VIGOGO CHAWASA WADAIWA KUIBA MAJI KUMWAGILIA MASHAMBA YAO
Na Daniel Limbe, Chato
BAADHI ya viongozi wa mamlaka ya maji mjini Chato (CHAWASA) iliyopo mkoani Geita wametuhumiwa kuchepusha maji ya mamlaka hiyo na kuyaingiza kwenye mashamba ya kilimo cha umwagiliaji wa mpunga kinyume cha sheria.
Pasipo kujali malalamiko ya baadhi ya wananchi kukosa huduma hiyo kwa takribani miaka miwili na wengine wakipata maji kwa mgao usioeleweka kikomo chake, imebainika maji mengi huelekezwa kwenye mashamba ya vigogo hao.
Wakizungumza na waandishi wa habari waliofika kujionea uhujumu wa miundo mbinu ya maji kwenye kitongoji cha mtakuja B, kata ya Muungano wilayani hapa,Leonard Shilengwa na John Daud, wamesema kilimo hicho kimekuwa kikifanywa kwa kutumia maji ya mamlaka hiyo pasipo kuwa na dira yoyote ya kusoma gharama za maji yanayotumika.
Wananchi wakiwa wamekusanyika kujionea maji yalivyo chepushwa kuelekea mashambani.Wamesema mchezo huo mchafu umekuwa ukifanyika kwa takribani misimu mitatu ya kilimo ukiwahusisha watumishi wa mamlaka hiyo(majina tunayahifadhi) kujinufaisha kwa maslahi binafsi kinyume cha sheria,huku kigogo mmoja akimwagilia takribani hekari 10 za shamba la mpunga na mwingine akiwa na hekari tano.
Mwenyekiti wa kijiji cha Kahumo,Paulo Manyilizu, mbali na kusikitishwa kwa kitendo hicho cha watumishi kukosa uzalendo kwa taifa lao,amesema changamoto kubwa ya uhaba wa maji imekuwa ikiwakumba watumishi wa Kituo cha afya Nyabilezi,uwanja wa ndege wa Geita uliopo chato pamoja na wakazi wa kijiji cha Buzirayombo ambao wanahudumiwa kupitia bomba hilo.
"Hili bomba ndilo linalokwenda kuhudumia kule uwanja wa ndege,Kituo cha afya Nyabilezi na wananchi wa Buzirayombo, maeneo yote hayo wanalia kwa kukosa maji hata baada ya kubaini wizi huu wa maji nimewasiliana na watumishi wa kituo cha afya Nyabilezi nao wamekiri hakuna maji kituoni hapo,maji yote yameelekezwa kwenye mashamba haya" amesema
"Wananchi 11 wamelipia kila mmoja sh. 120,000 tangu mwaka 2022 ili waunganishiwe huduma ya maji kwenye kijiji changu,hata ziara ya Waziri wa maji alipotembelea wilayani hapa mwaka jana aliagiza wananchi wangu wapewe huduma ya maji lakini mpaka leo hakuna kilichofanyika zaidi ya kuambiwa jambo hilo linashughulikiwa" amesema
Diwani wa kata ya Muungano,Charles Kapembe,amesema mchezo huo wa kuhujumu miundo mbinu ya maji kwenye kata hiyo huenda ndiyo chanzo cha wananchi wake kukosa huduma ya maji safi na salama na kwamba hali hiyo imesababisha adha kubwa kwa jamii baada ya kutumia gharama kubwa kujitibu magonjwa ya matumbo.
Mwonekano wa mpira unaopeleka maji kwenye mashamba ya mpunga."Nashukuru nami nimefika hapa kujionea wizi huu mkubwa wa maji,hakika nawapongeza sana wananchi kwa uzalendo wao kwa taifa hili,maana kama siyo wao huenda mchezo huu usingejulikana haraka nachoiomba serikali itimize wajibu wake kwa wote waliohusika na wizi huu".
"Kama mnavyoona wenyewe hapa hakuna dira yoyote inayosoma maji hayo, maji yote yanayomwagilia mashamba haya yanawanufaisha wachache kwa maslahi yao,hii haikubariki lazima hatua za kisheria zichukuliwe" amesema Kapembe.
Akijibu tuhuma zilizoelekezwa kwenye Mamlaka yake, Mkurugenzi wa mamlaka ya maji mjini Chato (CHAWASA) Mhandisi Isack Mgeni, amekiri kuwepo kwa wizi wa maji uliofanywa na mmoja wa viongozi wa mamlaka hiyo pia tuhuma hizo zikimhusisha aliyekuwa mkurugenzi wa mamlaka hiyo kabla ya uteuzi wake kutenguliwa mwaka jana na kwamba hatua za awali zimeanza kuchukuliwa kwa watuhumiwa hao.
Amesema tayali mtumishi mmoja,amekamatwa na jeshi la polisi kwaajili ya mahojiano zaidi, na kwamba mamlaka yake inaandaa utaratibu wa kumsimamisha kazi kabla ya uamuzi mwingine kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na kutazama sheria ina sema nini katika kulipa faini ya kosa kama hilo.
"Huyo mmoja ni mfanyakazi wa mamlaka yetu hatua tumeanza kuzichukua haraka ikiwemo kumsimamisha kazi,lakini huyo mwingine kwa kuwa siyo mtumishi wetu tena baada ya kustaafishwa naye tunatazama sheria inasema nini ili kulipa faini au kufikishwa mahakamani" amesema Mgeni.
Awali wakati waandishi wa habari wakifanya mahojiano na wananchi walioibua sakata hilo eneo la shamba la umwagiliaji,aliyekuwa mkurugenzi wa mamlaka hiyo kabla ya kutenguliwa,Mhandisi Mali Misango, alifika eneo hilo na kuanza kuporomosha matusi kwa waandishi pamoja na wananchi huku akijigamba kwa elimu na mafanikio yake.
Wakubwa WOTE wamefumba macho WAKATI issue wanaifahamu
ReplyDelete