HEADER AD

HEADER AD

WAAFUNZI ZAIDI YA 3000 CHALINZE WAFIKIWA NA KAMPENI YA MSAADA WA KISHERIA YA MAMA SAMIA


>> Wapewa elimu ya Sheria juu ya unyanyasaji wa kijinsia, ukatili, haki na wajibu

Na Gustaphu Haule, Chalinze 

KAMPENI ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ( Mama Samia Legal Aid Campaign) imewafikia zaidi ya  wanafunzi 3000 wa shule ya Sekondari Kikaro,shule ya Msingi Misufisini na Shule ya Msingi Kikaro.

Wanafunzi hao wamefikiwa na mpango huo Novemba 02 /2026 kupitia timu ya wataalamu inayoendelea kutekeleza kampeni ya Msaada wa Kisheria ikiongozwa na Mratibu wa Kampeni hiyo Wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Marwa Mohere.

      Mratibu wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ambaye ni wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Marwa Mohere akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kikaro iliyopo Kata ya Miono Halmashauri ya Chalinze Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani.

Wakiwa katika shule hizo wataalamu hao walitoa elimu kwa wanafunzi  kuhusu masuala ya unyanyasaji wa Kijinsia,ukatili,haki,wajibu  pamoja na elimu kuhusu maadili.

Akizungumza na wanafunzi hao Mratibu wa Kampeni ya msaada wa kisheria katika Halmashauri ya Chalinze Wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Marwa Mohere amewataka wanafunzi hao kuhakikisha wanatoa taarifa pale ambapo wanafanyiwa ukatili.

Mohere,amesema kuwa Rais Samia ameanzisha kampeni ya Msaada wa Kisheria ili kusudi kuwasaidia Watanzania katika utatuzi wa migogoro lakini akaona lazima kampeni hiyo ifike kwa wanafunzi ili wapate kujua namna ya kutoa taarifa pale wanapofanyiwa madhira ya ukatili.

      Mratibu wa Kampeni ya msaada wa kisheria ya  katika Halmashauri ya Chalinze ambaye ni wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Marwa Mohere akizungumza na wanafunzi wa shule ya Msingi Misufisini iliyopo Kata ya Miono ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa msaada wa kisheria wa Mama Samia.

Amesema mwanafunzi anatakiwa kutoa taarifa za kuhusu vitendo vya ukatili anavyofanyiwa au pale anapoona mwenzake anafanyiwa na kwamba hatua za kuchukua katika utoaji wa taarifa hiyo ni kuhakikisha anawasilisha kwa makamu Mkuu wa Shule na ikishindikana hapo anaende kwa Mkuu wa Shule.

Amesema kama ngazi hizo zitashindikana kwa utatuzi basi jambo lake litapelekwa katika bodi ya shule na endapo ikashindikana tena basi lalamiko lake alipelekea kituo cha Polisi ili hatua zaidi ziweze kuchukuliwa.

Amesema mwanafunzi hatakiwi kukaa kimya pale anapoona anafanyiwa vitendo vya unyanyasaji na ukatili kwakuwa kufanya hivyo kutapelekea kukosa amani ya kuendelea na masomo na hivyo kukwamisha ndoto za maisha yao.

      Wanafunzi wa shule ya Msingi Misufisini wakiwa katika mkutano wa kampeni ya Msaada wa Kisheria iliyokuwa ikitolewa na wataalamu wa kampeni hiyo akiwemo Wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Marwa Mohere.

"Hii ni timu ya wataalamu ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ambayo inapita kwa ajili ya kusaidia kutatua migogoro mbalimbali lakini Mama Samia ametuelekeza tufike kwenu kuwapa elimu ya masuala ya unyanyasaji wa Kijinsia, ukatili, haki,wajibu na maadili ili pale kunapotokea madhira muweze kutoa taarifa mapema," amesema Mohere 

Mohere amesema Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan anataka wanafunzi wasome katika mazingira mazuri na ndio maana ametuma wataalamu wa masuala ya kisheria ili kuona namna ya kuwasaidia wanafunzi waweze kutambua haki zao.

Mwanasheria wa Halmashauri ya Chalinze Elizabeth Lukumay, amewataka wanafunzi hao kuwa na maadili mema na kuhakikisha wanazingatia masomo yao na hivyo kuacha kujiingiza katika vitendo viovu.

      Mwanasheria wa Halmashauri ya Chalinze Elizabeth Lukumay akitoa somo la maadili kwa wanafunzi wa shule ya Sekondari Kikaro ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia iliyofanyika Novemba 02,2026 katika Kata ya Miono.

"Hakikisheni mnafanya kile kilichowaleta hapa,someni kwa bidii,acheni kujiingiza katika vitendo visivyofaa , Serikali inajitahidi kujenga miundombinu mizuri ya shule ili ninyi msome kwahiyo tumieni vizuri fursa hii kwa ajili ya kuandaa maisha yenu ya baadae,"amesema Lukumay.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Kikaro Emmanuel Kahabi,amesema wazazi wamesahau suala la malezi kwa watoto na kwamba inasaidia kuona pale ambapo watu wa sheria wanatokea na kuwapa elimu ambayo itawafanya waweze kubadilika.

      Wanafunzi wa shule ya Sekondari Kikaro wakiwa katika mkutano wa kampeni ya Msaada wa Kisheria ya mama Samia iliyofanyika shuleni hapo Novemba 02,2026 .

Amempongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha kampeni ya Msaada wa Kisheria kwakuwa jambo hilo linakwenda kuviokoa vizazi wakiwemo wanafunzi ambao kwa namna moja au nyingine walikosa malezi mazuri ya wazazi.

Nae Mkuu wa Shule ya  Msingi Misufisini iliyopo Kata ya Miono Bless Kanuti amewashukuru wataalamu wa msaada wa kisheria kwa kuona umuhimu wa kufika shuleni hapo na kutoa elimu ambayo imewasaidia kuwajenga kimasomo yao.


No comments