MJUMBE KAMATI YA UCHUMI JUMUIYA YA WAZAZI ATOA SIMU JANJA 26
Na Gustafu Haule, Pwani
MJUMBE wa Kamati ya Uchumi ya Jumuiya ya Wazazi Taifa Dk.Chakou Tindwa ameendelea na jitihada za kukiimarisha Chama cha Mapinduzi (CCM) ambapo kwasasa amekipiga tafu chama chake kwa kutoa simu janja 26 zenye thamani ya Tsh.Milioni 6.5 zitakazotumika kusajili wanachama waliopo Wilayani Mkuranga.
Dkt.Chakou ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Siasa ya mkoa wa Pwani mbali na kusaidia simu hizo lakini pia amekabidhi kadi za CCM 12,500 kwa ajili ya kuwagawia wanachama waliopo Wilayani humo.
Mjumbe wa kamati ya uchumi ya Jumuiya ya Wazazi Taifa na mjumbe wa kamati ya Siasa ya Mkoa wa Pwani Dr .Chakou Tindwa (Kushoto) akimkabidhi mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani Mwinshehe Mlao Kadi 12,500 Kwa ajili ya kuwagawia wanachama wa CCM Wilayani Mkuranga.
Hatua ya Dkt. Chakou kutoa simu na kadi hizo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi zake alizozitoa kwa kamati ya Siasa ya Wilayani Mkuranga siku chache zilizopita.
Akikabidhi simu na kadi hizo kwa Nwenyekiti wa CCM mkoa wa Pwani Mwinshehe Mlao katika kikao cha kamati ya Siasa Wilayani Mkuranga kilichofanyika Februari 22 mwaka huu Tindwa amesema kazi ya kujenga chama ni jukumu la kila wanachama.
Mjumbe wa kamati ya uchumi ya Jumuiya ya Wazazi Taifa na mjumbe wa kamati ya Siasa Mkoa wa Pwani Dkt Chakou Tindwa (Kushoto) akimkabidhi mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani Mwinshehe Mlao ( Kulia) simu janja 26 zenye thamani ya Sh.milioni 6.5 Kwa ajili ya kusajilia wanachama kwa njia ya kieletroniki.
Dkt .Tindwa amesema simu hizo zitagawanywa katika kila Kata zilizopo Wilayani humo na kwamba dhamira yake ni kuona kila mwanachama anasajiliwa na kupata kadi ya kieletroniki kama ambavyo CCM Taifa ilivyoelekeza.
"Niliahidi kununua simu za kusajilia wanachama kwa njia ya kieletroniki hapa Wilayani kwetu Mkuranga na leo natimiza ahadi yangu kwa kukabidhi simu hizi 26 zenye thamani ya Tsh. Milioni 6.5 naomba mwenyekiti uzipokee,"amesema Tindwa.
Aidha, Dkt.Tindwa ameiambia kamati ya Siasa Wilayani Mkuranga kuwa yeye ana mapenzi ya dhati na chama chake hivyo yupo tayari kuendelea kusaidiana na wanachama wenzake pamoja na wadau mbalimbali kuhakikisha wanakiimarisha chama kwa kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi ( CCM) Mkoa wa Pwani Mwinshehe Mlao, akizungumza baada ya kupokea simu na kadi hizo amemshukuru Dkt .Tindwa kwa namna anavyojitoa katika kuisaidia chama .
Mlao amesema kuwa CCM haiwezi kujengwa na mtu mmoja bali itajengwa kwa ushirikiano wa wanachama, viongozi na wadau mbalimbali na kwamba kama kuna mtu anataka kuchangia chama ni vyema akajitokeza.
"Naomba nitumie fursa hii kumshukuru ndugu yetu Dkt .Tindwa kwa msaada huu mkubwa kwani naamini kupitia simu hizi changamoto ya usajili kwa wanachama inakwenda kuisha,"amesema Mlao.
Hata hivyo Mlao amewaomba viongozi na wanachama ambao watakabidhiwa simu hizo kwenda kuzitumia kikamilifu kwa shughuli zilizokusudiwa ili kuweza kufikia malengo yaliyowekwa na chama.
Post a Comment