HEADER AD

HEADER AD

UVIKO ILIYOPITA, KAMA IMERUDI TENA



TAHADHARI ya ugonjwa, tayari imetolewa,

Watu kadha wanagonjwa, ndivyo tulivyoambiwa,

Sisi tusio wagonjwa, hili vema kuelewa,

UVIKO iliyopita, kama imerudi tena.


Wapo wanasimulia, ya kwamba wamepitiwa,

Asante wamesalia, tupate kusimuliwa,

Wengine wameishia, twasema wametwaliwa,

UVIKO iliyopita, kama imerudi tena.


Zamu hii inatisha, jinsi tunafanyiziwa,

Inavamia maisha, bila ya kujielewa,

Mara pumzi yaisha, uhai wakatiliwa,

UVIKO iliyopita, kama imerudi tena.


Kazi sasa kujikinga, tusije tukafikiwa,

Piga chafya domo kinga, mate tusijefikiwa,

Hiyo kwetu njema kinga, bora kama twaelewa,

UVIKO iliyopita, kama imerudi tena.


Vitu vya maambukizi, siyo vya kusogelewa,

Ukishika hivyo wazi, waweza ukafikiwa,

Uwasake wauguzi, wakati unapaliwa,

UVIKO iliyopita, kama imerudi tena.


Kama mtu anaumwa, UVIKO hujaelewa,

Na akili ukatumwa, apate kusogelewa,

Nawe waweza kuumwa, hili vema kuelewa,

UVIKO iliyopita, kama imerudi tena.


Tahadhari ni muhimu, kama mtu ahisiwa,

Pale ukimhudumu, hakika kuielewa,

Hapo waweza kudumu, usijeukavamiwa,

UVIKO iliyopita, kama imerudi tena.


Dalili ugonjwa huu, homa kali kupitiwa,

Kikohozi juujuu, kikavu unafikiwa,

Kupumua muda huu, shida unaingiliwa,

UVIKO iliyopita, kama imerudi tena.


Chakula unakipenda, ladha unapotelewa,

Koo kichwa vinadunda, maumivu wazidiwa,

Hapo sipitali nenda, kwa vipimo kufanyiwa,

UVIKO iliyopita, kama imerudi tena.


Kujikinga na kadhia, mikono sabuni nawa,

Na vitakasa tumia, hivi unanielewa,

Kitumia hizi nia, huwezi ukafikiwa,

UVIKO iliyopita, kama imerudi tena.


Wakati unakohoa, kujifunika elewa,

Chafya uzijekutoa, wengine wakavamiwa,

Hivyo vaa barakoa, pale inahitajiwa,

UVIKO iliyopita, kama imerudi tena.


Epuka mikusanyiko, isiyo lazima sawa,

Na UVIKO chanjo iko, ni vema ukapatiwa,

Hapo usalama wako, vema utaangaliwa,

UVIKO iliyopita, kama imerudi tena.


Tambua hakuna tiba, UVIKO ukijiliwa,

Ni dalili kuzikaba, tatizo kudhibitiwa,

Tahadhari zote beba, na ziweze kutumiwa,

UVIKO iliyopita, kama imerudi tena.


Na tulio wa imani, Mungu tunaomwelewa,

Vema kwenda magotini, tuombe tutasikiwa,

Kwamba tusiwe shidani, UVIKO tukazidiwa,

UVIKO iliyopita, kama imerudi tena.


Mtunzi ni Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments