HEADER AD

HEADER AD

DC MASWA AONYA UCHAFU HALMASHAURI YA MJI

Na Samwel Mwanga, Maswa

WAKATI wananchi wa mji wa Maswa katika mkoa wa Simiyu wakiendelea na harakati za kuhakikisha Mamlaka ya mji mdogo huo inakuwa halmashauri ya mji,Mkuu wa wilaya hiyo,Aswege Kaminyoge amesema ili jitihada hizo zifanikiwe lazima usafi ufanyike tofauti na hali ilivyo sasa.

Akizungumza leo mjini Maswa, januari 31,2025 wakati akizindua baraza la mamlaka hiyo amesema viongozi wa baraza hilo wanatakiwa kusimamia suala la usafi kwani mji huo ni mchafu kutokana na tabia ya watu kutupa taka hovyo.

Amesema kuwa wajumbe hao kwa umoja wao waisimamie mamlaka hiyo kwa kushauriwa na wataalam waliopo kwa kufuata miongozo, taratibu na sheria zilizopo ili kuhakikisha mji huo unakuwa safi

        Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge(aliyesimama)akizindua baraza la mamlaka ya mji mdogo wa Maswa.

“Katika kipindi chenu cha uongozi kuanzia mwaka 2025 hadi 2030 mkatengeneze historia ya kuupandisha mji wa Maswa hadhi kuwa halmashauri ya mji, ni lazima kwanza tusimamie suala la usafi katika mji wetu”amesema.

Amesema kuwa kuna haja ya baraza hilo kuweka mikakati mahususi ya kukabiliana na uchafu ikiwa ni pamoja na kusimamia sheria ndogo za usafi zilizowekwa na mamlaka hiyo.

“Ni ukweli usiopingika kwa macho tunaona mji wetu si msafi,ukitoka nje sasa hivi ni masika ni mapori ndani ya mji wa Maswa nani anayestahili kusimamia ni sisi hivyo tusimamie sheria ndogo za usafi zilizowekwa na mamlaka yetu.”amesema.

Naye Suzan Kisehna mfanyabiashara wa sokoni mjini Maswa amesema kuwa mji huo hauwezi kuwa safi kama mamlaka ya mji mdogo wa Maswa haitadhibiti taka zinazotupwa hovyo hovyo.

       Sehemu ya wajumbe wa mamlaka ya mji mdogo wa Maswa wakati wa uzinduzi wa baraza la mji huo.


“Tukitaka kuwa halmashauri ya mji,lazima tuwe wasafi kwanza mfano hapa sokoni takataka zinalundikwa ndani ya soko na hadi zinaanza kutoa harufu,lakini viongozi wetu wakati mwingine wanakuwa kimya mpaka inakuwa kero,kama mkakati wa kupandishwa hadhi ya mji upo,basi mazingira yasafishwe na watu wapewe elimu ya kila mara watunze mazingira,”amesema.

Kwa upande wake,Slivester Lugembe mkazi wa mji huo amesema kuwa pamoja na ushauri na maelekezo yanayotolewa na viongozi wa serikali kuhusu Mamlaka hiyo hiyo kuimarisha usafi lakini pia wananchi wanalo jukumu la kubadili tabia kwa kuacha kutupa taka hovyo hasa nyakati za usiku kwenye maeneo ya wazi pamoja na kwenye makaburi.

“Mamlaka ya mji mdogo wa Maswa inaweza kusimamia usafi na kuja na mikakati ya kuufanya mji uwe safi lakini wapo wakazi wa mji huu wanakusanya taka kwenye nyumba zao na kuziweka kwenye viroba na baadaye nyakati za usiku kwenda kuzitupa kwenye maeneo ya wazi na  wengine kwenye eneo lililotengwa kwa ajili ya makaburi hasa eneo la ujenzi,”amesema.

Mwenyekiti wa Mamlaka hiyo,Caroline Shayo amesema kuwa moja ya malengo ya baraza hilo ni kuhakikisha wanaipandisha hadhi  mamlaka na kuwa halmashauri ya mji, hivyo moja ya vipaumbele ni kuuweka mji huo safi.

       Mwenyekiti wa Mamlaka ya mji mdogo wa Maswa,Caroline Shayo(aliyesimama)akizungumza mara baada ya baraza la mji huo kuzinduliwa mjini Maswa.

“Tutaisukuma ofisi ya Mtendaji Mkuu wa Mamlaka yetu kuhakikisha suala la usafi katika mji wetu linapewa kipaumbele ili tuweze kufikia malengo ya kupandisha hadhi na kuwa halmashauri ya mji,”amesema.

Mamlaka ya mji mdogo Maswa ilianzishwa mwaka  2010 kufatia tangazo la serikali la GN NO: 287 la mwaka 1993 lengo likiwa ni kusimamia maendeleo ya shughuli za kiuchumi.kisiasa na kijamii.

No comments