HEADER AD

HEADER AD

MRATIBU KAMPENI YA MSAADA WA KISHERIA YA MAMA SAMIA AWATAHADHARISHA WANAUME WANAOISHI NA WANAWAKE BILA KUFUNGA NDOA


Na Gustaphu Haule, Chalinze 

MRATIBU wa Kampeni ya Msaada wa kisheria ya Mama Samia katika Halmashauri ya Chalinze Marwa Mohere, amewatahadharisha wanaume ambao wameishi na Wanawake katika kipindi cha miaka miwili na zaidi bila kufunga ndoa watambue kuwa hiyo ni dhana ya ndoa na kwa vyovyote Mwanaume akitaka kumuacha Mwanamke huyo ajue Sheria itafuata mkondo ikiwa pamoja na kugawana mali walizochuma.

Mohere ambaye pia ni Wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria amebainisha hilo Novemba 02 ,2027 wakati akitoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wajumbe wa bodi ya usuluhishi wa Kata ya Miono Halmashauri ya Chalinze Wilaya ya Bagamoyo mkoa wa Pwani yaliyofanyika katika ofisi ya Kata hiyo.

        Mratibu wa Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia katika Halmashauri ya Chalinze na Wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Marwa Mohere akiwaeleza wajumbe wa bodi ya usuluhishi ya migogoro ya ndoa ya Kata ya Miono namna ya kujaza fomu za usuluhishi wanapokuwa wakimsikiliza migogoro ya wananchi wao.

Amesema kuwa wapo wanaume wanaishi na watoto wa watu kwa miaka miwili au zaidi bila hata kufunga ndoa lakini unapofika wakati ambao wamefanikiwa kimaisha  mwanaume anatafuta sababu ya kumfukuza Mwanawake bila kujua kufanya hivyo ni kosa.

Amesema kifungu cha 160,sura ya 29 Sheria ya ndoa ya mwaka 2023 inatambua kuwa kama watu hao waliishi miaka miwili au zaidi wanatambulika kuwa ni kama mume na mke kupitia dhana ya ndoa na kwamba lazima mali zilizochumwa katika kipindi hicho zitagawanywa.

Mohere ameenda mbali zaidi kwa kusema wengine wameishi katika kipindi cha miaka miwili na watoto wakazaa lakini kwasababu mwanaume ameona amefanikiwa kimaisha basi anatoa taraka jambo ambalo sio sahihi.

Amewasisitiza wajumbe wa bodi ya usuluhishi wa migogoro ya ndoa kuhakikisha anapofika mtu kama huyo kutaka kutoa taraka kwa Mwanamke wahakikishe wanatenda haki kwakuwa sheria ipo na imewekwa kwa ajili ya kuwalinda Wanawake wanaoonewa .

      Wataalamu wa kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia akiwemo mratibu wa Kampeni hiyo katika Halmashauri ya Chalinze Marwa Mohere ,wakiwa na wajumbe wa bodi ya usuluhishi ya migogoro ya ndoa  Kata ya Miono mara baada ya kumaliza mafunzo ya kuwajengea uwezo wajumbe hao yaliyofanyika Novemba 02,2026 katika ofisi ya Kata ya Miono.

"Utakuta Mwanaume ameishi na Mwanamke kwa muda wa miaka miwili au zaidi na katika kipindi chote hicho wamefanikiwa kupata mali na uchumi umekuwa mzuri na hata watoto wamepata lakini Mwanaume baada ya kuona hivyo anatafuta sababu na mwisho wa siku anatoa taraka kwa Mwanamke jambo ambalo kisheria lazima lichukue mkondo wake,"amesema Mohere 

Mohere ameongeza kuwa sheria inatafsiri kuwa mwanamke huyo ni mke halali japo hawakufunga ndoa lakini italazimika kila walichokichuma wakati huo watagawana kwa mujibu  wa Sheria.

Amesema bodi ya usuluhishi ya Kata ni chombo cha usuluhishi na sio chombo cha kutoa hukumu isipokuwa  kama imeshindikana wanaweza kutoa fomu namba 3 ambayo inaruhusu shauri husika liende mbele katika ngazi inayofuata.

Amesema ili Taraka iweze kutolewa lazima ipite bodi ya usuluhishi ya Kata na wahusika waeleze matatizo yao na endapo itashindikana kusuluhisha basi bodi itaandika au itatoa fomu namba 3 ili waende Mahakamani .

Amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameanzisha kampeni ya msaada wa kisheria kwa ajili ya kuwasaidia wananchi kutatua migogoro yao lakini ameona wajumbe wa bodi za usuluhishi ni kundi la watu muhimu ndio maana wamefikiwa kwa kujengewa uwezo.

Amesema mara nyingi wajumbe hao walikuwa wanachanganya mambo kwani walikuwa wanajiita wajumbe wa Baraza la ardhi wakati huo huo wanajadili suala migogoro ya ndoa na migogoro ya ardhi jambo ambalo sio sawa.

         Mratibu wa Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia katika Halmashauri ya Chalinze Wakili kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Marwa Mohere (kushoto) akiteta jambo na Mwanasheria wa Halmashauri ya Chalinze Elizabeth Lukumay katika mafunzo ya kuwajengea uwezo wajumbe wa bodi ya usuluhishi wa migogoro ya ndoa wa Kata ya Miono yaliyofanyika Novemba 02,2026 katika ofisi za Kata hiyo.

Amesema kuwa wao ubadilika kulingana na mgogoro kwani wakati wanajadili au kusuluhisha masuala ya ndoa wanatakiwa kuwa wajumbe wa bodi ya usuluhishi wa ndoa na wakati wanasuluhisha masuala ya migogoro ya ardhi wanatakiwa kujiita wajumbe wa Baraza la Kata.

"Mara nyingi mlikuwa mnachanganya mambo ndio maana maamuzi mliyokuwa mnayatoa yalikuwa yanatupiliwa mbali lakini naamini baada ya mafunzo haya mtakuwa mmepata uelewa wakutosha na hivyo mambo yatakwenda vizuri," ameongeza Wakili Mohere.

Diwani wa Kata ya Miono Kilo Francis, amesema anawashukuru wataalamu wa kampeni ya msaada wa kisheria ya mama Samia kuona umuhimu wa kutoa mafunzo hayo kwa wajumbe wa bodi ya usuluhishi Kata ya Miono.

      Diwani wa Kata ya Miono Kilo Francis akizungumza wakati akifunga mafunzo ya wajumbe wa bodi ya usuluhishi ya migogoro ya ndoa yaliyokuwa yakitolewa na wataalamu wa kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia.

Francis amesema kwa wale ambao wamepata elimu hiyo waende kuwasaidia wananchi kutatua changamoto zao pamoja na kusuluhisha migogoro yao kwa haki bila upendeleo kwani Rais Samia ametoa mafunzo hayo nchi nzima ili kuwawezesha wajumbe kufanya kazi katika mazingira mazuri.

Amesema changamoto kubwa wananchi hawajui Sheria lakini anaamini kupitia wajumbe hao wananchi wengi watapata haki zao kwakuwa dhamana waliyopewa ni kubwa na kwamba na wakifanya vizuri itakuwa sehemu ya kudumisha amani ya nchi.

Mwenyekiti wa Baraza la Kata Miono Kessy Othman,amesema kuwa mafunzo ya msaada wa kisheria yamewasaidia kuwapa elimu ambayo hapo awali walikuwa hawajui na walikuwa wanashindwa waanzie wapi na waishie wapi.

         Mwanasheria wa Halmashauri ya Chalinze Elizabeth Lukumay akitoa elimu ya msaada wa kisheria kwa wajumbe wa bodi ya usuluhishi wa migogoro ya ndoa wa Kata ya Miono katika mafunzo yaliyofanyika Novemba 02,2026 katika ofisi za Kata ya Miono,Wilaya ya Bagamoyo mkoa wa Pwani.

Othmani amesema kuwa kabla ya mafunzo hayo walikuwa wanajua wao ni baraza la ardhi la Kata na walikuwa wanachanganya kila kitu lakini kupitia mafunzo hayo wameweza kutambua kuwa wao ni wajumbe wa bodi ya usuluhishi wa migogoro ya ndoa lakini wanapojadili masuala ya migogoro ya ardhi wanajiita wajumbe wa Baraza la Kata la Miono.

Othmani amesema anamshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo ameweza kuwagusa kupitia kampeni ya msaada wa kisheria wa Mama Samia na kupitia mafunzo hayo anaamini watafanya vizuri hasa katika kuwasaidia wananchi wao.

No comments