MBUNGE MATHAYO AWAHAKIKISHIA WANANCHI SOKO LA MWISENGE LILILOTELEKEZWA KUANZA KUTUMIKA
>> Soko hilo lilianzishwa miaka 19 iliyopita na kutelekezwa
>> Mbunge Mathayo asema halmashauri imetenga Milioni nane kuboresha soko
>>Wananchi wampongeza Mbunge kutatua kero ya ukosefu wa Soko.
>> Soko kuanza kutumika mwezi Septemba
Na Jovina Massano, Musoma
KILIO cha wananchi cha ukosefu wa huduma ya soko Kata ya Mwisenge kutatuliwa Mwanzoni mwa September 2023.
Soko hilo lililoanzishwa takribani miaka 19 iliyopita ikiwa ni moja ya miradi ya maendeleo katika kata hiyo na sasa huduma hiyo kuanza rasmi mara baada ya kukamilika kwa miundombinu ya choo na umeme September mwaka huu.
Hayo yameelezwa hivi karibuni katika ziara ya Mbunge wa Jimbo la Musoma Mjini Vedastus Mathayo kwa kuwahakikishia wakazi wa Kata hiyo kuwa tayari halmashauri imetenga kiasi cha Tsh. Million nane.
Fedha hizo ni kwa ajili ya ujenzi wa choo kitakachotumiwa na wafanyabiashara wa eneo hilo ili kuwapunguzia adha waliyonayo wananchi ya kwenda umbali mrefu kupata mahitaji yao.
"Mimi binafsi nitawawekea umeme kwenye majengo yaliyopo ili kuweka usalama nyakati za jioni mwanga uwepo wa kutosha na tutawaruhusu wale waliokuwa wameanza kujenga vibanda vya biashara waviendeleze na hapo tutakuwa tumelianzisha soko moja kwa moja na tayari nitakuwa nimetegua kitendawili cha Wakazi wa Kata ya Mwisenge cha muda mrefu" amesema Mathayo.
Ameongeza kuwa tayari ameshakutana na uongozi wa serikali za Mtaa kuanza kusimamia ujenzi wa choo ili kikamilike kwa wakati kabla ya mwezi ujao (September).
Wakiongea na Mwandishi wa DIMA ONLINE wakazi hao wamemshukuru kiongozi huyo kwa kuwasikiliza na kutoa maelekezo ya awali ya utekelezaji kwa viongozi wa Kata na mtaa.
Nae Pracseda Patil mkazi wa Zahanati amempongeza mbunge kwa hatua hiyo kwani ililazimu kutembea mwendo mrefu kutafuta mahitaji kwenye masoko ya Kata za jirani.
Amesema kwamba hatua hiyo itasaidia pia uwepo wa mzunguko wa fedha na kupata maendeleo.
Ameongezea Scholastica Wariana mkazi wa Mtakuja A wa Kata hiyo kuwa uanzaji wa soko utasaidia akina mama kwakuwa mahitaji yatapatikana karibu lakini pia wataanzisha biashara na kujiajiri wenyewe na kukuza vipato kwa kuwa hivi sasa wanawake ndio wahanga wakubwa wa kulea familia.
"Sisi wanawake wa maeneo haya tunampongeza sana mbunge kwa kuliona hili kwa jicho la upekee kwani ajira zitapatikana kwenye ulinzi,usafi, kuajiri wauzaji na kujiajiri na tayari serikali inaongeza chanzo kipya cha mapato na kukuza uchumi na kuongeza maendeleo kwa wananchi na kwa Taifa"amesema Scholastica.
Nao wafanyabiashara wa Dagaa katika maeneo hayo Sara Ndalo na Tausi Hamisi wamemuomba Mwenyekiti wa serikali za mitaa wa mtaa wa Sokoni George Faustine Mtete kuchangamkia fursa hiyo kwa kuanza utekelezaji wa maelekezo ya mbunge ili eneo hilo lililotengwa tangu mwaka 2004 kwa ajili ya soko lianze shughuli mara moja mwezi ujao kama alivyoelekeza kiongozi huyo.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wa Kata hiyo Mbogo Mnyugu amesema kuwa uanzishwaji wa soko hilo utajibu upatikanaji wa ajira mpya na maendeleo ya Kata na huo ndio utekelezaji wa ilani ya chama kwa vitendo .
Taarifa ya soko hilo lililokuwa limetelekezwa muda mrefu ililipotiwa na mwandishi wa DIMA ONLINE October 13 ,2022.
Post a Comment