Home
/
KIJIJINI KWETU
/
WANANCHI : MBUNGE JAFARI WEWE HUJUI, HATI IMETUKUTA TUKIISHI KWENYE MAKAZI YETU
WANANCHI : MBUNGE JAFARI WEWE HUJUI, HATI IMETUKUTA TUKIISHI KWENYE MAKAZI YETU
>> Wasema hawajavamia shamba la mifugo na kwamba, kama Kitongoji cha Begi, Kiwandani vipo ndani ya shamba basi ramani ni ya kugushi haikuwa shirikishi.
>>Ushahidi ni shule ya msingi Utegi iliyopo Kitongoji cha Begi iliyojengwa na mkoloni mwaka 1953 baada ya mwananchi kutoa ardhi.
>> Mwaka 1962/1963 Serikali ilianzisha shamba la mkonge, baadae lilibadilishwa matumizi na kuwa shamba la mifugo lililoanzishwa mwaka 1974/1975.
>> Machifu walioongoza katika ardhi ya Vitongoji hivyo ni Chifu Olambo Kateti, Chifu Igogo maarufu Odol Chora na Chifu Yusuf Sarungi.
>> Wasema Serikali wanatumia nguvu ya Kiserikali kutaka kuwanyang'anya ardhi, waitaka ijitafakari.
Na Dinna Maningo, Rorya
WANANCHI wa Kitongoji cha Begi na Kiwandani katika Kijiji cha Majengo, Kata ya Koryo Wilaya ya Rorya mkoani Mara, wamekanusha kauli iliyotolewa na Mbunge wa Jimbo la Rorya Jafari Chege, kwamba wananchi hawatafanyiwa uthamini wa ardhi kwakuwa wanaishi kwenye ardhi yenye hati ya mtu mwingine.
Mbunge Jafari aliyasema hayo wakati akizungumza na Mwandishi wa habari kama ilivyoripotiwa katika chombo hiki cha habari Agasti, 04 ,2023 yenye kichwa cha Habari 'MBUNGE RORYA ASEMA WANANCHI KITONGOJI CHA BEGI, KIWANDANI HAWAWEZI KUPIMIWA ARDHI NI ENEO LENYE HATI'.
Katika habari hivyo mbunge Jafari akasema " Kwenye kikao hatukukubaliana kuwa wananchi watapimiwa ardhi, bali walipwe ardhi kama sehemu ya kifuta jacho, na malipo yawe sawa kwa sababu lile eneo tayari lina Hati.
"Kwa hiyo isingekuwa rahisi lilipwe kwa fidia ya ardhi. Mthamini mkuu alitoa ushauri kwamba eneo lenye Hati ni ngumu kulilipa fidia kwa mtu mwingine unalilipaje? yaani ni sawa eneo lako unalimiliki alafu eti Serikali imlipe mtu mwingine anaitwa Juma na wewe unayemiliki ulipwe unaona tofauti hapo?.
Wananchi wamepinga vikali kauli hiyo na kusema kwamba mbunge Jafari hajui historia ya Vitongoji hivyo kwani uwekezaji shamba la mifugo la Utegi umewakuta wakiwa wanaishi kwenye makazi hayo na kwamba kulikuwa na mpaka wa fensi ya waya uliotenganisha shamba la Utegi na makazi ya wananchi.
Wananchi wa Kitongoji cha Begi na Kiwandani wakionesha mabango wakati wa mkutano wa Mbunge Jafari akizungumza na wananchi hao hivi karibuni.
Wanavitongoji hivyo wanasema iwapo hati inaonesha kuwa walivamia ardhi na wanaishi kwenye ardhi yenye hati ya mtu mwingine ambaye mbunge Jafari hajataja jina la mmiliki wa hati, basi ramani na hati hiyo ni ya kugushi hawakushirikishwa, hivyo ni vyema mbunge awaonyeshe ramani na hati na nani mmiliki ili wajiridhishe.
Imeelezwa kuwa mwaka 1962/1963 Serikali ilianzisha uwekezaji wa kilimo cha mkonge na Kiwanda cha kuchakata nyuzi za katani. Mwaka 1974/1975 ilibadilisha matumizi na kuwa shamba la mifugo na kiwanda cha maziwa, shamba la Na.168.
Serikali ilibinafsisha shamba hilo kwa vijiji 6 ambayo ni Utegi, Mika, Omuga, Nyanduga,Nyasoro na Ingiri vilivyo jirani na shamba la mifugo la Utegi vilivyounda umoja uuitwao UMONI FARMERS DEVELOPMENT ASSOCIATION (UFADA).
Habari zinasema kwamba, baada ya UMONI kubinafsishwa shamba hilo toka Serikalini waliingia makubaliano na mwekezaji Kampuni tanzu ya UDAFCO mwaka 1998 Kampuni iliyopata hati ya umiliki kati ya mwaka 2001-2002 ikiongozwa na aliyekuwa Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Otieno Igogo.
Hata hivyo Serikali ikaeleza kusuasua kwa uwekezaji huo kwa zaidi ya miaka 20 na hivyo chukua hati ya shamba na kiwanda cha maziwa Desemba, 2018 ambapo Otieno Igogo alimkabidhi Hati aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Mara Adam Malima katika ofisi ya mkuu wa mkoa huo.
Aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Mara Adam Malima (wa pili kulima) akipitia nyaraka baada ya kukabidhiwa hati na aliyekuwa Mkurugenzi wa Kampuni ya UDAFCO(aliyesimama) wa tatu kulia ni aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Rorya Simon Chacha na aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Rorya Lameck Airo (wa kwanza kushoto).
Hakimu mstaafu Patrick Ang'ulo mkazi wa Kitongoji cha Begi anasema" Hati imetukuta tukiishi kwenye maeneo hayo, kama wanasema wananchi wanaoishi Kitongoji cha Majengo na Begi ni wavamizi basi upimaji, ramani na hati hiyo hapakuwa na ushirikishwaji, wangetushirikisha tungewaeleza mipaka halisi.
"Serikali inaangalia Hati kwa upande mmoja ,hiyo Hati imetengenezwa wananchi wakiwepo kwenye Vitongoji hivyo"anasema Patrick.
Joseph Mang'ana anasema kuwa kitendo cha wananchi kwenda kulalamika ofisi ya CCM Julai, 27, 2023 kuhusu wathamini wa Serikali kutowafanyia uthamini wa ardhi kwa madai ni wavamizi walifanya makosa.
Wananchi wa Kitongoji cha Begi na Kiwandani wakiwa wameandamana ofisi ya CCM mwishoni mwa mwezi uliopita kama ilivyoripotiwa DIMA Online Julai, 27, na 28, 2023,wakilalamika uthamini kutotendeka kwa haki.
Anasema kwamba, wananchi hawapaswi kuchanganya maswala ya kisheria, kikatiba na kisiasa kwani Chama hakina mamlaka hayo kikatiba.
"Huyo mbunge je ana uhakika? hayo anayoyaeleza? mbunge mbona anakuwa na ndimi mbili? bungeni alieleza nini ukienda ukifuatili bungeni? ina maana aliongea bila kujua aliyoyasema kuhusu Begi?. Bungeni aliongea kuwa hivi Vitongoji viwili Begi na Kiwandani havijawahi kuchukuliwa na Farm.
"Shule ya msingi Utegi imejengwa mwaka 1953 wakati huo ilikuwa inatoa elimu ya kuanzia darasa la 1- 4, Elimu ya zamani hadi hapo elimu ya darasa la 5-7 ilipoanzishwa miaka ya 1970.
"Shamba la mifugo na kiwanda cha maziwa vimekuja mwaka 1974/1975, sasa unasemaje shule hiyo imevamia farm? wanaotuumiza ni viongozi hawa wanasiasa mbunge angefuatilia historia" anasema Joseph.
Joseph anaongeza" Hiyo shule kuna wazee walitoa maeneo yao kwa mkoloni kujenga shule kwa manufaa ya wananchi, wakati huo hatukuwa na Serikali za Vitongoji na Vijiji watu waliongozwa na machifu. Sasa hao wazee wanaambiwa wamevamia Farm!.
" Kama wameamua kuchukua ardhi ya wananchi bure hatushangai, ndio mfumo uliopo lakini hali halisi Kitongoji cha Begi na Kiwandani ni Vitongoji vya asili. Farm ilipokuja iliwekwa mipaka ya kutenganisha eneo la farm.
"Mipaka ilikuwa nje ya Vitongoji na miji inajulikana, wanamaana gani kusema tumevamia farm wakati sisi ndio tumeikaribisha farm imetukuta!"anasema.
Anasema shamba la mkonge na kiwanda cha kuchakata nyuzi za katani kilijengwa mwaka 1962/1963 mara tu baada ya Uhuru, kilichojengwa wakati wa Uongozi wa aliyekuwa Rais wa kwanza Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Joseph ameitaka Serikali hijitafakari " Ardhi kulikojengwa kiwanda wazee haohao wa Begi ndio walitoa ardhi. Serikali hijitafakari suala la Begi wawaulize wazee. Kama wanatathmini kwa kutumia nguvu ya kiserikali sawa lakini ukweli Kitongoji cha Begi kilichozaa Kitongoji cha Kiwandani ni cha asili havijawahi kuvamia farm.
"Farm imewakuta pale imefanya nao kazi na kiwanda kimewakuta wamefanya nao kazi wapo pale pale, farm imefirisika Kitongoji kiko paleple. Ni tamaa tu ya kibiashara ya kunyang'anya wananchi ardhi na imeshazoeleka.
"Migogoro ya ardhi Tanzania imeshakuwa jambo la kawaida hatushangai kwa kauli za hivyo, kumekuwa na visingizio kuwa watu wamevamia ardhi , wamevamia mbuga, ndiyo lugha ambayo wamekuwa wakiitumia kunyang'anya ardhi wananchi" anasema Joseph.
Anasema wakazi wa Begi ni wakazi wa asili kabla ya shamba la mifugo" Haya ya uvamizi yamekuja leo, mbunge hajui kuhusu Begi yeye siyo mzaliwa wa Utegi, awaulize wananchi wa utegi wamweleze asikurupuke na kusema wananchi wamevamia ardhi kama hawataki kulipa ardhi ni kwamba wamewanyang'anya wananchi ardhi kwa nguvu ya kiserikali.
"Serikali hii hii ilichukua ardhi kutoka Vijiji sita baadae ikawarudishia wananchi ardhi, hiyo Hati ya Farm ilisharudishwa mara mbili Serikalini ,awali ilirejeshwa kwa Tume ya Rais ya kurekebisha mashirika ya umma (PSRC) shirika lililokuwa linataifisha mashirika yaliyofirisika baada ya kiwanda kufirisika na Farm kufirisika.
"Serikali ya wakati huo iliyoongozwa na Rais Hayati Benjamin Mkapa na Waziri Mkuu Frederick Sumaye iliamuru wananchi wa Vijiji sita waunde ushirika ili waweze kukabidhiwa shamba na kiwanda, wananchi wakaunda umoja maarufu UMON, lakini wakapewa sharti la kulipa asilimia 10 ya thamani ya mali iliyokuwepo ya farm na kiwanda kama Milioni 95 wakalipa pesa wakamiliki shamba" anasema Joseph.
Anaongeza " Ninayeongea na wewe nimezaliwa hapo hapo Begi mwaka 1954, baba yangu mzee Agastin Owenga Mang'ana alizaliwa 1912, alifariki mwaka 2006 na kuzikwa katika boma lake la asili kitongoji cha Begi alifia kwenye eneo lake ambalo leo tunaitwa sisi ni wavamizi.
"Wakati baba anaota eneo la shamba mimi nilikuwepo wakati huo nilikuwa nachunga mbuzi, alafu leo ardhi ya mzee ichukuliwe bure bila kulipwa. Eneo hili la Begi ndicho Kitongoji kilichopokea watu waliohamishwa toka mlima Koryo" anasema mwananchi huyo.
Anasema mlima Koryo ulikuwa na makazi ya watu walipohamishwa hawakulipwa fidia, na kwamba wanakitongoji cha Begi waliwakaribisha na kuwapa ardhi wakajenga Nyumba na kuishi.
"Miji iliyokuwepo kabla ya Farm haizidi miji kumi, wazee hao ndiyo walikuwa na maeneo yao. Wananchi walioondolewa mlima Koryo walipokelewa na kuishi na wameishi Begi karibu miaka 50 tangu 1974/1975 lilipoanzishwa shamba la mifugo.
"Kama kuna ramani ya Farm ni ramani iliyoghushiwa juzijuzi ya kutuingiza ndani ya Farm, ramani ya kwanza ilikuwa nje kabisa na Farm na waliweka fensi, kama kuna ramani mpya basi kuna ujanja tu wa watu, tamaa za watu wanataka kuchukua ardhi hiyo yote kwakutumia kauli ya uvamizi.
"Waulize historia, ni jambo linaloumiza kwakweli kuambiwa eti umevamia farm wakati umezaliwa hapohapo na Farm iliwakuta " anasema Joseph .
Wazee walioishi Begi tangu miaka ya 1900
Imebainika kuwa wazee wenye asili ya Vitongoji vya Begi na Kiwandani ambao wameishi hapo tangu miaka ya 1900 ambao baadhi yao walishafariki na wengine bado wapo wakiishi ni pamoja na Augustine Owenga Mang'ana, na wanaye, Otieno Waryato na wanaye
Olengo Waryato na wanaye, Obade Akoto na wanaye, Sime Koyi na wanaye.
Wengine ni Osodo Ang'ulo na wanaye
Randiala Ang'ulo na wanaye, Patrick Okaka Atiyo na wanaye na Mwl. Alphaxad Nyakeke ambapo kaya zingine zinazoishi Kwenye vitongoji hivyo walihamia mwaka 1974/1975.
Machifu walioishi Kitongoji cha Begi
Machifu walioishi Kitongoji cha Begi na Kiwandani wa kwanza alikuwa ni Olambo Kateti akafuatia Chifu Igogo aka Odol Chora pamoja na Chief Yusuf Sarungi baba yake Prof. Sarungi.
Inaelezwa kuwa Chief Sarungi alikuwa akifanya vikao vya Baraza eneo la Begi kulikokuwa na mti mkubwa katika shule ya msingi Utegi hivyo wananchi wa vitongoji hivyo wanastahili fidia ya ardhi na Maendelezo ya vitu juu ya ardhi.
Na ikumbukwe kuwa mwaka 1974 Serikali ilipotwaa Ardhi ya vijiji sita vya Utegi, Mika, Omuga Nyasoro, Nyanduga na Ingri kwa ajili ya uwekezaji shamba la Utegi hawakulipwa fidia.
Arina Sewe anasema kama Vitongoji hivyo vipo ndani ya Hati ya shamba la mifugo kwanini serikali imebandika namba za makazi kwenye nyumba zao ikijua wananchi wanaishi eneo lenye hati ya mtu mwingine?
George Albetus Otieno anasema " Wathamini wamekuja kwangu sikuwepo wakafanya tathimini na kuchora maandishi kwenye nyumba mbili wakaacha kuhesabu ya mke mdogo na jiko, shamba la miwa na migomba hawajajesabu, na hatukuwepo hatujui wameorodhesha nini .
Anaongeza " Wazazi waliopisha kiwanda cha mkongwe walihamishwa hawakulipwa wakakubali kutoa eneo kwa ajili ya mradi wa mkonge mwaka 1963 tukapisha.
"Waliopisha ni mzee akoto Matara na ndugu yake Obade Matara na shule ya msingi utegi mzee Agustino Mang'ana alitoa eneo kupisha ujenzi wa shule iliyojengwa mwaka 1953 na hakulipwa kitu.
Anaiomba serikali uthamini uwe wa wazi na haki kwani ardhi aliyonayo alilithishwa na baba wamezaliwa Tisa waliohai ni Saba na yeye ndio msimamizi wa familia.
Rejea
>>> Desemba, 2018 Serikali ya awamu ya tano iliyoongozwa na Rais Hayati John Pombe Magufuli kupitia aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Mara, Adam Malima ilikabidhiwa Hati za shamba la mifugo na kiwanda cha maziwa kutoka kwa Otieno Igogo aliyekuwa Mkurugenzi wa Kampuni hiyo baada ya kushindwa kuendeleza huku Mifugo na mali zingine kutojulikana ziliko.
Serikali ya mkoa wa Mara kupitia aliyekuwa mkuu wa mkoa huo, Adam Malima ilitoa ombi kwa Rais Hayati John Pombe Magufuli, kuwa shamba hilo wapewe vijiji sita vilivyounda Chama cha UMONI FARMERS DEVELOPMENT ASSOCIATION (UFADA), kisha kupitia Wizara ya Uwekezaji, Viwanda, na Biashara, Wizara ya mifugo, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) wapate mwekezaji.
Hadi sasa UMONI haijarejeshewa Hati ya shamba na kiwanda cha maziwa na haijabainika wazi nani mmiliki wa shamba hilo, nani Mwenye Hati ya shamba wala nani anayetaka kuwekeza katika shamba hilo kutokana na Serikali kutobainisha wazi uhalali wa shamba hilo.
Shamba la mifugo linaendelea kulindwa na askari wanaodaiwa ni wanajeshi wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT). Kwa sasa vitongoji kadhaa Kata ya Koryo na Bukwe vimefanyiwa tathmini ya maendeleo juu ya ardhi kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kutaka kufidiwa wapishe Makazi hayo ili Serikali iendeleze shughuli za uwekezaji.
Mwaka 1997 aliyewahi kuwa Waziri wa Kilimo na Ushirika, Paul Kimiti wakati akiwasilisha Bungeni hotuba ya wizara hiyo ya makadilio na matumizi ya fedha kwa mwaka 1997/1998,wakati huo Waziri mkuu akiwa ni Frederick T. Sumaye, Waziri huyo alisema Wizara ilikubaliana na Tume ya Rais ya kurekebisha mashirika ya umma (PSRC) kupendekezwa utaratibu wa kununua hisa katika shamba la mifugo la Utegi.
Hisa hizo ni kwa wananchi ambao maskani yao yapo karibu na shamba hilo
katika kufanikisha urekebishaji na ubinafsishaji wa mashirika yaliyo chini ya Wizara hiyo ambapo wananchi wa Vijiji 6 waliunda Chama cha UMONI UMON FARMERS DEVELOPMENT ASSOCIATION (UFADA) kilichofanikiwa kununua shamba hilo na kupata mwekezaji Kampuni ya UDAFCO.
Hata hivyo Kampuni hiyo UDAFCO iliingia mgogoro na UMONI baada ya kukiuka makubaliano zikiwemo hisa jambo lililopelekea Serikali kuchukua hati ya umiliki kutoka kwa Mkurugenzi wa UDAFCO.
Awali akizungumza na Mwandishi wa DIMA ONLINE kama ilivyoripotiwa katika Chombo hiki cha habari, Mkuu wa wilaya ya Rorya Juma Chikoka alisema kuwa uthamini uliofanyika katika baadhi ya Vitongoji Kata ya Bukwe na Koryo kikiwemo Kitongoji cha Begi na Kiwandani hauhusiani na Serikali ya Wilaya hiyo.
" Sisi kama Serikali jukumu letu ni kusimamia usalama na amani, lile eneo linamilikiwa na watu wengine, kwahiyo nilichotaka nikwambie hilo jambo la uthamini halina uhusiano wowote na Serikali ya Wilaya" DC Chikoka.
Wananchi wanaiomba Serikali kuzingatia Sheria za nchi na Katiba na iwatendee haki katika zoezi la uthamini lililofanyika badala ya kutumia nguvu ya kiserikali kufanya uthamini usio wa haki.
Isemavyo Katiba
>>>Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 16 .-(1) inasema kila mtu anastahili kiheshimiwa na kupata hifadhi kwa nafasi yake, maisha yake binafsi na familia yake na unyumba wake, na pia heshima na hifadhi ya maskani yake na mawasiliano yake ya binafsi.
Ibara ya 24.-(1) inasema, kila mtu anayo haki ya kumiliki Mali, na haki ya hifadhi ya Mali yake aliyonayo kwa mujibu wa sheria.
................ Itaendelea
Post a Comment