HEADER AD

HEADER AD

HALMASHAURI KIBAHA YAPIMA VIWANJA NA KUWAPA WANANCHI HATIMILIKI

 


Na Gustaphu Haule, Pwani 

HALMASHAURI ya Manispaa ya Kibaha chini ya mkurugenzi wake Dkt .Rogers Shemwelekwa imefanikiwa kumaliza migogoro ya ardhi katika Kata ya Pangani baada ya kupima viwanja 18000 na kukabidhi hatimiliki kwa Wananchi wa Kata hiyo.

Hafla ya uzinduzi wa ugawaji wa hatimiliki za viwanja kwa Wananchi hao imefanyika Septamba 03,2025 chini ya Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson John huku ikihudhuriwa na wananchi pamoja na baadhi ya maafisa watendaji wa Kata mbalimbali.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa hiyo Dkt . Rogers Shemwelekwa amesema kuwa aliona jambo hilo alishughulikie kwa haraka  ili kuwapunguzia ugumu wa maisha Wananchi wake lakini hatahivyo jambo hilo tayari limepata ufumbuzi.

        Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dkt. Rogers Shemwelekwa akizungumza na Wananchi wa Kata ya Pangani ikiwa ni sehemu ya uzinduzi wa hafla ya ugawaji hati miliki za viwanja kwa wananchi hao.

Amesema kuwa katika utekelezaji wa jambo hilo wamekubaliana mtu akikamilisha malipo yake wanazibeba nyaraka zake hadi kwa kamishna wa ardhi na hati ikiwa tayari wanamletea mwananchi papo hapo bila usumbufu.

Shemwelekwa amesema kuwa viwanja walivyopewa Wananchi hao vimepewa namba na kiwanja kinasoma kwenye ramani lakini lipo tatizo ambalo miongoni mwao la kugawa vipande vya ardhi kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi na kuviuza.

Amesema kufanya hivyo ni kosa kisheria kwani ni utapeli na pia wanaharibu kwasababu kiwanja wanachokiuza kimeshasajiliwa na kwamba mtu anayeuziwa hawezi kusajiliwa tena.


      Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dkt. Rogers Shemwelekwa wa pili kutoka kulia akimkabidhi ramani ya Kata ya Pangani kwa mmoja wa afisa wa Kata hiyo katika hafla iliyofanyika Septemba 03,2025.

"Mimi nawaomba msije mkagawa kipande na kuuza na kama unataka kuuza basi ni vyema ukauza kizima kwakuwa mali ni yako na hakuna wakuzuia,"amesema Mkurugenzi.

Shemwelekwa amesema kama wanachangamoto ni vizuri wakawatumia viongozi wao wakiwemo wenyeviti wa Mitaa na wasijaribu kuwatumia makanjanja kwakuwa ndio mara zote wanakuwa chanzo cha migogoro.

Amesema kuwa wao wamepewa majukumu na Rais Dkt .Samia Suluhu Hassan na kazi yao ni kuwahudumia wananchi ndio maana hakuna mwananchi aliyekwenda katika ofisi yake akaondoka na  machozi na aliyekwenda na machozi ameondoka na faraja.

Amesema wapo watu wamekaa na migogoro miaka Sita na wengine miaka 10 lakini walipofika katika ofisi yake wamefanikiwa kutatua mgogoro na maisha yanaendelea ambapo amewaomba kuacha kupotozwa na watu wa Mitaani na badala yake waende katika ofisi za Serikali kwa ajili ya kupata ufumbuzi wa changamoto zao.

         Wananchi wa Kata ya Pangani katika Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha wakiwa katika mkutano wa uzinduzi wa ugawaji hati miliki za ardhi hafla ambayo imefanyika Septamba 03,2025 katika viwanja vya ofisi ya Mtendaji Kata ya Pangani iliyopo Mtaa wa Kidimu.

Msajili wa hati msaidizi wa Mkoa wa Pwani Burton Rutta lengo la kutoa hati hizo ni kuhamasisha wale ambao hawajalipa waende wakalipie ili kuhakikisha wanapewa hati zao kwa wakati kama ambavyo wengine wamepewa.

Amesema hati zilizotolewa zitadumu miaka 66 hadi 99 na kinachotakiwa ni kuhakikisha hati hizo zinahifadhiwa katika sehemu salama ili zisiweze kuharibika.

Rutta amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita chini ya Dkt.Samia Suluhu Hassan imerahisisha mambo mengi kwani maombi ya kumiliki ardhi ni Sh.5000 kwani awali gharama zilikuwa juu na sasa zimeshuka kwa asilimia 25.

Pia amesema kuwa Serikali ya Rais Samia imeondoa urasimu wa utoaji wa hatimiliki ya ardhi kutoka miezi sita hadi wiki mbili ambapo amewahamasisha Wananchi hao kutumia vizuri fursa hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya a Kibaha Nickson John amesema Kata ya Pangani wamepima viwanja 18000 na wamezindua kwa kugawa hati 180 huku akisema hati nyingine 7000 zipo tayari na zinasubili wahusika wakimaliza kulipia wanapewa hati zao.

Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson John (Kulia) akikabidhi hati kwa Mwananchi wa Kata ya Pangini (kushoto) na katikati ni Msajili wa hati msaidizi wa Mkoa wa Pwani Burton Ruttaa.

Mmoja wa Wakazi wa  Kata ya Pangani akiwemo Clementina Mwankeja amesema kuwa amefurahi kuona Serikali imefanyakazi kubwa katika Kata yao ambapo ameomba wanapopita kupima ardhi ni vyema wakawahusisha wenyeji ili kuondoa migogoro ya mipaka.

Mwanahamisi Mangu amemshukuru mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha kwa hatua kubwa aliyoifanya kwani wameteseka miaka mingi na migogoro ya ardhi lakini kwasasa imekwisha .

Hatahivyo, Mangu amesema kwasasa ameridhishwa na viongozi wa Serikali kutoka Manispaa ya Kibaha kwakuwa wamekuwa watu ambao wanafanyakazi ya kusikiliza changamoto za Wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.

       Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson John (wa kwanza Kulia )akiangalia ramani ya Kata ya Pangani katika hafla ya ugawaji hatimiliki kwa wananchi wa Kata hiyo Septemba 03,2025

No comments