HEADER AD

HEADER AD

UMEFIKIA WAKATI WA VITENGE NA KHANGA

ULE muda mefikia,  wa zawadi kuzitoa,

Jimboni watarejea, shida kuwaulizia,

Nasaha watazitoa, mengi wataelezea,

Tujiepushe na khanga hiyo ni hongo ya wazi.

Tusikubali jamani, kudanganywa na sukari,

Tuungane kwa yakini, tupeane na habari,

Kamwe tusiwaamini, watu hao ni hatari,

Tujiepushe na khanga hiyo ni hongo ya wazi.

Watapita mitaani, na sukari mikononi,

Watajitwisha vichwani, na kuzigawa jimboni,

Wala tusizithamini, ni waongo asilani,

Tujiepushe na khanga hiyo ni hongo ya wazi.

Wanaotoa rupia, hawatufai jamani,

Vigezo hawana pia, rushwa wanaithamini,

Moyoni hawana nia, tutajutia mwishoni,

Tujiepushe na khanga hiyo ni rushwa ya wazi.

Na sabuni watatoa, hata na zile kofia,

Na bati watazitoa, mchele na nguo pia,

Akili watatumia, ya watu kuwahadaa,

Tujiepushe na khanga hiyo ni rushwa ya wazi.

Maneno yao mazuri, yanavutia hakika,

Yanasikika vizuri, ni yenye nguvu hakika,

Wanasema kwa uzuri, tena bila ya mashaka,

Tujiepushe na khanga hiyo ni rushwa ya wazi.

Nimefikia mwishoni, saba ni wa ukingoni,

Kura yetu tuthamini, kwa kiongozi makini,

Tumpate wa thamani, mwenye watu kuthamini,

Tujiepushe na khanga hiyo ni hongo ya wazi.

Mtunzi ni SirDody- Kilimanjaro

0762396923 au 0675654955

No comments