DC CHIKOKA : UTHAMINI ULIOFANYIKA HAUNA UHUSIANO NA SERIKALI YA RORYA
>>Asema Serikali ya Rorya haijataka kuwadhulumu ardhi wananchi wa Kitongoji cha Begi na Kiwandani.
>>Asema waliofanya uthamini vitongoji jirani na shamba la Mifugo la Utegi siyo Serikali ya Rorya ni watu wengine wenye shamba.
>> Awapoza wananchi na kusema watalipwa fidia ya ardhi kwa mahesabu yatakayofanyika.
>>Awali akizungumza na wananchi DC Chikoka aliwaambia kuwa Serikali imeona wana haja ya hilo eneo kwa ajili ya kuliendeleza kwa maendeleo ya Rorya na wananchi kwa ujumla.
Na Dinna Maningo, Rorya
SERIKALI ya Wilaya ya Rorya Mkoani Mara imesema kuwa uthamini uliofanyika katika baadhi ya Vitongoji Kata ya Bukwe na Koryo kikiwemo Kitongoji cha Begi na Kiwandani ili kupisha uendelezaji wa shamba la mifugo la Utegi hauhusiani na Serikali ya Wilaya hiyo.
Akizungumza na Mwandishi wa DIMA Online, Mkuu wa Wilaya ya Rorya Juma Chikoka alikanusha habari iliyoripotiwa katika chombo hiki cha habari Julai, 28, 2023 yenye kichwa cha habari kisemacho' WAANDAMANA OFISI YA CCM KUILALAMIKIA SERIKALI YA RORYA KUTAKA KUWADHULUMU ARDHI'.
Habari hiyo ilihusu Wananchi wa Kitongoji cha Begi na Kitongoji cha Kiwandani Kijiji cha Majengo Kata ya Koryo katika Wilaya hiyo, ambao Julai, 27, 2023 majira ya asubuhi waliandamana na kufika ofisi ya Chama cha Mapinduzi CCM wilaya ya Rorya.
Wanachi walifika ofisini ili kutoa kero zao dhidi ya Serikali ya wilaya yao kutaka kuwadhulumu ardhi kwa kutowatendea haki katika zoezi la uthamini wa fidia baada ya wathamini kukataa kuwa ardhi haitapimwa wala kulipwa fidia na badala yake uthamini utakaofanyika ni wa maendelezo ya vitu vilivyopo juu ya ardhi.
Hata hivyo, hawakufanikiwa kueleza kero zao baada ya kukuta milango ya ofisi ya Chama hicho ikiwa imefungwa kwa kufuli.
Mkuu huyo wa Wilaya hiyo alimwambia Mwandishi wa DIMA Online kwamba;
" Stori uliyoripoti kuwa Serikali inataka kuwadhulumu wananchi ardhi imezua taharuki. Nikwambie kitu kimoja katika hizi kazi sisi tunapambana kubeba taswira chanya ya Rorya.
"Hii ishu uliyosema Serikali kudhulumu ardhi hili jambo halihusiani na Serikali, jukumu langu ni kusimamia amani na utulivu, hilo shamba wanaofanya uthamini siyo Wilaya ya Rorya, wanaofanya uthamini ni watu wengine ni wenye shamba.
Ameongeza " Sisi kama Serikali jukumu letu ni kusimamia usalama na amani, lile eneo linamilikiwa na watu wengine, kwahiyo nilichotaka nikwambie hilo jambo la uthamini halina uhusiano wowote na Serikali ya Wilaya.
"Kwahiyo kama una nukuu usinukuu kitu ambacho hauna uhakika, nikutakie kila la kheri kwenye majukumu yako lakini uwe makini" amesema DC Chikoka.
Mwandishi wa DIMA ONLINE alimuuliza Mkuu huyo wa Wilaya ni vigezo gani alivyotumia kuthibitisha kuwa habari iliyoripotiwa imezua taharuki, kwani Mwandishi wa habari hajapata malalamiko kutoka kwa wananchi au viongozi wengine wa Serikali kwamba habari zinazoripotiwa kuhusu malalamiko ya zoezi la uthamini kwa wananchi wanaoishi karibu na shamba la mifugo ambalo kuna kiwanda cha maziwa zimezua taharuki.
Simu iliyopigwa ya malalamiko kuwa habari imezua taharuki ni ya mkuu wa wilaya pekee aliyedai kuwa habari imezua taharuki kwamba amepigiwa simu na watu wengi akiwemo Waziri mkuu.
Mkuu huyo wa Wilaya licha ya kusema kuwa Serikali haihusiki na uthamini na kwamba uthamini unafanywa na wenye shamba hakuweza kutaja wazi nani mmiliki wa shamba hilo la mifugo na kiwanda cha maziwa, na nani mwekezaji.
Julai, 27, 2023, Mwandishi wa DIMA ONLINE akiwa katika Kitongoji cha Begi na Kiwandani akifuatilia mgogoro wa wananchi na Serikali ya Rorya wakiilalamikia Serikali kutowatendea haki katika uthamini. Punde si punde mkuu huyo wa Wilaya aliwasili shule ya msingi Utegi.
Mkuu huyo wa Wilaya akiwa ameambatana na Kamati ya ulinzi na usalama alifika katika shule hiyo iliyopo Kitongoji cha Begi na kuzungumza na baadhi ya wananchi waliokuwa wakizungumza na DIMA ONLINE kuhusu zoezi la uthamini.
Mkuu huyo wa Wilaya aliwapoza wananchi na kuwataka wakubali kufanyiwa uthamini na ikiwezekana ufanyike ndani ya siku mbili.
Alisema kwamba kuhusu uthamini wa ardhi wananchi watalipwa fidia ya ardhi kwa kufanyiwa mahesabu. Wananchi walitekeleza kauli ya mkuu wa wilaya na kukubali kufanyiwa uthamini.
"Jambo la msingi ambalo nataka nilizungumze ni kwamba utatuzi wa changamoto unahitaji ushirikiano lakini kutumia namna nyingine ya kutatua changamoto mara nyingi huwa haisaidii hata hatma yake hakuna.
"Mimi napenda sana kushirikiana na wananchi kwasababu ninyi ndio wana Rorya bila ninyi mimi nisingekuwepo, mimi nikipata jambo napenda kwanza nikae na wananchi au viongozi tushirikiane ndiyo maaa nimekuja niwasikilize" alisema DC Chikoka.
Mkuu huyo wa Wilaya alisema kuwa lengo la Serikali siyo wananchi wapate shida lakini mara nyingi Serikali huwa inafanya vitu kwa mipango endelevu na maslahi ya wananchi lakini pia na maslahi mapana ya Serikali.
" Kwa hiyo Serikali imeona wana haja ya hilo eneo ili kuliendeleza kwa ajili ya maendeleo ya Rorya na wananchi kwa ujumla, ni sawa sawa na yanayofanyika kwenye maeneo mbalimbali, tuliona Tarime na kwingineko, kwahiyo na hapo Serikali ina mpango napo" alisema DC Chikoka.
Akizungumzia kikao kilichoketi Julai, 14, 2023 na viongozi wa kata kunakofanyika uthamini pamoja na viongozi wa Serikali amesema;
" Tulipata fursa ya kukaa kikao cha pamoja na viongozi wa Chama, Viongozi wa Serikali na wenye shamba wenyewe, pamoja na watu wa Wizara, timu ilikuwa kubwa akiwemo Mbunge, Mwenyekiti wa CCM na Katibu wa CCM wilaya, Madiwani wa Kata ya Koryo na Bukwe,Wenyeviti wa Vitongoji na Vijiji , Watendaji, lengo lilikuwa kuendelea kushirikiana.
"Tulizungumza na hatua zinazotakiwa katika uthamini, swali lilikuwa uthamini unafanyikaje kwa utaratibu gani? Tukatoa ufafanuzi uthamini unafanyika wa kulipa fidia, lakini hapo awali lugha ilikuwa inatumika kuwa wanaenda kulipwa kifuta jasho .
"Lakini nikasema hapana hao ni wana Rorya lazima walipwe kwa mujibu wa taratibu kwahiyo hiyo lugha ikafutwa. Fidia itapatikana kwenye maendelezo kama mtu kajenga nyumba, ana mazao atalipwa kwa mujibu wa sheria.
Amesema fidia ya ardhi italipwa kulingana na mahesabu yatakayofanywa kutokana na ardhi waliyopo ambapo aliwaomba wananchi watoe ushirikiano na waruhusu zoezi la uthamini liendelee vyema kama lilivyoanza kwenye vitongoji vingine.
"Niwaombe kama tulivyofika hapa na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama, yupo DAS, Mkurugenzi , Kaimu Afisa Elimu na timu nzima naomba mfanyiwe uthamini.
"Wathamini walipita wakakosa ushirikiano wapeni ushirikiano wakifika wakute mpo, ikiwezekana zoezi hili lifanyike ndani ya siku mbili wananchi mkae kwenye nyumba zenu, kama awali walipita hamkuwepo zoezi hilo litarudiwa
DC Chikoka aliwahakikishia wananchi kuwa fidia ya ardhi ipo ila uthamini wake utafanyika baadae ambapo kwenye ardhi watafanya asilimia.
Kauli hiyo ya DC iliwapa kigugumizi wananchi kutoakana na kauli ya awali ya wathamini kuwahakikishia kuwa hawatafanyiwa uthamini wa ardhi isipokuwa maendelezo vitu vilivyo juu ya ardhi kwakuwa wananchi wa Vitongoji hivyo ni wavamizi walivamia na kuishi kwenye shamba la mifugo la Utegi kauli iliyopigwa na wananchi wakisema wao si wavamizi .
Katika mkutano huo Serikali ya Rorya ilimzuia Mwandishi wa Habari wa DIMA ONLINE kupiga picha ambapo ilimwamuru kufuta picha alizokuwa amepiga huku mwandishi wa habari mwingine aliyekuwepo kwenye mkutano huo yeye hakuzuiliwa, aliendelea kupiga picha hadi kuhitimishwa kwa mkutano.
Mwandishi alipohoji sababu za kuzuiliwa kupiga picha mkutano wa wazi wa wananchi ambapo pia alikuwa akitekeleza majukumu yake kikatiba kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 18, Serikali hiyo haikutoa sababu huku ikisema kuwa mwandishi aliyekuwa akipiga picha hakuzuiliwa kwakuwa alikuwa Mwandishi maalum.
Rejea
>>> Mei, 18, 2023, Mkuu wa wilaya ya Rorya, Juma Chikoka akiwa kwenye mkutano wa wananchi wa Vijiji saba vinavyozunguka shamba la mifugo lenye kiwanda cha maziwa uliofanyika Kijiji cha Nyasoro alinukuliwa katika vyombo vya Habari.
Mkuu huyo wa wilaya alinikuliwa akiwaambia wananchi kuwa kila mtu ambaye ardhi yake itatwaliwa na kuingizwa kwenye mradi wa kufufua shamba hilo atalipwa fidia stahiki.
Dc Chikoka alisema shamba la mifugo la Utegi lina ukubwa wa ekali 4,400 kati ya hizo ekali 400 zinadaiwa kuwa ni makazi ya watu, mashamba na malisho ya mifugo katika vijiji hivyo.
>>>Awali akizungumza na DIMA Online MBUNGE wa Jimbo la Rorya mkoani Mara, Jafari Chege alisema kuwa Wananchi wa Kitongoji cha Begi na Kitongoji cha Kiwandani,katika Kijiji cha Majengo, Kata ya Koryo hawawezi kupimiwa ardhi kwakuwa wanaishi kwenye ardhi yenye hati.
Mwandishi wa DIMA Online alizungumza na mbunge huyo kuhusu malalamiko ya wananchi wa Vitongoji hivyo wakiilalamikia Serikali kuendesha zoezi la uthamini wa maendelezo kwenye ardhi huku ikiacha kupima ardhi kwa madai kuwa wananchi walivamia na kuishi kwenye eneo la Serikali la shamba la mifugo (Utegi Dairy Farm) kama ilivyoripotiwa katika chombo hiki cha habari Agasti, 04, 2023.
>>> Desemba, 2018 Serikali ya awamu ya tano iliyoongozwa na Rais Hayati John Pombe Magufuli kupitia aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Mara, Adam Malima ilikabidhiwa Hati za shamba la mifugo na kiwanda cha maziwa kutoka kwa Otieno Igogo aliyekuwa Mkurugenzi wa Kampuni hiyo baada ya kushindwa kuliendeleza huku Mifugo na mali zingine kutojulikana ziliko.
Aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Mara, Adam Malima wa pili kulia akipitia nyaraka mbalimbali baada ya kupokea Hati za umiliki shamba la mifugo kutoka kwa Mkurugenzi wa UDAFCO Otieno Igogo (aliyesimama) wa tatu kulia ni aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Rorya Simon Chacha na wa kwanza kushoto ni aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Rorya Lameck Airo (Picha na Mtandao).
Igogo alipigwa faini na kodi kwa kushindwa kuliendeleza shamba na kiwanda huku kampuni hiyo ikiwa na mgogoro na vijiji sita vilivyokuwa na umiliki wa shamba hilo.
Serikali ya mkoa wa Mara kupitia aliyekuwa mkuu wa mkoa huo, Adam Malima wakati akikabidhiwa Hati alimuomba Rais Hayati Magufuli, kuwa shamba hilo wapewe vijiji sita vilivyounda Chama cha UMON FARMERS DEVELOPMENT ASSOCIATION (UFADA), kupitia Wizara ya Uwekezaji, Viwanda, na Biashara, Wizara ya mifugo, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) wapate Mwekezaji.
Hadi sasa UMON haikurejeshewa Hati ya shamba na kiwanda cha maziwa na haijabainika wazi nani mmiliki wa shamba hilo, nani mwenye Hati ya shamba wala nani anayetaka kuwekeza katika shamba hilo kutokana na Serikali kutobainisha wazi uhalali wa shamba hilo huku shamba likiendelea kulindwa na askari wanaodaiwa ni wanajeshi wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Inaelezwa kuwa ni zaidi ya miaka 20 tangu Serikali ibinafsishe shamba hilo kwa vijiji 6 ambapo Kijiji cha Majengo kiliongezwa baada ya kugawanywa Kijiji cha Utegi na kuwa Vijiji 7.
Vijiji hivyo ni Kijiji cha Utegi, Mika, Omuga, Nyanduga,Nyasiro, Ingiri na Majengo vilivyo jirani na shamba la Mifugo la Utegi vilivyounda umoja uuitwao UMON FARMERS DEVELOPMENT ASSOCIATION (UFADA) iliyosajiliwa mwaka 1995.
Imeelezwa kuwa UMON ilinunua shamba hilo lililokuwa linamilikiwa na DAFCO kutoka serikalini baada ya kulibinafsisha kwao na kisha UMON ikaweka mwekezaji katika shamba hilo Kampuni ya UDAFCO ambayo iliingia makubaliano ya hisa 51 kwa UMON mwaka 1998, UDAFCO ilipata Hati ya umiliki kati ya mwaka 2001/2002.
Kampuni ya UDAFCO ilingozwa na aliyekuwa Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Otieno Igogo. Hata hivyo uwekezaji huo ulisuasua kwa zaidi ya miaka 20.
Mwaka 1997 aliyewahi kuwa Waziri wa Kilimo na Ushirika, Paul Kimiti wakati akiwasilisha Bungeni hotuba ya wizara hiyo ya makadilio na matumizi ya fedha kwa mwaka 1997/1998,wakati huo Waziri mkuu akiwa ni Frederick T. Sumaye, Waziri huyo alisema Wizara ilikubaliana na Tume ya Rais ya kurekebisha mashirika ya umma (PSRC) kupendekezwa utaratibu wa kununua hisa katika shamba la mifugo la Utegi.
Hisa hizo ni kwa wananchi ambao maskani yao yapo karibu na shamba hilo ikiwa ni katika kufanikisha urekebishaji na ubinafsishaji wa mashirika yaliyo chini ya Wizara hiyo ambapo wananchi waliunda Chama cha UMON kilichofanikiwa kununua shamba hilo na kupata mwekezaji Kampuni ya UDAFCO.
Hata hivyo Kampuni hiyo iliingia mgogoro na UMON baada ya kukiuka makubaliano zikiwemo hisa jambo lililopelekea Serikali kuchukua hati ya umiliki kutoka kwa Mkurugenzi wa UDAFCO.
...... Itaendelea
Post a Comment