MAPANA AZINDUA SHINDANO LA KUTAFUTA VIPAJI VYA MAWAZO KWA VIJANA 100
Na Gustaphu Haule, Pwani
NAIBU Katibu Mkuu ,Ofisi ya Rais , Maendeleo ya Vijana Kedmon Mapana amezindua shindano la kutafuta vipaji vya mawazo mazuri kwa vijana 100 linalojulikana kwa jina la Vijana Uchumi Challenge ikiwa ni hatua ya pili ya muendelezo wa shindano hilo.
Mapana amefanya uzinduzi huo Juni 23/2026 katika chuo cha uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo kwa Mfipa Kata ya Kibaha katika Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Mkoa wa Pwani.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana Dkt.Kedmon Mapana akizungumza na Waandishi wa habari katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kibaha Mkoani Pwani mara baada ya kuzindua shindano la Vijana Uchumi Challenge Juni 23/2026.Uzinduzi huo ulishuhudiwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mkurugenzi wa uwezeshaji na uendeshaji vijana kibiashara kutoka Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana Edward Haule, Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Vijana Uchumi Challenge Josephu Malekela pamoja na majaji wa shindano hilo wakiongozwa na Profesa Neema Mboja kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Akizungumza katika uzinduzi huo Naibu Katibu Mkuu , Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana Kedmon Mapana amesema kuwa wazo hilo lipo katika utekelezaji na linakwenda vizuri.
Amesema anamshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kuanzishwa kwa wazo hilo kwakuwa litasaidia kupata mawazo mazuri ya kuinua uchumi wa taifa huku akimpongeza Rais kwa kuendelea kuongoza nchi kwa amani na usalama.
Vijana 100 waliofanikiwa kuingia katika shindano la Vijana Uchumi Challenge linalofanyika chini ya Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana .Mapana ,amesema kuwa asilimia 70 ya Watanzania ni vijana walio na umri wa chini ya miaka 35 ambapo Serikali iliona ichukue jukumu la kuwainua vijana kupitia shindano hilo muhimu lililoanzishwa chini ya Wizara ya Maendeleo ya Vijana.
Amesema awali wakati wanatembea katika Mikoa mbalimbali kuwasikiliza vijana walibaini kuwepo kwa changamoto kubwa za vijana zilizoonyesha vijana kukosa ajira,kushindwa kufahamu mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Serikali kupitia Halmashauri pamoja na kukosa kufahamu fursa nyingine za kiuchumi.
Amesema,lakini pia walibaini vijana walikuwa wanakosa fursa ya kusikilizwa changamoto zao na kwamba kutokana na sababu hizo Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Vijana iliona ianzishe shindano la Kitaifa la Vijana Uchumi Challenge ambapo kila mmoja ataweza kutoa mawazo yake kwa faida ya taifa.
Vijana waliofanikiwa kuingia katika 100 bora kwenye shindano la Vijana Uchumi Challenge chini Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana.Amesema awali walipotangaza shindano hilo zaidi ya vijana 7,852 walijitokeza kutoa mawazo yao lakini katika mchujo walipatikana vijana 100 ambao wameweka kambi katika chuo cha uongozi cha Mwalimu Nyerere Kibaha kwa ajili ya kuendelea na mchujo mwingine.
Amesema mchujo unaoendelea kufanyika hivi sasa upo chini ya majaji mahiri kutoka vyuo vikuu mbalimbali ambapo baadhi yao ni Profesa Neema Mboja, Profesa Rwekaza Mkandala kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ,Silvia Shayo kutoka Chuo Kikuu cha Tumaini na Profesa Anna Temu kutoka Chuo cha kilimo Sua kilichopo Mkoani Morogoro.
Mapana , ameongeza kuwa mchujo unaofanyika kupitia Majaji hao utafanyika kwa siku nne ikiwa ni kuanzia Juni 23/2026 hadi Juni 26/2026 na kwa awamu ya kwanza utatoa vijana 30 na kisha kuingia awamu ya pili kwa ajili ya kuwasaka vijana 10.
Mapana ameongeza kuwa siku ya Jumamosi shindano hilo litafungwa na Katibu Mkuu,Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana Jenifa Omolo ambaye pia atatoa vyeti kwa vijana wote 100 walioshiriki shindano hilo.
Naibu Katibu Mkuu,Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana Dkt.Kedmon Mapana akiwa katika picha ya pamoja na vijana 100 mara baada ya kuzindua shindano la Vijana Uchumi Challenge uliofanyika katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kibaha Mkoani Pwani.Amesema baada ya kupatikana vijana 10 ndio watakwenda katika killele Julai 06/2026 katika ukumbi wa JKNCC Jijini Dar es Salaam ambapo mgeni rasmi wa kilele hicho atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Amesema ,katika shindano hilo mshindi wa kwanza atazawadiwa fedha kiasi cha Sh . milioni 50,mshindi wa pili Sh .milioni 20 na mshindi wa tatu ataondoka na Sh.milioni 10 huku akisema mawazo ya vijana wengine wote yatachukuliwa na kufanyiwa kazi lakini pia itaanzishwa Kambi maalum ya kuwaendeleza vijana hao.
Amesema Dira ya 2050 ina mambo makubwa mawili ambayo ni masuala ya kukuza uchumi kupitia viwanda pamoja na kukuza kipato cha mtu mmoja mmoja na ili tufike huko lazima vijana wawe katika mstari wa mbele na Serikali ipo pamoja kuhakikisha jambo hilo linafanikiwa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Vijana Uchumi Challenge Josephu Malekela amesema kuwa shindano hilo lilitangazwa Aprili 10,2026 na Waziri wa Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana Joel Nanauka na kamati ilipewa majukumu na kufungua dirisha Aprili 13 /2026.
Naibu Katibu Mkuu ,Ofisi ya Rais , Maendeleo ya Vijana Kedmon Mapana (watatu kutoka kushoto)azinduzi shindano la Kitaifa Vijana Uchumi Challenge uliofanyika Juni 23/2026 katika chuo cha uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kibaha Mkoani Pwani.Malekela,amesema kuwa baada ya kufungua dirisha walipokea mawazo mengi na mazuri yaliyofikia 7,852 kutoka mikoa yote nchini na hatimaye kufanya mchujo na kuwapata vijana 100 ambao ndio kwasasa kazi inaendelea ili kuwapata vijana 10 bora.
Amesema vijana 100 ambapo wameingia katika mchujo huo wametoka katika Mikoa 27 ya Tanzania Bara na Zanzibar huku akibainisha kuwa Mkoa wa Dar es Salaam umetoa vijana 20 na Zanzibar umetoa vijana 18 na wengine wametoka katika Mikoa mbalimbali .
Malekela ,amesema vijana walikuwa na mawazo mazuri lakini wengi wao walijikita katika Kilimo,Tehama,Sera za uchumi na kidigitali ambapo anaimani kupitia majaji waliopo watafanyakazi vizuri na hatimaye kuwapata 10 bora watakaoingia fainali.
Mkurugenzi wa uendelezaji na uwezeshaji vijana Kibiashara kutoka Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana Edward Haule ameishukuru Serikali chini Rais Dkt .Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha jambo hilo muhimu lenye faida kwa Taifa.
Naibu Katibu Mkuu ,Ofisi ya Rais , Maendeleo ya Vijana Kedmon Mapana (watatu kutoka kushoto)azinduzi shindano la Kitaifa Vijana Uchumi Challenge uliofanyika Juni 23/2026 katika chuo cha uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kibaha Mkoani Pwani.Haule,amesema vijana wanatakiwa kuipongeza Serikali kwa kuibeba ajenda hiyo kubwa na kuwafungulia fursa hiyo na kwamba kupitia shindano hilo wengi wa vijana watakuwa wamepata kufahamu wa kutambua fursa mbalimbali za kiuchumi.
Hata hivyo, Adrian Sabudema mmoja wa Vijana aliyeingia katika shindano hilo kutoka Mkoa wa Shinyanga amesema amefurahi kuwepo kwa shindano kwani tangu Uhuru haijawai kutokea shindano kama hilo.
Sabudema,amesema kumekuwa na changamoto nyingi za vijana lakini hapakuwa na pakusemea lakini kitendo cha kuanzisha Wizara ya Vijana imekuwa fursa ya Vijana wa Kitanzania kutoa mawazo yao.
Sabudema, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa kuanzia Wizara ya Vijana sambamba na kukubali kuanzisha shindano la Vijana Uchumi Challenge kwani vijana watakuwa wanatumia kutoa mawazo ambayo yatalisaidia taifa.







Post a Comment