LAKAIRO, SANGO WATOA MSAADA WA KITANDA, GODORO, SHUKA, KWA CHARLES OWINO MWENYE ULEMAVU
Na Dinna Maningo, Rorya
HATIMAYE Charles Owino Ogada mwenye ulemavu wa viungo mkazi wa Kitongoji cha Begi, Kijiji cha Majengo Kata ya Koryo wilaya ya Rorya mkoani Mara, amepata msaada wa kitanda, godoro, shuka nne na fedha Tsh. 100,000 kutoka kwa wasamalia wema.
Msaada huo wenye jumla ya Tsh.500,000 umetolewa na Mbunge Mstaafu Jimbo la Rorya Lameck Airo kwa jina maarufu Lakairo pamoja na mjumbe wa mkutano mkuu Taifa Chama cha Mapinduzi (CCM) Sango Kasera Gungu.
Akikabindi msaada huo kwa niaba ya wasamalia hao, Diwani wa Kata ya Koryo Nelson Simba Ores akiwa ameongozana na viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Koryo na Tawi la Majengo na kufika Kitongoji cha Begi amemkabidhi Jenifer Mussa shemeji wa Charles Owino mahitaji hayo.
Diwani wa Kata ya Koryo Nelson Simba Ores akimkabidhi fedha Jenifer Mussa mke wa kaka yake Charles Owino
"Nimefika hapa kwa kazi ya kumkabidhi Charles vifaa ambavyo ni kitanda kimoja, godoro moja, shuka nne na pesa Tsh. 100,000 lakini hatujamkuta yupo Mwanza kwa ajili ya matibabu.
"Vifaa hivi tunamkabidhi shemeji yake anayeishi nae hapa Begi. Msaada umetolewa na walezi wetu wa CCM Kata ya Koryo Mbunge mstaafu Lameck Airo na mjumbe wa mkutano mkuu taifa CCM Sango Kasera. Tunaomba hii laki moja imsaidie katika matibabu na tunaamani vitu hivyo vitamsaidia.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Kata ya Koryo Jacob Obade Matara, amesema amefurahi kwa msaada huo wa vifaa kwa ajili ya kumshika mkono Charles huku akizidi kuwaombea kwa mwenyezi Mungu waliotoa msaada huo kuendelea kuwasaidia watanzania wengine wenye hali kama ya mlemavu Charles.
"Tunamshukuru Lakairo na Sango kwa msaada huo kwani wametimiza pia Ilani ya CCM inayohimiza kuwasaidia wahitaji wasiojiweza wakiwemo walemavu. Tunaomba na wengine wamsaidie kwa hali yake bado anahitaji kupata msaada wa kifedha ili kumudu maisha yake.
"Kitanda ni cha futi nne kwa sita Tsh. 220,000, Godoro 140,000, shuka nne Tsh. 40,000 vimenunuliwa Utegi, anakabidhiwa na fedha taslimu Tsh. 100,000.
" Hakika vifaa hivi vitamsaidia sana Charles sasa hatopata maumivu kama alivyokuwa akiteseka kulala kwenye kipande cha godoro lililozeeka" amesema Jacob.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kiwandani Onunda Agingo Kimweli ambaye ni ndugu wa Charles, akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kitongoji cha Begi Christian Odundo Othiong'o, amewashukuru viongozi wa CCM Tawi, Kata, mabalozi kufika nyumbani kwa Charles kushuhudia tukio hilo ambapo amemshukuru Lakairo na Sango kwa tendo jema.
"Charles kila siku alikuwa akiongea lazima atasema anatamani kupata kitanda kizuri, godoro zuri na pesa za kujikimu, sasa amepata matamanio yake ya kulala pazuri yametimia, Mungu azidi kuwabariki na awaongezee walipotoa "amesema Onunda.
Amewaomba wasamalia hao kuendelea kuwa na moyo huo wa kusaidia watu wenye huitaji kama Charles mwenye ulemavu wa viungo.
Jenifer shemeji wa Charles ambaye ni mke wa kaka yake Mussa ameshukuru kwa msaada huo huku akiwaomba waliotoa msaada huo pamoja na watu wengine waendelee kusaidia wahitaji.
" Charles ni shemeji yangu tuna ishi nae mimi na mme wangu, tangu alipofiwa na wazazi wake 2002, namchukulia kama mwanangu. Kwa sasa hayupo mme wangu alienda nae Mwanza kwa ajili ya matibabu kisha atarudi kijijini.
" Nashukuru kwa niaba yake, msaada huu utamsaidia sana na atafurahi sana kwakuwa matamanio yake yalikuwa kulala katika kitanda kizuri na godoro. Uwezo wetu ni mdogo hatukuweza kumudu matamanio yake yote " amesema Jenifer.
Febuari, 21, 2024 DIMA Online iliripoti makala simulizi iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho 'UGUMU WA MAISHA UNAVYOMTESA CHARLES OWINO OGADA'
Charles Owino Ogada
Pia ilielezwa ndani ya nyumba yake yenye chumba kimoja kuna kipande kidogo cha godoro kilichozeeka kilichowekwa juu ya jamvi anachokitumia kulala.
Katika makala hiyo Charles Owino aliyezaliwa mwaka 1964, anayeishi na kutunzwa na kaka yake Mussa Daniel Ogada alieleza matamanio yake ya kuwa na ndoa, malazi mazuri na mlo kamili.
Pia ilielezwa ndani ya nyumba yake yenye chumba kimoja kuna kipande kidogo cha godoro kilichozeeka kilichowekwa juu ya jamvi anachokitumia kulala.
Kipande cha godoro anacholalia kinampa maumivu katika mwili wake na kumnyima usingizi kwakuwa hana uwezo wa kununua kitanda na godoro la kisasa huku akilala kwenye godoro lisilotandikwa shuka.
Rejea Nukuu za Charles Owino
" Natamani kuwa na mke, natamani kuwa na watoto, natamani tendo la ndoa, natamani kulala kwenye kitanda kizuri, natamani kula nyama ya kuku, natamani kula samaki, natamani kunywa soda.
" Nalala chini kwenye kipande hiki cha godoro kama unavyokiona, huwa naumia viungo vya mwili. Natamani na mimi nilale kwenye kitanda kizuri chenye godoro zuri.
"Mwambie Rais Samia anisaidie na mimi nipate maisha mazuri kama walemavu wengine, aninunulie hata Kiti mwendo nateseka na ugumu wa maisha " anasema Charles.
"Mwambie Rais Samia anisaidie na mimi nipate maisha mazuri kama walemavu wengine, aninunulie hata Kiti mwendo nateseka na ugumu wa maisha " anasema Charles.
Charles Owino anahitaji msaada wa matunzo na matibabu bora. Anayewiwa kumsaidia awasiliane na kaka yake Mussa Daniel anayeishi na kumuhudumia kwa kumpigia simu kwa namba +255767987809 au +255782948660.
Post a Comment