HEADER AD

HEADER AD

ASKARI CHALINZE WATAKIWA KUTOKUWA NA HURUMA NA MADEREVA WANAOKIUKA SHERIA ZA BARABARANI



Na Gustafu Haule, Pwani

KAMANDA wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani Pius Lutumo, amewaaagiza askari waliopo katika kituo cha Polisi cha Chalinze kutokuwa na huruma kwa madereva wanaokiuka Sheria za usalama barabarani na kutaka anayekiuka Sheria hizo ahadhibiwe vikali.

Lutumo, ametoa kauli hiyo Agosti 16 mwaka huu wakati akizungumza na maafisa wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali ikiwa ni sehemu ya muendelezo wa ziara yake katika Wilaya mbalimbali za Kipolisi zilizopo Mkoani Pwani.

  Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani ACP Pius Lutumo

Akiwa katika mkutano wa pamoja na askari hao Kamanda Lutumo amewataka kuendelea na jukumu la ukamataji wa madereva wanaovunja Sheria huku akisema kazi hiyo inapaswa kufanywa na askari wote na sio kuwaachia askari wa usalama  barabarani pekee.

"Tusiwaachie askari wa kikosi cha usalama barabarani pekee, badala yake tushirikiane kwa pamoja kuchukua hatua ili kuweza kutokomeza ajali za mara kwa mara zinazotokana na makosa ya kibinadamu kama vile kuyapita magari mengine bila tahadhari, mwendokasi, matumizi ya vileo na kutokuheshimu vivuko vya watembea kwa miguu,"amesema Lutumo

Lutumo ameongeza kuwa,hivi karibuni watu wa nne wa familia moja walipoteza maisha katika ajali ya barabarani eneo la Mapatano, Kata ya Mbwewe tukio ambalo lilivuta hisia kwa watu wengi kutokana na ajali hiyo ya barabarani hivyo wanapaswa kuweka mikakati ambayo haitaruhusu ajali kama hizo.




 " Askari wote wana jukumu la kutoa taarifa kwa wenzao waliopo barabarani pindi wanapoona dereva anaendesha gari kwa kuvunja Sheria za usalama barabarani ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa", amesema Lutumo.

Hatahivyo, Lutumo amewakumbusha umuhimu wa utoaji huduma bora pindi wanapowakamata madereva wanaovunja sheria kwa kuwaeleza makosa yao kabla ya kutoa adhabu ili wajue makosa yaliyopelekea kupewa adhabu husika.



No comments