HEADER AD

HEADER AD

RPC PWANI AWATAKA POLISI BAGAMOYO KUACHA KUFANYA KAZI KWA MAZOEA

Na Gustafu Haule, Pwani

ASKARI wa Jeshi la Polisi waliopo Wilayani Bagamoyo, katika mkoa wa Pwani wameonywa kuacha tabia ya kufanyakazi kwa mazoea na badala yake waanze kubadilika kifikra na kufanyakazi kwa weledi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishina Msaidizi wa Polisi, Pius Lutumo ,ametoa kauli hiyo Agosti 15 mwaka huu wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa kuangalia utendaji kazi Wilayani hapo .
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani Pius Lutumo akizungumza na askari wa Jeshi hilo waliopo Wilayani Bagamoyo katika ziara yake aliyoifanya Agosti 15 mwaka huu.

Katika ziara hiyo Lutumo amezungumza  na maafisa, wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali ambapo amewataka kuzingatia ufanyaji kazi kwa mujibu wa Sheria za nchi na kuacha kufanya kazi kwa mazoea hali inayopelekea utendaji usioridhisha.

Pia, Kamanda Lutumo amesisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa nidhamu na kuzingatia maadili ya Jeshi la Polisi kwa kujiepusha na vitendo vya mmomonyoko wa maadili ikiwemo vitendo vya rushwa vitakavyolichafua Jeshi ambavyo huweza kusababisha kufukuzwa kazi.

Kadhalika, amewataka askari kufanya kazi kwa kusimamia misingi ya utendaji bora kwa kutenda haki kwa tunao wahudumia vituoni kwakuwa kazi ya Polisi ni kutenda haki pasipo dhuruma.


 " Wananchi hawapendi kuja kwenye vituo vyetu ila wanafika kwa kuwa wanashida zinazohitaji kusaidiwa nasi,hivyo ni jukumu letu kuwapa huduma bora wanapofika kwenye vituo vyetu vya Polisi”,amesema Lutumo

Aidha, amewakumbusha askari umuhimu wa kutunza vizuri vielelezo na kutokuwa na tamaa au kushawishika katika kuiba vielelezo hivyo viwapo kituoni.

 Hatahivyo, Lutumo amesema kuwa  jukumu la Jeshi la Polisi ni kulinda vielelezo vilivyopo kituoni na kuhakikisha vinatunzwa vizuri na siyo kuwa sehemu ya upotevu wa vielelezo hivyo ambavyo vitatumika kama ushahidi Mahakamani.


No comments