HEADER AD

HEADER AD

HALMASHAURI YA PWANI YAMKOSHA RC KWA UBUNIFU WA VYANZO VYA MAPATO


Na Gustaphu Haule, Pwani

MKUU wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge, ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha kwa kuweka vipaumbele sahihi vya maendeleo vinavyochangia kuongezeka kwa mapato ya ndani na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Kunenge ametoa pongezi hizo katika kikao maalum cha Baraza la Madiwani kwa ajili ya kujadili hoja za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa ukaguzi wa mwaka 2024/2025.

        Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akizungumza katika Baraza maalum la madiwani wa Manispaa ya Kibaha lililofanyika Juni 18/2026.

Kunenge amesema Halmashauri zinapaswa kuendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato na kuwekeza katika miradi ya maendeleo yenye tija ili kuendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2020/2050.

Amesema Manispaa ya Kibaha imeonyesha mafanikio makubwa katika ukusanyaji wa mapato, baada ya kuvuka lengo ililowekewa na Serikali kutoka makusanyo ya Sh.bilioni 19.4 kwa mwaka 2024/2025 hadi kufikia Sh. bilioni 26 kwa mwaka 2025/2026.

Kunenge amesema kuwa mafanikio hayo yameiwezesha Halmashauri kuendelea kutekeleza miradi ya kimkakati inayoboresha maisha ya wananchi katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya maji.

Kunenge amesema matumizi sahihi ya rasilimali na uwekaji wa vipaumbele vinavyozingatia mahitaji ya wananchi ndiyo msingi wa maendeleo endelevu na kuongeza pato la Taifa.

      Madiwani wa Baraza la Madiwani ya Kibaha wakiwa katika kikao chao kilichofanyika Juni 18/2026.

"Mkijiwekea vipaumbele sahihi kwa kuzingatia Dira ya 2020/2050 mtakuwa salama kwa mambo mawili, kwanza ni  kupata Hati Safi na kuwa na mipango endelevu yenye manufaa kwa wananchi amesa,"  Kunenge.

Aidha, Kunenge ameipongeza menejimenti ya Manispaa ya Kibaha kwa kuonesha ukomavu na uwajibikaji katika kushughulikia hoja za ukaguzi, ambapo tayari hoja 18 kati ya 23 zilizokuwa zinahitaji majibu zimefanyiwa kazi.

Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Mkoa, Mkoa wa Pwani umeendelea kufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato na tayari umevuka lengo kwa asilimia 111, huku Halmashauri ya Chalinze ikiongoza, Manispaa ya Kibaha ikishika nafasi ya pili na Halmashauri ya Mkuranga nafasi ya tatu.

Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Mawazo Nicas, amesema Halmashauri imepokea maelekezo yote yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa na itaendelea kuyafanyia kazi kwa kuongeza uwekezaji katika miradi ya kimkakati pamoja na kuimarisha ukusanyaji wa mapato.

        Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Mawazo Nicas katika Baraza maalum la kujibu hoja za CAG lililofanyika Juni 18/2026.

Nicas amesema miongoni mwa mipango inayoendelea kutekelezwa katika Manispaa hiyo ni ujenzi wa shule mbili za sekondari za ghorofa katika kata za Pangani na Tumbi, miradi ambayo inalenga kupanua fursa za elimu kwa watoto wa Manispaa hiyo.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha, Dkt. Rogers Shemwelekwa, amesema menejimenti itaendelea kushughulikia hoja tano zilizobaki ili kuhakikisha Halmashauri inafikia viwango bora vya usimamizi wa fedha na utendaji.

       Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa katika kikao cha Baraza maalum la kujibu hoja za CAG lililofanyika Juni 18/2026.

Diwani wa Kata ya Kibaha Omary Bura ameipongeza Manispaa ya Kibaha kwa kazi yake kwani hoja zilikuwa 23 lakini zimefanikiwa kujibiwa hoja 18 na bado hoja tano lakini jambo la kujibu hoja ni la kitaalam .

Bura amesema ni matumaini yake kuwa hoja tano zilizobaki zitajibiwa kufuatia vielelezo halisi na majibu yake yatapelekwa mezani kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa wakati.

Amesema anaungana na maoni ya hoja zilizotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) lakini pia anaunga mkono taarifa ya uwasilishaji iliyotolewa na Sekretarieti ya Manispaa ya Kibaha.

Hata hivyo,baraza hilo maalum limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, wakaguzi wa hesabu za Serikali kutoka Mkoa wa Pwani, madiwani, wataalam wa Halmashauri pamoja na viongozi wa vyama vya siasa.
 

No comments