HEADER AD

HEADER AD

CCM PWANI YAWAONYA WANACHAMA WAKE KUACHA KUJIBIZANA MITANDAONI, HAKUNA ALIYE JUU YA CHAMA

>> Yaelekeza migogoro yote Kushughulikiwa ndani ya vyombo rasmi, Yawataka Wanachama Kuepuka Majibizano Mitandaoni

Na Gustaphu Haule,Pwani

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani kimewaonya wanachama wake kuacha tabia ya kutatua tofauti zao nje ya utaratibu wa Chama kwakuwa hakuna mwanachama aliye juu ya Katiba, Kanuni na mamlaka ya Chama.

Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani Dkt.David Mramba ametoa kauli hiyo Oktoba 21, 2026,katika mkutano na Waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za chama hicho.

         Katibu wa Siasa, Uenezi, na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani Dkt.David Mramba akizungumza na waandishi wa habari Oktoba 21,2026 katika ofisi za Chama hicho zilizopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha.

Dkt.Mramba amesema kuwa CCM ina vyombo na vikao halali vilivyowekwa kwa ajili ya kusimamia nidhamu na kutatua migogoro, hivyo kila mwenye hoja anatakiwa kufuata mkondo huo na kuheshimu maamuzi yatakayotolewa.

"Chama ni kikubwa kuliko mwanachama, hakuna mgogoro unaopaswa kuvunja taratibu za kiuongozi na ujasiri wa kweli ndani ya Chama si kupaza sauti zaidi ya wengine, bali ni kuwa na hoja, nidhamu na subira,"amesema Dkt Mramba

Aidha, Dkt Mramba  amekemea tabia ya baadhi ya wanachama na wasio wanachama kutumia lugha za uchochezi na kujibizana kwenye mitandao ya kijamii kwani tabia hiyo inahatarisha umoja wa Chama.

Mramba ameongeza kuwa CCM Mkoa wa Pwani imesisitiza kuwa tofauti za kimtazamo zisigeuzwe kuwa mapambano ya hadharani kabla ya taratibu za Chama kufuatwa.

          Dkt.David Mramba Katibu wa Siasa, Uenezi, na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi ( CCM) Mkoa wa Pwani.

"Tofauti za kimtazamo zisigeuzwe kuwa mapambano ya hadharani kabla ya taratibu za chama kufuatwa kwani kila mwanachama lazima aheshimu na kukilinda chama kwa mujibu wa utaratibu,"amesema Dkt.Mramba.

Mramba ametoa wito kwa wanachama wote kuelekeza nguvu zao katika kuzisemea na kuzitangaza kwa ujasiri kazi kubwa zilizofanywa na Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, badala ya kutumia muda mrefu kujibizana mitandaoni.

Hatahivyo, Mramba amewataka viongozi wote wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani kuheshimu na kulinda mipaka yao katika utekelezaji wa majukumu yao.


No comments