HEADER AD

HEADER AD

RAIS MWINYI ASISITIZA AMANI NCHINI

Na Andrew Chale, Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt Hussein Ali Mwinyi amesisitiza suala la Amani na kulinda maadili ya Mzanzibar kwani jambo hilo ni jema kwa maendeleo na ukuaji wa nchi.

Rais Dkt Mwinyi amesema hayo Septemba 3, 2023 katika dua maalum ya kumuombea pamoja na kuombea nchi kuwa na amani iliyoandaliwa na Wananchi katika eneo la Kaskazini A, kwenye msikiti wa Ijitimai, Kidoti Kaskazini A, Zanzibar. 

Akizungumza katika dua hiyo, Dkt Mwinyi amesisitiza wananchi kuendelea kuwa pamoja na mashirikiano kwa kufuata misingi ya dini ya Kiislamu ambayo itawasaidia kulinda maadili na kuepuka vivunjifu vya amani.


"Tuwe na amani, tuwe na umoja na tuwe na mshikamano kwa umoja wetu. Nchi ikikosa amani, hakuna lingine lolote linaloweza kufanyika.

Hivyo tunaomba tuendelee kuliombea dua taifa letu ili amani idumu." Amesema Rais Dkt Mwinyi 

Ameongeza kuwa "Amani tunayo, umoja upo, hili linapaswa kushukuriwa huku akitaka jambo hilo la dua kufanyika mara kwa mara.

"Nashukuru kwa dua hii, nimefarijika sana kwa kutuombea sisi viongozi ili kutimiza yale tulioahidi kutimiza.

Nitajitahidi kipindi kilichobakia, yale yote niliyotolea ahadi, nifanikiwe na kuendeleza kutimiza zaidi na zaidi." Amesema Rais Dkt Mwinyi. 

Aidha, amesisitiza suala la la Maadili mema kwani kumekuwa na mmong'onyoko wa Maadili ikiwemo uzalilishaji na matumizi mabaya ya madawa ya kulevya.

"Zipo dalili za mmong'oko wa maadili kwa udhalilishaji, madawa ya kulevya.

Maadili haya yaanzia ngazi ya familia, tunatakiwa kuwalea vijana wetu kwa maadili ya kiisilamu, hii itasaidia hata jamii kujiondoa katika maadili mabaya." Amesema Rais Dkt Mwinyi.

Nae Waziri wa Katiba na Sheria,  Harun Ali Suleiman ameomba jambo hilo liendelezwe na maeneo mengine katika kuhakikisha nchi inakuwa na maadili mema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja,  Ayub Mohammed Ahmoud ameshukuru kwa wananchi hao kumuandalia Rais dua maalum kwani ni jambo jema na ishara nzuri ya utendaji kwa Rais Dkt Mwinyi ambaye ameweza kupeleka maendeleo mbalimbali ndani ha Mkoa huo na Zanzibar kwa ujumla. 

Mkuu wa mkoa huyo, amesema kuwa, watu zaidi ya 6000 wameshiriki dua hiyo kutola maeneo mbalimbali ya Mkoa Kaskazini Unguja .

"Tunafarijika sana, Madrasa 250 zimetoa Wanafunzi na Walimu wao na kufanya idadi ya 3,000.

Ameongeza " Maimamu 700 kutoka misikiti ya ndani ya mkoa huu na wananchi wa maeneo yote wapo hapa, si jambo dogo na mimi nimefarijika sana." Amesema Ayub.


No comments