TRA PWANI YAKUSANYA BILIONI 266
Na Gustaphu Haule, Pwani
MAMLAKA ya Mapato Tanzania(TRA) Mkoa wa Pwani imefanya kongamano la kuelekea katika maadhimisho ya miaka 30 ya kuzaliwa kwake huku ikieleza mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika kipindi hicho.
Mafanikio hayo yameelezwa na meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania ( TRA) Mkoa wa Pwani Peter Jackson wakati akifungua kongamano hilo lililofanyika Juni 23/2026 Katika Manispaa ya Kibaha.
Kongamano hilo liliwashirikisha wadau mbalimbali kutoka sekta binafsi na sekta za Umma, wakiwemo wamiliki wa viwanda,madereva bodaboda, viongozi wa dini, watumishi kutoka TRA,maafisa biashara,wafanyabiashara wadogo na Waandishi wa habari.
Meneja wa TRA Mkoa wa Pwani Peter Jackson akifungua kongamano la wafanyabiashara lililofanyika Juni 23/2026 Katika Manispaa ya Kibaha.
Katika kongamano hilo ,Jackson amesema moja ya mafanikio hayo ni kuongeza mapato ya Serikali ambayo yameongeza utoaji wa huduma za kijamii kama vile maji,afya ,elimu ,barabara na huduma nyingine.
Amesema TRA katika katika kipindi cha miaka 30 imefanikiwa kuvuka lengo la ukusanyaji wa mapato kwani katika kipindi cha mwaka 2015/2016 ilipanga kukusanya Sh. bilioni 23 lakini ilivuka lengo na kukusanya Sh.bilioni 27 lakini katika kipindi cha mwaka 2025/2026 TRA ilijiwekea lengo la kukusanya Sh.bilioni 235 lakini ilivuka lengo na kukusanya Sh.bilioni 266.
Jackson amesema mafanikio mengine ni pamoja na kuanzisha mifumo mbalimbali ya kimtandao ikiwemo malipo kwa njia ya elekitroniki ,kulipa na kusajili kupitia mfumo pamoja na kutoa risiti kwa njia ya simu janja hali ambayo imeondoa usumbufu kwa wafanyabiashara.
Amesema pia,katika kipindi hicho TRA imefanikiwa kuongeza kasi ya utoaji elimu kwa mlipa kodi hali ambayo imeongeza molari ya kulipa kodi kwa hiari na kwamba TRA itaendelea kutoa elimu katika eneo hilo.
Amesema mbali na hayo, lakini pia TRA imefanikiwa kuimarisha mazingira ya biashara kwani wafanyabiashara wameendelea kupata huduma ya TRA kirahisi sambamba na kuongeza uwazi na uwajibikaji.
Jackson amesema pamoja na mafanikio hayo lakini zipo changamoto mbalimbali ambazo TRA Mkoa wa Pwani imekuwa ikikabiliananazo ambazo ni pamoja na ukwepaji wa kodi unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara .
Baadhi ya wafanyabiashara na wadau mbalimbali wa kodi wakishiriki katika kongamano la miaka 30 ya kuanzishwa kwa TRA lililofanyika Juni 23/2026.
Amesema changamoto nyingine ni kufanyika kwa biashara haramu na magendo ambazo zinafanyika kwa kutumia stempu feki hali ambazo inachangia kukwamisha mapato ya Serikali.
Amesema kutokana na hali hiyo ,TRA Mkoa wa Pwani imejipanga kuhakikisha inaondoa biashara zote haramu na magendo pamoja na kusimamia maadili ya watumishi wa TRA kwa kuongeza uadilifu,uaminifu,uweledi na kuaminika ili kujenga ushirikiano kati ya TRA na mlipakodi.
Jackson,amewaomba wadau wa kodi kutoa ushirikiano kwa kuwabaini maafisa wa TRA ambao wamekuwa na tabia ya kuomba rushwa huku akiwaomba viongozi wa dini kuendelea kutoa elimu ya kulipakodi huku viongozi wa wafanyabiashara wahakikishe wafanyabiashara wanalipa kodi kwa hiari.
Pia,amewaomba wakala wa mashine za kutolea risiti za kieletroniki (EFD) watimize wajibu wao kwa kuwasaidia walipakodi kujua matumizi ya mashine hizo ikiwa pamoja na kuwafundisha namna ya kutoa risiti kwa kutumia simu janja.
Ametoa wito kwa wadau wote kuhakikisha kila anayetakiwa kulipakodi analipa sasa kwani mwisho wa kulipa kodi kwa mwaka 2025/2026 ni Juni 30/2026 japo anatambua wapo ambao wanalipa kodi kwa mwaka.
Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara Mkoa wa Pwani Said Mfinanga, imeipongeza TRA mkoa wa Pwani kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana ndani ya miaka 30 kwani awali kulikuwa na usumbufu mkubwa kwa wafanyabiashara lakini sasa hivi umeondoka.
Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara Mkoa wa Pwani Said Mfinanga akizungumza katika kongamano la miaka 30 ya kuanzishwa kwa TRA lililofanyika Juni 23/2026 katika Manispaa ya Kibaha.
Mfinanga,amesema kuwa kuondoka kwa usumbufu huo kumesaidia kuhamasisha walipakodi kulipa kodi kwa hiari na hivyo kupelekea kuongezeka kwa mapato huku akisema kwasasa wafanyabiashara wapo tayari kulipakodi bila kusukumwa.
Amesema uhusiano wa TRA na walipakodi ni mzuri kwani awali walikuwa wakisikia maafisa wa TRA wanakuja walikuwa wakikimbia na kufunga maduka lakini sasa hivi wamekuwa marafiki kwakuwa mazingira yameimarika na kuboreshwa zaidi.
Amesema anapendekeza katika miaka ijayo TRA iendelee kutoa elimu ya teknolojia ili kuendana na kasi ya mifumo iliyopo hivi sasa na elimu hiyo itolewe kwa wafanyabiashara ililenga masuala ya Sheria ya kodi.
Mbali na hilo lakini pia Mfinanga amesema kuwa TRA isogee zaidi katika jamii kwakufanya matukio mbalimbali ya kijamii ili kujenga ushirikiano, kuwaleta karibu wafanyabiashara pamoja na kupanua wigo kwa ongezeko la wafanyabiashara ili kuongeza ukusanyaji wa mapato.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa wa Pwani ( JWT) Abdallah Ndauka aliipongeza TRA kwa kazi nzuri kwani malalamiko mengi ya wafanyabiashara yamepungua lakini aliwaomba wasitegemee kukusanya mapato kwa mtindo wa adhabu.
Amesema anatamani kuiona TRA inakusanya mapato kwa njia halali na katika kufanikisha hilo ni vyema ikahakikisha wamiliki wa viwanda waliopo Mkoa wa Pwani wanalipa kodi ndani ya mkoa wa Pwani kwani kwasasa wengi wao wameanzisha viwanda Mkoa wa Pwani halafu mapato wanalipa Mkoa wa Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wafanyabiashara wadogo ( SHIUMA) Mkoa wa Pwani Philemoni Maliga ameipongeza TRA kwa mafanikio makubwa hususani katika ukusanyaji wa mapato kutoka Sh.bilioni 27 hadi kufikia Sh.bilioni 266.
Hata hivyo,Maliga ameiomba TRA kutoa elimu zaidi kwa walipakodi ili waweze kuongeza idadi ya walipakodi watakaosaidia kuongeza mapato ya Mkoa huku akisisitiza kujenga mahusiano mema kwani anaamini ikifanyika hivyo wafanyabiashara watakuwa wanalipa kodi kwa hiari.





Post a Comment