HEADER AD

HEADER AD

SHAIRI: NIMEFANYWA MSHUMAA


ANAPONIJIA mtu, shida zinapombana,

Kwa sababu za kiutu, siwezi nikamkana,

Lakini mbona majitu, yaniliza kila kona?

Nimefanywa mshumaa, wema hakika ujinga.


Wenyewe wateketea, huku mwanga unanona,

Mali inanipelea, mwingine fuko latuna,

Enda akichekelea, huku mimi kijibana,

Nimefanywa mshumaa, wema hakika ujinga.


Mtu aja analia, hajapata hata nguna,

Kwa macho namwangalia, asema kweli naona,

Pesa nikimpatia, yeye anapiga kona,

Nimefanywa mshumaa, wema hakika ujinga.


Wasema dini murua, wenye shida kuwaona,

Si wa nguo za hariri, ni walopigika sana,

Sio wacheza kamari, majanga yamewabana,

Nimefanywa mshumaa, wema hakika ujinga.


Naona yangu huruma, yaniletea sonona,

Namba miye naisoma, jinsi wanavyonikana,

Hata shamba la kulima, pembejeo ni hakuna,

Nimefanywa mshumaa, wema hakika ujinga.


Juzi alikuja Judi, mtoto wa Kinyamana,

Alalamika baridi, homa kali membana,

Ile bima yenye kadi, nyumbani hajaiona,

Nimefanywa mshumaa, wema hakika ujinga.


Nikamkopesha pesa, anilipe mwezi jana, 

Hadi sasa kanitosa, njiani tunakwepana,

Wema wangu ni mkasa, roho tunaumizana,

Nimefanywa mshumaa, wema hakika ujinga.


Yule wa toroli langu, hataki hata niona,

Alikuja homu kwangu, mzigo umembana,

Katumia siku nyingi, kabaki na yangu zana,

Nimefanywa mshumaa, wema hakika ujinga.


Nilikuwa na rafiki, toka tukiwa vijana,

Alipita kwenye dhiki, akakosa mdhamana,

Akaja kindakindaki, tatizo lipombana,

Nimefanywa mshumaa, wema hakika ujinga.


Mimi akanililia, akitafuta kupona,

Na nilipomwangalia, njaa limkaba sana,

Bila chochote kutia, angekufa tu naona,

Nimefanywa mshumaa, wema hakika ujinga.


Mkopo akaniomba, ale na nguo kushona,

Na mimi nikamuomba, rehani yenye maana, 

Akazuga kenda shamba, haazimi pesa tena,

Nimefanywa mshumaa, wema hakika ujinga.


Kama kimuona mtu, bahili aonekana,

Usidhani hana utu, mambo mengi kakumbana,

Yamefanya awe butu, watu wakiomba dona,

Nimefanywa mshumaa, wema hakika ujinga.


Hebu uje kunikopa, rehani tutapatana,

Hunayo ondoka hapa, kwangu ndani hutaona,

Acha unione papa, jambo hapendi Rabana,

Nimefanywa mshumaa, wema hakika ujinga.


Shairi limetungwa na Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments