HEADER AD

HEADER AD

DC TARIME AMWAGIZA OCD KUHAKIKISHA ANAKAMATWA BABA ALIYEMFANYIA UKATILI BINTI YAKE WA KAMBO

Na Dinna Maningo, Tarime

MKUU wa wilaya ya Tarime Kanali Michael Mtenjele, amemwagiza Mkuu wa Polisi wilaya Tarime, SSP Ramadhani Sarige kuhakikisha anakamatwa baba wa kambo aliyekuwa akimbaka binti yake wa kambo mwenye umri wa miaka 11 ili afikishwe kwenye vyombo vya sheria.

Kanali Michael ametoa agizo hilo katika kikao cha Baraza la Madiwani halmashauri ya mji Tarime kilichofanyika Mei, 17,2023 huku akishangazwa kuona Jeshi la Polisi kutofanikiwa kumkamata licha ya kufahamu tukio hilo la baba kumfanyia ukatili mwanae.

    Mkuu wa wilaya ya Tarime Kanali Michael Mtenjele

"Tulipata changamoto ya binti aliyekuwa akiishi na mama yake na baba wa kambo, wale baba na mama ni walevi wanaenda kwenye pombe wanarudi usiku. Mama anakuwa kalewa baba anaingia kwenye chumba cha binti wa miaka 11 na kujifanyia mambo yake.

"Baba anamfanyia ukatili, mtoto akaripoti kwa mama yake, mama yake akamwambia utajuana na awala yako, yaani amekuwa awala yake ambaye ni mme wake yeye.

"Yule mtoto alipofanyiwa vitendo vile na baba yake wa kambo alienda kwa baba yake mzazi napo akatumikishwa, tukachukua hatua kumnusuru akapelekwa kwenye nyumba salama kule Kituo cha Masanga walau akae kwenye uangalizi.

DC Michael ameongeza kusema" Niliagiza Polisi wachukue hatua kwa yule baba lakini bahati mbaya walienda siku moja wakamkosa na mpaka leo hawajamkamata.

" OCD nataka nipate taarifa za awali kujua huyo mtu amekamatwa na hatua za kisheria zimechukuliwa" amesema Michael.

Mkuu huyo wa wilaya amesema kwa sasa Tarime siyo salama kutokana na kuwepo mmomonyoko wa maadili katika jamii.

Amesema kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya imechunguza mwenendo wa maadili katika jamii na kubaini vitendo vya mmomonyoko wa maadili wakiwemo watoto kujihusisha na vitendo viovu.

"Kuna tatizo la mmomonyoko wa maadili katika jamii, mwezi uliopita iliundwa kamati, kamati ya ulinzi na usalama ilifanya uchunguzi kuona mwenendo wa maadili katika jamii.

"Kamati ilikuja na majibu ambayo kimsingi hatuko salama sana watoto kadhaa wanajihusisha na vitendo viovu. 

DC Michael ametoa wito kwa Madiwani na Watendaji wa Kata kulichukulia swala hilo kwa umuhimu kushirikiana kuelimisha jamii ili kuzingatia malezi bora kwa watoto.

Amesema endapo kuna tatizo watoe taarifa mapema kwani mmomonyoko wa maadili huanzia kwenye jamii au familia hivyo ni vyema suala hilo likatazamwa kwa ukaribu ili kuondokana na uvunjifu wa maadili.




No comments