DC SERENGETI AMPONGEZA NYANSAHO KUWAPATIA CWT MAJIKO 190 YA GESI
Na Mwandishi Wetu, Serengeti
CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT) wilayani Serengeti mkoani Mara kupitia kitengo cha wanawake kimefanikiwa kuwezesha upatikanaji wa majiko 190 kutoka kwa mdau wa maendeleo Rhimo Nyansaho.
Mkuu wa wilaya ya Serengeti Dkt. Vincent Mashinji amewapongeza wadau mbalimbali wa maendeleo kwa kutoa misaada yao katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo wilayani Serengeti ambapo ametoa wito kwa wakazi wa Serengeti kuchangia maendeleo katika wilaya hiyo.
Akikabidhi majiko hayo ya gesi kwa walimu wawakilishi mahala pa kazi kutoka shule 190 za Msingi na Sekondari Dkt.Vincent amempongeza Nyansaho kwa kushirikiana na Taifa gesi kwa kutoa majiko hayo ya gesi.
Mkuu wa wilaya ya Serengeti Dkt. Vincent Mashinji akikabidhi majiko ya gesi.
" Tunawashukuru Nyansaho na Taifa gesi kwa kutoa msaada huo, tunaomba ituletee na gesi zingine ikiwezekana mtusaidie na kwenye magereza kuweka gesi ili tupunguze uharibifu wa mazingira.
" Majiko 190 yatasaidia sana, kama kuna mzaliwa wa Serengeti yupo huko ana nia ya kuleta maendeleo mimi niambieni nitamfuata. Pale tunapopata vijana ambao wanapenda kutuletea maendeleo tupunguze Ruelue Rwembowe( maneno ya kukatisha tamaa) amesema Dc Mashinji.
Dc Mashinji amesema gesi hizo zitasaidia katika uhifadhi wa mazingira na kuokoa muda wa walimu katika kujipatia chakula wawapo shuleni.
Naye Mwenyekiti wa CWT wilaya ya Serengeti Mwl.Lusawi Mayala amekipongeza kitengo cha walimu wanawake kwa kuomba msaada wa majiko na kuhakikisha yanapatikana.
Mwl. Lusawi amewakumbusha walimu waliofaidika na msaada huo wa majiko kwamba majiko hayo ni zana za kufundishia hususani katika kuelimisha wanafunzi juu ya nishati safi na faida za matumizi ya nishati hiyo ili kuondokana na uharibifu wa mazingira.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa CWT wilaya ya Serengeti kitengo cha wanawake Mwl.Rahabu Mgesi amesema’’Katika ziara tulibaini walimu wengi wanakaa nje na vituo vya kazi, ili kuleta ufanisi katika majukumu yao tukaona ipo haja ya kutafuta majiko ya gesi ili kuweza kuharakisha walimu kupata chai wawapo shuleni’’.
Katibu CWT Mkoa wa Mara Susane Shesha amemshukuru Nyansaho kwa namna alivyojitoa katika kutoa msaada wa majiko hayo ya gesi, amewataka walimu kutunza majiko hayo ili yaweze kudumu.
Awali akisoma risala kwa mgeni Rasmi katibu wa CWT kitengo cha wanawake Mwl.Grace Mutaengerwa amesema;
‘’Kitengo cha walimu wanawake kwa kutambua michango ya walimu katika kuinua kiwango cha elimu na uhifadhi mazingira kiliwasilisha maombi yao ya msaada wa kupatiwa majiko ya gesi kwa mdau wa elimu Rhimo Nyansaho,mdau huyu kwa kushirikiana na Taifa gesi wamewezesha shule zote 190 kupata majiko ya gesi’’amesema Mwl Grace.
Hafla hiyo fupi ilijumuisha viongozi mbalimbali wa Serikali,Chama cha walimu Mkoa wa Mara na Serengeti, pamoja na taasisi mbalimbali zilizopo wilayani Serengeti.
Post a Comment