HEADER AD

HEADER AD

TRA PWANI YAWAHIMIZA WANAWAKE KULIPA KODI KIKAMILIFU


Na Gustaphu Haule, Pwani

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa Pwani imesema kuwa Wanawake wananafasi kubwa ya kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi endapo watashiriki kikamilifu katika suala la ulipaji wa kodi.

Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Pwani Salim Makame, ametoa kauli hiyo Oktoba 20,2026 wakati akifungua kongamano la Jukwaa la Wanawake na Kodi lililofanyika Kibaha kwa Mathias.

          Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Pwani Salim Makame akiwa katika kongamano la Jukwaa la Wanawake na Kodi lililofanyika Oktoba 20,2026 .

Kongamano hilo lilikuwa ni kwa ajili ya kutoa elimu ya kodi kwa wanawake ambapo lengo kubwa ni kuwashirikisha wanawake hao juu ya umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari kupitia biashara zao mbalimbali.

Makame amesema kuwa Wanawake ni muhimili mkubwa wa Taifa kwani takwimu zinaonyesha Wanawake ndio wanachangia kwa kiasi kikubwa uchumi wa Tanzania kupitia shughuli zao za kibiashara na za kijasiriamali.

Amesema bila Wanawake kushiriki katika kulipa kodi yapo mambo yanaweza kukwama na hata uchumi wa nchi ukashindwa kukua na hivyo kuchelewesha baadhi ya malengo ya Taifa.

       Kongamano la Jukwaa la Wanawake na Kodi  lililofanyika Oktoba 20,2026 Kibaha Mkoa wa Pwani.

Makame ameongeza kuwa, TRA kwa kutambua umuhimu wa Wanawake hao imeona ni vyema ikawakutanisha pamoja na kuwapa elimu ya kodi ili na wao waweze kushiriki moja kwa moja katika suala la ulipaji kodi.

Amesema TRA inataka Wanawake washiriki suala la ulipaji kodi kwakuwa kodi ndio nguzo ya uchumi wa Taifa kwani mapato yake ndio yanayosaidia kujenga barabara, miundombinu ya elimu, afya na kuboresha huduma nyingine za kijamii.

"Kupitia Jukwaa hili la Wanawake mtapata uelewa wa namna ya kulipakodi, kutambua umuhimu wa kudai na kutoa risiti katika biashara zenu na mkifanya hivyo mtakuwa mmelisaidia Taifa katika kuboresha miundombinu ambayo itasaidia kuboresha utoaji wa huduma za jamii,"amesema Makame.

Makame amesema kuwa TRA inatoa huduma kwa kuzingatia uwazi, uwajibikaji, uadilifu na uaminifu na kwamba wapo tayari kuhakikisha wanashirikiana vyema na Wanawake hao ili waweze kufikia malengo yao ya kibiashara.

        Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Pwani Salim Makame akizungumza wakati akifungua Kongamano la Jukwaa la Wanawake na Kodi lililofanyika Oktoba 20,2026 Kibaha Pwani.

Amewasihi Wanawake kuhakikisha wanazitumia fursa zilizopo TRA ili waweze kupata elimu ya namna ya kukuza biashara zao na hivyo kufikia hatua ya kuwa wafanyabishara wakubwa hapa nchini.

Mratibu wa kongamano la Jukwaa la Wanawake na Kodi ambaye pia ni afisa uhusiano Mkuu wa TRA nchini Rechal Mkundai amesema kuwa Jukwaa la Wanawake na Kodi ni msingi wa kuwajenga Wanawake kiuchumi ambapo kauli mbiu yake ni"Nguzo ya Maendeleo ya Tanzania.

Mkundai, amesema kuwa Jukwaa hilo lilianzishwa Machi 6,2026 na Kamishna wa TRA Nchini Yusuf Mwenda ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani.

            Afisa Uhusiano Mkuu wa TRA ambaye pia ni Mratibu wa Jukwaa la  Wanawake na Kodi Rachel Mkundai akizungumza katika kongamano la Wanawake na Kodi lililofanyika Oktoba 20,2026 Kibaha Mkoa wa Pwani.

Amesema lengo la kuanzisha Jukwaa hilo ni kutoa elimu ya kodi kwa Wanawake na hata vijana kwakuwa TRA inataka kuona Wanawake wanapata kuinuka kiuchumi kupitia mafunzo na elimu mbalimbali wanayoitoa.

Amesema tangu kuanzishwa wa Jukwaa hilo tayari wamewafikia Wanawake wajasiriamali zaidi ya 2,300 kutoka mikoa mitatu waliyofanya kongamano hilo ukiwemo Mkoa wa Dar es Salaam, Mkoa wa Tanga na Mkoa wa Pwani.

Mkundai amesema  lengo la TRA ni kuhakikisha wanafanya kongamano la majukwaa ya Wanawake na Kodi katika Mikoa yote ya Tanzania Bara lakini mipango ya mbeleni ni kushuka katika ngazi ya Wilaya na hadi ngazi ya Kata ili kuweza kuwafikia Wanawake wengi zaidi.

"Jukwaa la Wanawake na Kodi la TRA lengo lake kubwa ni kutoa fursa kwa Wanawake wajasiriamali kupata elimu ya kodi kwa lugha rahisi ambayo inaeleweka kwa wajasiriamali lakini pia lengo kuu ni kumpa elimu na kumpa fursa mbalimbali mwanamke kutoka kwa wadau ili waweze kukua kibiashara na kuingia katika mnyororo wa kuchangia uchumi wa Taifa,"amesema Mkundai

Mkundai ameongeza kuwa katika makongamano hayo si tu wanatoa elimu ya kodi bali wanatoa pia huduma mbalimbali ikiwemo ya usajili na kutoa namba ya utambulisho kwa mlipakodi mjasiriamali ( TN Number), elimu kuhusu forodha, manunuzi na huduma nyingine za kibiashara.

Mwenyekiti wa Umoja wa Machinga Mkoa wa Pwani Philemon Maliga, ameipongeza TRA Mkoa wa Pwani kwakuwakutanisha Wanawake hao katika kongamano hilo ambapo ameahidi kushirikiana na TRA pamoja na Serikali katika kuhamasisha Wanawake kujisajili na kulipakodi.

       Mwenyekiti wa Umoja wa Machinga Mkoa wa Pwani Philemoni Maliga( Katikati) akiwa katika kongamano la Jukwaa la Wanawake na Kodi lililofanyika Oktoba 20,2026 Kibaha - Pwani.

Akizungumza kwa niaba ya Wanawake hao mwenyekiti wa UWT Kata ya Tangini Yohana Mwananjela ameishukuru TRA Mkoa wa Pwani kwa kuwapa elimu hiyo huku akisema watakwenda kuitumia elimu hiyo katika kukuza biashara zao.

Hata hivyo,Mwananjela ameiomba TRA kuendelea kutoa elimu hiyo mara kwa mara ili kuhakikisha wanawajengea uwezo ambao utawasaidia kuimarisha na kukuza biashara zao na hivyo kusaidia katika kukuza uchumi wa Taifa.

       Viongozi mbalimbali wakiwa katika Kongamano la Jukwaa la Wanawake na Kodi lililoandaliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) Mkoa wa Pwani.


No comments