MEYA KIBAHA ATAKA WANAOCHIMBA MCHANGA BWAWA LA CHUMVI KUFUATA UTARATIBU

Na Gustaphu Haule, Pwani
MSTAHIKI Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Mawazo Nicas ameendelea kusimamia msimamo wake wa kusitisha Shughuli za uchimbaji wa mchanga katika bwawa la Chumvi lililopo Kata ya Visiga na kusema kama mtu anataka kuchimba mchanga katika eneo hilo ni vyema akafuata utaratibu.
Amesema hawezi kukubali kuona mapato ya Manispaa yanapotea ili hali yapo mambo mengi ya kimaendeleo yanatakiwa kufanywa na yanahitaji fedha kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato ya ndani.
Dr.Nicas ametoa kauli hiyo Oktoba 23/2026 katika kikao cha pamoja na wawekezaji waliokuwa wakichimba mchanga katika bwawa la Chumvi pamoja na waandishi wa habari.
Kikao cha Mstahiki meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Nicas Mawazo juu ya kujadili namna ya kudhibiti uchimbaji mchanga katika bwawa la chumvi lililopo Kata ya Visiga, kikao hicho kilifanyika Oktoba 23/2026.[10/25, 7:34 PM] gustafu82@gmail.com: Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Mawazo Nicas akiwa katika kikao baina yake na mwekezaji wa machimbo ya mchanga Bwawa la Chumvi Innocent Godwin.
Amesema kuwa yeye hamtambui mwekezaji yeyote kwakuwa Manispaa ya Kibaha haikutoa kibali cha kuchimba mchanga katika eneo hilo huku akisisitiza hataki kuona mtu anafanya shughuli za uchimbaji wa mchanga katika eneo hilo.
Dr.Nicas amesema anachotaka ni kuona Manispaa inakusanya kodi ili itoe huduma kwa wananchi lakini kama kuna ujanja ujanja unatumika kuhujumu mapato ya Manispaa yeye hayupo tayari.
Amesema kwa kipindi ambacho mchanga umechimbwa katika machimbo hayo hakuna taarifa zinazoonyesha Manispaa imekusanya kodi kwa kiasi gani na badala yake mazingira yanaharibiwa na hakuna kinachopatikana.
"Narudi tena, hakuna ruhusa kwa mtu yeyote kuchimba mchanga katika eneo hilo na sisi Manispaa ya Kibaha tumejipanga vizuri kuhakikisha kila atakayejaribu kuingia katika eneo hilo anakamatwa na kuchukuliwa hatua,"amesema Nicas.
Nicas, amesema kama kuna mtu anataka kuchimba mchanga katika eneo hilo ni vyema akafuata utaratibu na kupewa vibali vinavyoeleweka ili kuhakikisha mapato ya Manispaa yanapatikana kwa usahihi na njia halali.
Dr.Nicas ameagiza kuchukuliwa kwa hatua dhidi ya watendaji ambao walihusika kutoa ruhusa ya kuchimba mchanga katika eneo hilo pasipo kutanguliza mbele maslahi ya Manispaa huku akisema wanaopaswa kuchukuliwa hatua ni mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, Mtendaji wa Mtaa na Mtendaji wa Kata.
Amesema kuwa wakati alipofanya ziara katika machimbo hayo alihoji uhalali wa kuchimba mchanga katika eneo hilo na aliomba kibali lakini aliambiwa ataletewa na alipoletewa kibali hicho kilionyesha kimetoka katika Halmashauri ya Kibaha Vijijini.
Amesema kibaya zaidi watu waliokuwa na mashine za kukatia ushuru (Posi) baada ya kuona amefika katika eneo hilo walikimbia na hawakuonekana hadi alipoondoka eneo hilo jambo ambalo lilimtia mashaka na ndio maana anataka kuona mapato ya eneo hilo yanajulikana.
Amesema anashangaa kuona kibali kimeonyesha Kibaha Vijijini lakini eneo lipo Manispaa jambo ambalo ni tofauti lakini hata kibali alicholetewa kimeonyesha kina utata na kwamba anachotaka Manispaa ya Kibaha kipate mapato yake kikamilifu.
Ameongeza kuwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ameleta fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo lakini hawezi kuleta fedha kwa ajili ya kila kitu kwakuwa anajua yapo mapato ya ndani ambayo yanaweza kusaidia katika utatuzi wa changamoto ndogondogo.
Amesema kutokana na hali hiyo lazima Manispaa ikusanye fedha kutoka katika vyanzo vyake kwa ajili ya kupeleka huduma kwa wananchi lakini inapofika mahali anaona mambo yanakwenda tofauti hawezi kukubali.
"Nimeaminiwa na waheshimiwa madiwani wenzangu niwe mwakilishi wao wa Manispaa kwa miaka mitano na moja ya kazi ninayotakiwa kuifanya ni kuhakikisha nalinda raslimali za Manispaa na kuwa msimamizi wa mapato kwahiyo sitokuwa na mchezo wala kucheka na watu wanahujumu mapato ya Manispaa,"amesema Nicas.
Mwekezaji aliyekuwa anachimba mchanga katika eneo la Bwawa la Chumvi Innocent Godwin amesema kuwa yeye alipata kibali cha kuchimba mchanga katika eneo hilo kupitia vikao halali vya Kata ya Kawawa.
Mwekezaji wa machimbo ya mchanga katika bwawa la Chumvi lililopo Kata ya Visiga Manispaa ya Kibaha Innocent Godwin akiwaeleza waandishi wa habari namna alivyopata kibali cha kuchimba mchanga katika bwawa hilo.Amesema amechimba mchanga kwa muda wa siku mbili na ndipo akashangaa anasimamishwa kuchimba ili hali alifuata utaratibu kuanzia ngazi ya Kijiji hadi Kata na fedha zilikuwa zinalipwa kupitia Posi ya Halmashauri ya Kibaha Vijijini na Manispaa ya Kibaha.
Godwin amesema yeye hana kosa kwani kama kuna kosa basi wanaopaswa kuadhibiwa ni viongozi wa Serikali ya Kijiji, Mtaa na Kata ambao ndio walitoa ruhusa kwa yeye kuwekeza katika eneo hilo.
Amesema kwa muda wa siku mbili alizochimba mchanga katika eneo hilo alikuwa analipa kila gari ushuru wa Sh.15000 na kwamba hakuna mahali ambapo hakulipa ila kama changamoto imejitokeza basi ni upande wa Serikali yenyewe.
Ameiomba Serikali kupitia watumishi wake kuwa wakweli kwa wawekezaji kwa kuwapa taarifa sahihi kwani inapotokea changamoto wanaopata hasara ni mwekezaji ambaye ametumia fedha nyingi kuwekeza.

Post a Comment