HONGERA TMDA, WABUNGE WAMEPATA JAMBO LA KUSEMEA KUNUSURU VIWANDA
NA ANDREW CHALE, KIBAHA
MSEMA LEO natoa kongole kwa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba nchini (TMDA) kwa hatua sahihi na muhimu ya kuratibu ziara ya Kamati ya kudumu ya Bunge ya Afya na masuala ya Ukimwi ambao ni watunga sheria katika viwanda vya uzalishaji dawa hapa nchini hususan vya Wazawa
Ziara hiyo maalum iliyofanyik tarehe 19-20 Februari, 2024 mkoani Pwani na Dar es Salaam,
Msema Leo, jambo hili nimeliona ni kubwa na nyeti sana hivyo taasisi nyingine za udhibiti zinapaswa kuiga mfano huu wa TMDA ambao kwa kiasi kikubwa unaongeza uwajibikaji na kubaini changamoto zinazowakabiri wadau katika sehemu husika.
TMDA ambao ni wasimamizi wa masuala ya ubora,usalama na ufanisi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi ambazo ni bidhaa muhimu katika kulinda uzima wa binadamu, imeleta faraja kwa wamiliki wa viwanda vya ndani kwani wamekuwa wazi na kufunguka juu ya kero zao na kutoa ya moyoni, ambayo Msema Leo pia ameyasikia na baadhi nayaleta kwenu.
Katika ziara hiyo, TMDA wameweza kuratibu kamati hiyo ya kudumu ya Bunge kwa kutembelea viwanda vitatu vya uzalishaji wa dawa za binadamu hapa nchini ambavyo ni kiwanda cha Kairuki na kiwanda cha Katwaza vyote vya Kibaha, Mkoani Pwani huku Dar es Salaam.
Walitembelea kiwanda cha maji tiba cha Alfa hata hivyo, kote huko Kamati imepokea kero na chagamoto lukuki ambazo zinatishia viwanda hivyo kufungwa hivyo Serikali na Bunge wanapaswa kuzifanyia kazi kwa haraka.
Miongoni mwa kero hizo ni iwepo wa utitiri wa kodi kutoka kwa mamlaka za udhibiti kama TRA, TBS, GCLA, TMDA, TAEC huku pia wakieleza namna uhaba wa fedha za Kigeni hususani dola inavyowakwamisha katika ununuzi wa malighafi nje ya nchi.
Ellen Magita ni Meneja wa Kiwanda cha kuzalisha dawa cha Kairuki ameeleza kuwa, miongoni mwa changamoto yao kubwa ni ucheleweshwaji wa malipo kutoka Bohari ya Dawa nchini (MSD) hali inayowapa ugumu wa uendeshaji pamoja na kununua malighafi kwa ajili ya uzalishaji dawa.
Amesema kuwa mwaka 2018 wametumia Tsh. takriban Bilioni 60 katika kuanzisha kiwanda hicho, fedha ambazo ni mikopo ya benki za ndani na nje kama mdhamini huku wakihitajika kulipa Sh 500 bilioni na endapo watachelewesha wanatakiwa kulipa faini.
"Sheria iliyopo inayotumika na MSD inamtaka mzabuni wa ndani kutoa kwanza bidhaa na malipo yake yanakuja baada kusambazwa kwa dawa lakini yule wa nje analipwa asilimia 80 ndipo analeta mzigo,"amesema Magita.Kutokana na utaratibu huo wamejikuta wanazalisha bidhaa na kujilimbikizia madeni na hivyo wanashindwa kuagiza malighafi kwa kukosa fedha.
Changamoto zingine ni pamoja na mkanganyiko wa taasisi za Serikali katika ukaguzi na utoaji vibali, tozo za kuingiza malighafi, uhaba wa mahali pa uhifadhi wa bidhaa kwa kuwa kuna mlundikano wa bidhaa kwa kukosa soko la uhakika, mazingira suni ya uhifadhi malighafi bandarini na uhaba wa dola.
Pia ameongeza kuwa, kumekuwa na kero ya tatizo kubwa la umeme na maji ya kisima walichochimba kutozwa sh 1 kwa kila lita moja kiasi kwamba kwa siku wanatozwa na WAMI/RUVU sh. laki 3 kwa lita hali ambayo ni kikwazo kikubwa katika uzalishaji wa dawa kwani wamekuwa wakitumia fedha nyingi katika uzalishaji.
"Tunanunua maji lita moja 1, kutoka Wami Ruvu kwa Sh 1 ambapo kisima ni chetu,umeme ni wetu lakini tunatakiwa kutoa kiasi hicho kwa tanki la lita milioni moja ambalo linatumika kwa siku tatu,"amesema.
David Lutabana ni Meneja wa Ubora Kiwanda cha dawa cha Katwaza, amesema umeme umekuwa ni tatizo kwenye uendeshaji wa viwanda kwani hautabiriki na kusababisha hasara wakati wa utengenezaji wa dawa.
"Baada ya kufuatilia kwa muda tumegundua tunakatiwa umeme pasipokuwa na ratiba walianza kila jumatano mwisho wa siku unakatwa mara mbili au tatu kwa wiki hivyo inatubidi kusimamisha uzalishaji,"amesema Lutabana.
Amesema kama itawezekana wawekewe laini maalum ambayo viwanda vitajitegemea wakati mchakato wa gesi asilia ukiwa unaendelea ambapo wataunganisha ili kuepukana na gharama kubwa za mafuta kwenye utumiaji wa jenereta.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Bunge, Stanslaus Nyongo wakati wa majumuisho amesema kuwa, watakaa kikao na chama cha wazalishaji dawa nchini (TPMA), Wizara ya fedha, Wizara ya Viwanda na Wizara ya Afya ili kujadili changamoto zilizotolewa.
"Tulishatoa ushauri kwa Serikali lakini leo tumekuja kutembelea viwanda tumekuta changamoto ambazo zimetupa hisia kubwa hususani ucheleweshaji malipo ya wazabuni kutoka MSD na uhaba wa dola," amesema Nyongo.Hata hivyo Nyongo amesema Serikali inatakiwa kuangalia kwa namna ya kipekee suala la ukosefu wa dola kwani litaweza sababisha upungufu wa dawa nchini.
Mjumbe wa Kamati hiyo ya Bunge, Khamis Kigwangalla ambaye ni Mbunge wa Nzega Vijijini aliomba kufahamishwa kama kuna sheria ambayo iliwekwa na Serikali kupewa bidhaa za ndani kwa mkopo huku za nje wakilipa asilimia 80.
Akijibu hoja hiyo ya Kigwangalla, Kwa niaba ya Mfamasia Mkuu wa Serikali Bi. Suma Jairo amekiri uwepo wa sheria ya manunuzi ambayo kwa sasa imefanyiwa marekebisho.
"Sheria iliyopo nje ya nchi zinatutaka kulipa kwanza kwa sababu haiendi kwa mwenye kiwanda moja kwa moja bali inamfikia mtu wa kati ambaye ni benki halafu yeye ndiye atakaye husika na malipo kwa wenye viwanda,"amesema Suma.
Msema leo nasema kwamba kilio cha wenye viwanda vya dawa nchini kisipofanyiwa kazi kwa haraka na Serikali na Bunge katika kupata ufumbuzi viwanda hivi vitafungwa
Vitakapofungwa italeta changamoto ya upatikanaji wa dawa nchini ikizingatiwa kuwa viwanda hivi vimepunguza wafanyakazi na kufunga baadhi ya njia za uzalishaji kwa gharama za uendeshaji kuwa kubwa na ukosefu wa soko.
Post a Comment