HEADER AD

HEADER AD

…SIYO CHINI YA MKANDA - 1

WAJUKUU wa kiume, hekima hiyo pokea,

Tulieni myasome, yaweze kuwakolea,

Ikibidi yawaume, na mema kuwachochea,

Heshima kuwajibika, siyo chini ya mkanda.

Bibi yenu kachukia, uvivu awatolea,

Yale mnajifanyia, mbele mkiendelea,

Huku mkifikiria, ujiko yanawagea,

Heshima kuwajibika, siyo chini ya mkanda.

Kwamba wengi wanaume, tamaa yawachochea,

Warembo wawatazame, na kisha kuwatokea,

Kwenye zinaa wazame, hadi inawakolea,

Heshima kuwajibika, siyo chini ya mkanda.

Bibi awaonya sasa, maonyo yake pokea,

Msiendeleze visa, wanawake kutokea,

Mnadhani hiyo fursa, kumbe mwazidi potea,

Heshima kuwajibika, siyo chini ya mkanda.

Mabinti wengi warembo, dunia yawaletea,

Msifuate mkumbo, nao hao kutembea,

Mkadhani hilo chimbo, mahaba kujichotea,

Heshima kuwajibika, siyo chini ya mkanda.

Wanaozaliwa wengi, wanyange utapotea,

Hata uwatake wengi, kuja wanaendelea,

Hapo huupigi mwingi, utu wajiondolea,

Heshima kuwajibika, siyo chini ya mkanda.

Uwatake Tanzania, wote wa kujichotea,

Njiani utaishia, vile watakupotea,

Ni wengi wanaingia, zaidi wamekolea,

Heshima kuwajibika, siyo chini ya mkanda.

Mjukuu wa kiume, wosia huu pokea,

Hebu oa mwanaume, mema utayapokea,

Si kotekote uzame, mabaya tajichochea,

Heshima kuwajibika, siyo chini ya mkanda.

Na kijana wa kiume, na elimu endelea,

Usichanganye usome, karama yako chochea,

Kesho matunda uchume, mke utampokea,

Heshima kuwajibika, siyo chini ya mkanda.

Kama wewe mcha Mungu, kuamini endelea,

Dini ikupige pingu, wake kutowamezea,

Mazoezi yako nyungu, tamaa italegea,

Heshima kuwajibika, siyo chini ya mkanda.

Mtunzi ni Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments