PUNDA AMEKOSA NINI?
PUNDA amekosa nini, wafugaji nijibuni,
Ni ipi yake thamani, wafugaji nijuzeni,
Punda yupo mashakani, ana shida maishani,
Punda amekosa nini wafugaji nijibuni.
Mizigo mwambebesha, sokoni kuelekea,
Punda mnamkondesha, kwa mizigo kuzidia,
Wafugaji mnatisha, kwa punda kuwaonea,
Punda amekosa nini wafugaji nijibuni.
Kutwa mnamfungia, akishafika sokoni,
Masikini analia, pale mtini Jamani,
Njaa anaposikia, mnamnyima majani,
Punda amekosa nini wafugaji nijibuni.
Waoneeni huruma, punda wana haki pia,
Wapeni pia huduma, ya maji chakula pia,
Punda pia ni wanyama, huduma wahitajia,
Punda amekosa nini nijibuni wafugaji.
Ana vidonda, mwilini, na makovu miguuni,
Kaharibika shingoni, nayasema si utani,
Si leo tangu zamani, punda yupo mashakani,
Punda amekosa nini nijibuni wafugaji.
Sita ni wa ukingoni, shairi ninalitoa,
Wafugaji nijibuni, kwa kina nasubiria,
Majibu nipatieni, nami nataka kujua,
Punda amekosa nini nijibuni wafugaji.
Sirdody.
Soyakijijini@fmail.com
0675654955 au
0762396923.
Kilimanjaro Tanzania.
Post a Comment