WATAALAMU WA KAMPENI YA MSAADA WA KISHERIA YA MAMA SAMIA WATINGA KANISA LA MORAVIAN CHALINZE

>> Mchungaji Mwambona amwagia sifa Rais Samia
Na Gustaphu Haule, Chalinze
MCHUNGAJI wa Kanisa la Moravian lililopo Kata ya Bwilingu katika Halmashauri ya Chalinze Ipyana Mwambona amemshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kubuni mpango wa kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia(Mama Samia Legal Aid Campaign).
Mwambona ,ametoa pongezi na shukrani hizo katika Ibada iliyofanyika Kanisani hapo siku ya Jumapili ya Novemba 01,2026 mara baada ya timu ya wataalamu wa kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia kufika katika Kanisa hilo na kutoa elimu mbalimbali.
Mchungaji wa Kanisa la Moravian lililopo Kata ya Bwilingu Halmashauri ya Chalinze Ipyana Mwambona akizungumza kuhusu umuhimu wa kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia inayoendelea kutolewa katika Halmashauri hiyo.
Amesema kuwa jambo la kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi bila malipo ni ibada na upendo kwa Watanzania na kusema kampeni hiyo mbali na kutoa msaada wa kisheria lakini inachangia kuleta utulivu na kudumisha amani ya nchi.
Amesema maeneo mengi ya Tanzania yamekuwa na migogoro hususani ya ardhi na wananchi wengi hawana elimu wala uwezo wa kujua wapi watakwenda kupata haki zao lakini kupitia kampeni hiyo wananchi wengi watasaidika kwa kupata haki zao.
Mwambona amesema kuwa Rais Samia amefanya jambo jema na kwakutambua umuhimu wa jambo hilo amekubali kwa moyo wa dhati kuwapa nafasi wataalamu kwa ajili ya kuwaeleza waumini wake kile ambacho wanakifanya katika Halmashauri ya Chalinze.
Waumini wa Kanisa la Moravian lililopo Kata Bwilingu Halmashauri ya Chalinze wakimsikiliza mtaalamu wa kampeni ya msaada wa kisheria Moses Matiko ( haonekani pichani)akieleza kuhusu umuhimu wa kampeni hiyo.
Mwambona amewaomba waumini wake kuhakikisha wanajitokeza kutumia fursa hiyo kikamilifu ili waweze kupata msaada wa kisheria katika kutatua migogoro na changamoto zilizopo katika maeneo yao.
"Mimi nampongeza Rais Samia kwa kuanzisha mpango huu mzuri wa kampeni ya msaada wa kisheria lakini nawashukuru ninyi wataalamu kwa kuona umuhimu wa kuja hapa kanisani na kutuletea elimu hii muhimu maana Makanisa yapo mengi na mkachagua kuja hapa,hakika huu ni upendo mkubwa,"amesema Mwambona.
Mwambona amemuomba Rais Samia kuhakikisha kampeni hiyo inakuwa endelevu ili kusudi iweze kuwasaidia Watanzania wengi zaidi ambao kwa namna moja au nyingine huwa wanashindwa kupata haki zao kwakuwa hawana pa kukimbilia.
Mtaalamu wa masuala ya sheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Moses Matiko amesema kuwa lengo la kampeni ya msaada wa kisheria ni kuwafikia wananchi wote na kuwapa msaada wa kisheria katika masuala mbalimbali yanayojitokeza katika jamii.
Mtaalamu wa kampeni ya msaada wa kisheria Wakili kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Moses Matiko akitoa elimu katika Kanisa la Moravian lililopo Kata ya Bwilingu Halmashauri ya Chalinze katika Ibada ya Jumapili Novemba 01,2026 .
Matiko amesema kuwa kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia inasaidia katika utatuzi wa migogoro ya ardhi, migogoro ya ndoa,masuala ya mirathi, ukatili na unyanyasaji wa Kijinsia.
Matiko amesema kuwa kampeni hiyo inaendelea kufanyika Katika Halmashauri ya Chalinze kwa kupita Kata mbalimbali na kwamba pamoja na kupita Kata nyingine lakini kipo kituo maalum cha kupokea migogoro kilichowekwa katika eneo la soko la Bwilingu.
"Kwa hapa Chalinze kampeni hii inaendelea hadi Novemba 07/2026 na tumeweka kituo cha kupokea migogoro ya ardhi,ndoa na mingine katika soko la Bwilingu kwahiyo niwaombe waumini wa Kanisa hili yeyote mwenye mgogoro aje eneo la soko tumuhudumie bila malipo lakini nendeni mkawe mabalozi kwa wengine ili wajue kuhusu kampeni hii,"amesema Matiko.
Hata hivyo,Matiko aliambatana na wataalamu mbalimbali waliofika Kanisani hapo akiwemo mratibu wa Kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia ambaye ni Wakili kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Marwa Mohere pamoja na Msajili Msaidizi wa Kampeni hiyo kutoka katika ya Halmashauri ya Chalinze Michael Mwakanjuki.




Post a Comment