SHAIRI : UISHI KAMA KISIWA
UISHI kama kisiwa, usije ukafikiwa,
Jumba la kuangukiwa, na hata kuchafuliwa,
Ifikie kufukiwa, na pumzi kuishiwa,
Kuwasikiliza watu, waweza kuwa mtego.
Watu wamefanikiwa, kukwepa kusingiziwa,
Ni kisiwa kwenye ziwa, si rahisi kufikiwa,
Wamekaa sawasawa, kwa mawimbi wakingiwa,
Kuwasikiliza watu, waweza kuwa mtego.
Vile unavyoambiwa, usiweze kufikiwa,
Mishale unatumiwa, ili sumu kupatiwa,
Ngao hiyo unapewa, usiweze ingiliwa,
Kuwasikiliza watu, waweza kuwa mtego.
Ni watu wamejaliwa, kama shoti wametiwa,
Maneno ya kuambiwa, maanani yatiliwa,
Hata yasoaminiwa, na hayo wabarikiwa,
Kuwasikiliza watu, waweza kuwa mtego.
Hasira wanaingiwa, hatua zachukuliwa,
Maneno waliyopewa, hayo yanafwatiliwa,
Kesi zinafunguliwa, na hata kupaliliwa,
Kuwasikiliza watu, waweza kuwa mtego.
Wewe uliye kisiwa, likija la kuambiwa,
Kwako linakubaliwa, bila ya kuhakikiwa,
Maamuzi yatolewa, si yako ya kupangiwa,
Kuwasikiliza watu, waweza kuwa mtego.
Wadhani wafurahiwa, rafiki wa kuzaliwa,
Kumbe taka wabebewa, uweze kuchafuliwa,
Watoka kwenye kisiwa, hapo ndipo watekewa,
Kuwasikiliza watu, waweza kuwa mtego.
Akili ya kuambiwa, huko tulishaambiwa,
Ili kutovurugiwa, usifanye kuvamiwa,
Kwa pupa sijezolewa, na wimbi kuchukuliwa,
Kuwasikiliza watu, waweza kuwa mtego.
Huko unakoambiwa, yao yametatuliwa,
Au wewe waambiwa, mboga uweze mwagiwa?
Mabaya ukifikiwa, ubaki unazomewa?
Kuwasikiliza watu, waweza kuwa mtego.
Hivi na nani wajiwa, ya kwake umeambiwa?
Vipi anaaminiwa, hayo unayoambiwa?
Vipi wathibitishiwa, yale yaliyosikiwa?
Kuwasikiliza watu, waweza kuwa mtego.
Ni bora uwe kisiwa, vigumu wa kufikiwa,
Mawimbi utapepewa, uipate nzuri hewa,
Huko ni kufanikiwa, kukwepa ya kuambiwa,
Kuwasikiliza watu, waweza kuwa mtego.
Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
Post a Comment