MWENYEKITI WA KIJIJI ACHOMWA KISU, MWINGINE AKATWA MAPANGA NYAMONGO
Na Mwandishi Wetu, Tarime
MWENYEKITI wa Kijiji cha Matongo Kata ya Matongo-Nyamongo wilaya ya Tarime mkoani Mara, Daud Itembe amejeruhiwa kwa kuchomwa kisu mkononi na mtu mmoja ambaye bado hajafahamika jina lake akiwa barabarani akielekea nyumbani kwake.
Pia mkazi mwingine wa Kijiji hicho Vincent Maningo amejeruhiwa kwa kukatwakatwa mapanga wakati wakiwa barabarani akielekea nyumbani.
Majeruhi hao waliofanyiwa tukio la uhalifu siku moja kwa nyakati tofauti Septemba, 02, 2023 saa tano usiku wamelazwa katika Kituo cha Afya cha Nyangoto maarufu (Sungusungu) wakiendelea na matibabu.
Wakizungumza na Mwandishi wa Habari wa DIMA Online aliyefika katika Kituo hicho cha Afya wameeleza tukio lilivyokuwa.
Daud Itembe amesema" Nilikuwa kwenye usafiri wa pikipiki mida ya saa tano usiku nikielekea nyumbani kwangu ghafla akatokea mtu mbele yetu akiwa ameshika kisu mkononi, yule mwenye pikipiki akaruka akakimbia mimi nikandondoka chini na pikipiki.
"Akanichoma kisu mkononi, ile anataka kunichoma kisu mara ya pili nikajihami kwa kupiga risasi hewani akakimbia, sijamfahamu kwa jina. Damu zilivuja sana nikaletwa hospitali, naendelea na matibabu nasikia maumivu makali kama unavyouona mkono" amesema Mwenyekiti.
Naye Vincent Maningo mwenye miaka (45) amesema kwamba akiwa barabarani akielekea nyumbani mida ya saa tano usiku alivamiwa na watu watatu ambao aliwatambua kwa sura na kisha kumkatakata mapanga wakisema ni kibaka.
Vincent Maningo
" Ilikuwa saa tano usiku nikiwa karibu na Grosari ya Bokobora Kirindo maeneo ya Bomgeti nikielekea nyumbani walifika vijana watatu wakaniambia wewe ni kibaka nikawaambia mimi siyo kibaka lakini wakanikomalia kuwa mimi ni kibaka.
"Wakanikatakata kwa mapanga kama unavyoona majeraha, mtu mmoja alifika akawaambia Vincent siyo kibaka nina mfahamu, akawaambia kama mnadhani ni kibaka mpelekeni Kituo cha Polisi.
" Wakanipeleka hadi Polisi tulipofika alikuwepo askari Polisi mmoja nikamwambia hawa walionileta ndiyo wamenikatakata mapanga, akawaambia Vincent siyo Kibaka na mmemleta hapa mkiwa mmeshampiga sana akawaambia mpelekeni hospitali akawapa PF3." amesema.
Amesema watu hao waliomkatakata mapanga waliongozana naye hadi Kituo cha afya wakitembea kwa miguu kisha kumtelekeza na wakaondoka na fomu namba tatu ya Polisi (PF3) na kwamba mpaka sasa hawajafika hospitali kujua hali yake.
"Tumetembea kwa miguu nikiwa na maumivu makali, wakanifikisha hospitali wakaniacha wakaondoka zao na PF3, sikupata huduma kwa wakati huo. Nimepata huduma baada ya kufika Mwenyekiti mstaafu wa Kijiji cha Nyangoto Bw. Ngocho aliyekuja kumuona Mwenyekiti wa Kijiji ndiyo akamwambia Nesi kwamba huyu ninamfahamu siyo kibaka.
"Nilihudumiwa kama unavyoona mida ya saa sita usiku baada ya hapo mpaka leo hii saa sita mchana sijapata huduma nyingine ya matibabu.
Mimi siyo kibaka tena bahati nzuri nikiwa kwenye Grosari tulikuwa na Mwenyekiti wa Kijiji aliyechomwa kisu alininunulia bia mbili, baadae nikaondoka zangu nikamwacha. Wakati nikiwa njiani ndipo nikakutana na hao vijana wakanikatakata na kunisababishia majeraha na maumivu makali" amesema.
Samwel Mariba mkazi wa Kitongoji cha Mnadani ndugu wa Vincent amesikitishwa kwa kitendo cha Polisi kuwaagiza waliomkata Vincent mapanga kumpeleka hospitali badala ya kuwaweka chini ya ulinzi kwa kosa la kujichukulia sheria mkononi.
"Watu wamemfanyia tukio mtu wanampeleka Polisi alafu haohao waliofanya tukio wanaambiwa wampeleke hospitali, hii ni hatari je huko njiani wangemdhulu au kumuua wakati ndio wamemjeruhi kwa mapanga wakimtuhumu ni kibaka! hii ndiyo sheria ya nchi yetu ? kwamba mhalifu ametenda kosa na amefika Polisi alafu yeye huyohuyo ampeleke hospitali mtu aliyemfanyia tukio hii siyo sawa" amesema Samwel.
" Nilipata taarifa leo saa tatu asubuhi nilipigwa simu na Yoel akinieleza Mwenyekiti wa Kijiji kukatwa mapanga nikafika hospitali nikamkuta na ndugu yangu.
"Nilipozungumza nao, walisema walikuwa njiani wanatembea wakakutana na vijana pale Bomgeti wakamuuliza nyie ndo mnaotuibia?akasema yeye sio mhalifu, wakati wa majibizano hayo wakamkatakata mapanga, hao hao wakampeleka Polisi, Polisi wakasema nyie mmemkata hatuwezi kumpokea labda tuwape PF3 mumpeleke hospitali wakampeleka na kumtelekeza.
"Nilimpigia simu Mkuu wa Kituo cha Polisi Nyamongo (OCS) akaniambia kwamba taarifa aliyopewa yeye aliambiwa ni kibaka, akasema kama si kweli majeruhi ni kibaka basi arudi kituo cha Polisi atoe maelezo ili afungue kesi wahusika wakamatwe.
Ameongeza" OCS akasema kama hajiwezi Daktari aongee na OCS amdhihirishie kama hawezi kufika kituoni basi Polisi ije kituoni kuchukua maelezo.
Amesema kuwa matukio ya watu kujichukulia sheria mkononi yakiwemo ya watu kuchomwa visu kukatwa mapanga yamekuwa yakitokea sana Nyamongo.
Post a Comment