KAZI YENU KIMYA KIMYA
KAZI yenu kimya kimya, mpo ni kama hampo,
Mwatembea kimya kimya, twaridhika mkiwepo,
Mbele yenu tuko kimya, twajua amani ipo,
Ulinzi wa nchi yetu, wawategemea ninyi.
Usalama wa mipaka, bila ya ninyi haupo,
Wavamizi wangebweka, tukakipata kichapo,
Hawawezi kusikika, kwa sababu ninyi mpo,
Ulinzi wa nchi yetu, wawategemea ninyi.
Mmethibitisha kweli, sawa sawa na kiapo,
Kazi zote za akili, mwazifanya tungalipo,
Ndiyo mana serikali, yaweka hapo mlipo,
Ulinzi wa nchi yetu, wawategemea ninyi.
Mmefanya mengi sana, na heshima ingalipo,
Ukombozi wa kufana, mwajulikana na Swapo,
Amini mlimvuna, kumbukumbu bado ipo,
Ulinzi wa nchi yetu, wawategemea ninyi.
Kazi za kimataifa, huko nako ninyi mpo,
Kuzuia watu kufa, vita za papo kwa papo,
Nyie wa kimataifa, Lebanoni nako mpo,
Ulinzi wa nchi yetu, wawategemea ninyi.
Wilayani mikoani, huko kote ninyi mpo,
Hata kazi wizarani, mnafanya kwa kiapo,
Jinsi mlivyo makini, mnapendwa mkiwepo,
Ulinzi wa nchi yetu, wawategemea ninyi.
Ninyi egemeo letu, majanga mengi kiwepo,
Mwaokoa ndugu zetu, mafuriko yakiwepo,
Amani ikiwa butu, twatulia mkiwepo,
Ulinzi wa nchi yetu, wawategemea ninyi.
Imani kwenu ni kubwa, popote pale mlipo,
Wala hatuwezi kabwa, sare zenu zingalipo,
Wabaya wote wabebwa, na kupatiwa kichapo,
Ulinzi wa nchi yetu, wawategemea ninyi.
Endeleza kutimiza, kazi yenu ya kiapo,
Nasi tunaikoleza, imani hapo mlipo,
Ya kwetu tutatimiza, vile muda ungalipo,
Ulinzi wa nchi yetu, wawategemea ninyi.
Mtunzi ni Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
Post a Comment