SERIKALI KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA WAWEKEZAJI KIKIWEMO KIWANDA CHA GOODLWILL CERAMIC COMPANY LTD

>> DC Mkuranga asema uwekezaji umesaidia kuongeza uchumi
Na Gustaphu Haule, Pwani
MKUU wa Wilaya ya Mkuranga Mwinyi Ahmed, amesema Serikali Wilayani humo itaendelea kushirikiana na Wawekezaji wa kiwanda cha GoodWill Tanzania Ceramic Company Ltd katika kuhakikisha inatatua changamoto zinazokikabili kiwanda hicho.
Mwinyi,ametoa kauli hiyo Oktoba 26/2026 wakati akizungumza na viongozi mbalimbali wa kiwanda hicho, akiwemo Mwenyekiti wa Kampuni ya Goodwill Ceramic Wu-QiQuan, MKurugenzi Mtendaji wa Goodwill Ceramic Sharifa Shen,kamati ya ulinzi na usalama Wilaya ya Mkuranga na wananchi wa Kijiji cha Mkiu alipokuwa akifanya ziara ya kutembelea na kukagua maendeleo ya kiwanda hicho.
Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Mwinyi Ahmed wa kwanza (kulia) akikagua bidhaa zinazotengenezwa katika kiwanda cha Goodwill Tanzania Ceramic kilichopo katika Kijiji cha Mkiu Wilayani Mkuranga, katikati ni MKurugenzi Mtendaji wa Goodwill Tanzania Ceramic Sharifa Chen na watatu kushoto ni Mwenyekiti wa makampuni ya Goodwill Tanzania Ceramic Wu QiQuan.
Amesema uwekezaji uliofanywa na kiwanda hicho ni mkubwa kwani umesaidia kuongeza uchumi kwa wananchi wa Wilaya ya Mkuranga pamoja, kuongeza pato la Taifa sambamba na kutoa ajira rasmi kwa watanzania wapatao 2,800 na zisizo rasmi 25,000.
Amesema kufuatia umuhimu mkubwa uliopo katika kiwanda hicho ni lazima Serikali ione namna ya kushirikiana na uongozi wa kiwanda hicho ili kusudi kutatua Changamoto zao na hivyo waendelee na uzalishaji ambao umekuwa na manufaa kwa Taifa la Tanzania.
"Leo ni mara yangu ya kwanza kutembelea kiwanda hiki,nimeona uwekezaji mkubwa uliofanyika katika kiwanda hiki kwani nimejionea shughuli mbalimbali za uzalishaji wa Marumaru, Vikombe,Sahani, Bakuli,vifaa vya chooni "amesema Mwinyi.
Mwinyi amesema kuwa kwa uwekezaji uliofanywa na kiwanda cha Goodwill lazima Serikali ione namna ya kutatua Changamoto zao kama ambavyo dira ya maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050 inavyoelekeza asilimia 70 ya ajira inatoka katika sekta binafsi na kwamba atakaa na Waziri wa Viwanda na Wizara nyingine zinazohusika ili kuona namna ya kutatua Changamoto za kiwanda hicho.
Sinki za choo zinazotengenezwa na kiwanda cha Goodwill kilichopo Mkiu Wilayani Mkuranga Mkoa wa Pwani.
Mwinyi amekipongeza kiwanda cha Goodwill katika kurudisha kwa jamii kwa kusaidia mahitaji mbalimbali hususani katika kujenga na kuboresha madarasa ya shule mbalimbali, kusaidia katika ujenzi wa vituo vya kutolea huduma ya afya na mahitaji mengine huku akisema kitendo hicho ni kizuri kwakuwa kinasaidia kujenga mahusiano mazuri na jamii.
"Nimepata orodha ya vitu vilivyofanywa na kiwanda hiki cha Goodwill Tanzania Ceramic kwa jamii kwani wamejenga madarasa shule Msingi Mkiu na kuboresha miundombinu yake, wamesaidia katika ujenzi wa Zahanati na maeneo mengine mbalimbali hivyo nawapongeza kwa kazi nzuri waliyoifanya," Amesema Mwinyi
Mwinyi ametoa wito kwa wawekezaji wengine wa viwanda kuangalia namna bora ya kurudisha kwa jamii ili kujenga mahusiano na wananchi na jamii inayowazunguka kwa ujumla.
Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga akikagua mashine ya kutengenezea Sahani katika kiwanda cha Goodwill Kilichopo Mkuranga Mkoa wa Pwani .
Kuhusu uwekezaji Wilayani humo, Mwinyi amesema anawakaribisha wawekezaji wengine kwenda kuwekeza Wilayani humo kwakuwa Mkuranga ni eneo nzuri la uwekezaji lenye ardhi kubwa na yakutosha.
Amesema Mkuranga imepata bahati ya kupitiwa na bomba la gesi na umeme upo wa kutosha hivyo kama kuna mtu anataka kuwekeza atakuta mazingira ya uwekezaji yapo vizuri yakiwa sambamba na upatikanaji wa nishati ya umeme na gesi.
Amesema kuwa kwasasa tayari wapo wadau wameanzisha Kongani ya viwanda kwa nguvu zao wenyewe na wapo ambao wanaeneo la ukubwa wa hekta 5000 na pia yapo maeneo ya wazi ambayo ni mazuri kwa uwekezaji kwahiyo mtu yeyote anayetaka kuwekeza atapewa kipaumbele.
MKurugenzi wa utawala wa kampuni ya goodwill Ceramic Tanzania Xie Xiaoming amesema moja ya Changamoto inayowakabili ni ucheleweshaji wa kusafirisha mizigo kutoka Bandarini hali ambayo inakwamisha shughuli za uwekezaji.
MKurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Goodwill Tanzania Ceramic Sharifa Shen {kulia} akifafanua jambo kwa Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Mwinyi Ahmed alipotembelea kukagua kiwanda cha Goodwill kilichopo katika Kijiji cha Mkiu Oktoba 26/2026.
Amesema wakati mwingine kushusha mizigo bandarini hapo inachukua muda mrefu ikiwa ni mwezi mmoja hadi miezi miwili ambapo ameomba Serikali kuona namna ya kupanua bandari hiyo ili kuongeza uwezo wake.
Amesema Changamoto nyingine ni muingiliano wa soko kwani yapo makampuni yanazalisha Marumaru chini ya kiwango na hivyo kuathiri soko lao ambapo ameomba msaada kutoka uongozi wa Serikali ya juu kuona namna ya kudhibiti uzalishaji holela wa bidhaa za Marumaru ili kukipa heshima kiwanda cha Goodwill.
Mwenyekiti wa Makampuni ya Goodwill Tanzania Ceramic Company Ltd Wu-QiQuan amesema anaishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji.
Amesema Serikali ya Tanzania imekuwa na mazingira mazuri ya uwekezaji pamoja na masoko mazuri ya kuuza bidhaa zao na kwamba kutokana na hali hiyo kampuni imejipanga kujenga viwanda vingine vitakavyotoa ajira 10,000 kwa Watanzania.
Hata hivyo, akiwasilisha mada juu ya kiwanda hicho mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Meneja biashara wa kiwanda hicho Jiang Hong,amesema kiwanda hicho kilianzishwa mwaka 2016 na hadi sasa kimetimiza miaka 10 tangu kuanzishwa kwake.
Amesema kuwa awali walianza kuzalisha Marumaru za chini na ukutani lakini kwasasa kiwanda kimepanuka na kuzalisha Bakuli, Sahani, vikombe, vifaa vya bafuni na utengenezaji wa vyoo vya kisasa huku akisema kiwanda kimesaidia kutoa ajira rasmi 2,800 na ajira zisizo rasmi 25,000.
Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Mwinyi Ahmed= {Katikati} akiwa katika ziara yake ya kukitembelea kiwanda cha Goodwill kilichopo Mkiu Wilayani humo, kushoto ni Mwenyekiti wa makampuni ya Goodwill Tanzania Ceramic Wu QiQuan na kulia ni MKurugenzi Mtendaji wa Goodwill Tanzania Ceramic Sharifa Shen.






Post a Comment