo, Nasri amesema kuwa miradi inatekelezwa kupitia force akaunti lakini changamoto kubwa ni kwamba miradi mingi inatekelezwa kwenye maeneo ambayo wanaishi viongozi jambo ambalo linapelekea baadhi ya maeneo kukosa miradi ya utekelezaji.






Post a Comment