UGONJWA WA BUNGUA MWEUSI WASHAMBULIA KAHAWA BUKOBA
>>DC BUKOBA asema wataalam wa kilimo wanaendelea kuudhibiti
Na Alodia Dominick, Bukoba
MKUU wa wilaya ya Bukoba , Erasto Sima amesema wataalamu wa kilimo katika wilaya hiyo wanaendelea na jitihada za kudhibiti ugonjwa wa bungua mweusi wa Kahawa kwani kuendelea kusambaa kwa ugonjwa huo kutashusha uchumi wa mkoa hasa Wilaya ya Bukoba.
Mkuu huyo wa wilaya ya Bukoba Siima ameyasema hayo wakati akizungumza na vyombo mbalimbali vya habari wilayani humo.
Siima amesema Tegemeo kubwa la mkoa na Wilaya ya Bukoba katika kukuza uchumi ni zao la kahawa ambalo sasa umeibuka ugonjwa unaoshambulia mmea huo.
" Hili jambo likiendelea litashusha uchumi wetu, wataalam wa kilimo wameshasambaa maeneo yenye mashamba ya kahawa kuangalia namna ya kufanya utatuzi, nimeagiza wataalam wa kilimo kuangalia hasa maeneo yaliyo na uhalibifu ili kuweza kushughulikia haraka "amesema Sima
Afisa kilimo halmashauri ya Bukoba Babylus Mashauri akiongea katika kikao cha baraza la madiwani amesema halmashauri hiyo imepata changamoto ya kisumbufu kinachoshambulia zao la kahawa kinaitwa bungua mweusi wa Kahawa.
Mashauri amesema madhara yake ni kwenye matawi ya Kahawa anatoboa matundu madogo na kuingia ndani anataga mayai kwa ajili ya kuzaa.
Anasema Bungua wa kiume anaweza kuishi siku 6 na Bungua wa kike anaishi siku 58 na ana uwezo wa kutaga mayai kati ya ( 20- 50 ) kwa uzao mmoja lakini baada ya kuanguliwa hao wadudu bungua wa kike anakaa siku ( 19 ) kisha anaondoka kwenda kutafuta makazi mengine.
Anasema Athari za Bungua huyu ni kukauka kwa matawi yaliyoshambuliwa na kadiri anavyoendelea kushambulia athari inaweza kuwa kubwa kupelekea kupoteza uzalishaji kwa kiwango kinachoanzia asilimia ( 20- 50 ) ya uzalishaji wa zao la kahawa.
Amesema mikakati ya kukabiliana na ugonjwa huo ni pamoja na kuwajengea uwezo wa taalamu wa kilimo kwa maana ya kuwatambua wadudu pamoja na madhara yake.
Ametaja hatua ya pili ni kampeni kwa ajili ya kumtokomeza mdudu huyo mwenye madhara makubwa kwa jamii inayojishughulisha na zao hilo kujiongezea kipato.
Aidha amesema zao la kahawa ndiyo kipaumbele kwa mkoa wa Kagera na ni zao la kiuchumi na kudai kuwa wapo kwenye mapambano ambayo kimsingi ni ya kiuchumi kwa sababu kahawa ndiyo uchumi wao.
Naye mwenyekiti wa Halmashauri ya Bukoba Murshid Ngeze ,amemuomba mkuu wa Wilaya kuwasaidia katika kukabiliana na tatizo la ugonjwa huo unaotishia maisha ya wakulima wa Kahawa.
Ngeze amewataka wataalam wa kilimo kutafuta suluhisho la haraka ili kudhibiti kabla ya tatizo kuwa kubwa kwenye jamii.
Post a Comment