HEADER AD

HEADER AD

MAISHA PIGA HATUA

KWENYE hofu songa mbele, wala usirudi nyuma,

Usingoje hofu ile, iishe umesimama,

Wewe angalia mbele, hofu yote itakoma,

Maisha piga hatua, kama nyumbu Serengeti.

Nyumbu wanasonga mbele, hawaangalii nyuma,

Japo mto uko mbele, hakuna kurudi nyuma,

Hata mamba wako mbele, hawabaki wakagoma,

Maisha piga hatua, kama nyumbu Serengeti.

Mambo ya kutisha tele, ambayo yatuandama,

Mengine yana kelele, hata kimya yatulima,

Bado twanyanyua dole, mbele kwa mbele twavuma,

Maisha piga hatua, kama nyumbu Serengeti.

Muda wa kusonga mbele, wala si wa kusimama,

Nyumbu hao wako mbele, kama muda wa kuhama,

Mbio wanasonga mbele, wala hawarudi nyuma,

Maisha piga hatua, kama nyumbu Serengeti.

Katika kusonga mbele, unaweza ukazama,

Hiyo kwa wengine shule, nao wasije kukwama,

Lakini fursa tele, mbele zaweza simama,

Maisha piga hatua, kama nyumbu Serengeti.

Maendeleo ni mbele, wala si kurudi nyuma,

Kama umekwenda shule, sio mwisho wa kusoma,

Umejenga nyumba ile, ujenzi usijekoma,

Maisha piga hatua, kama nyumbu Serengeti.

Chura mwangalie vile, teke ni hatua njema,

Hapo hapigi kelele, kwamba yeye amekwama,

Bali anaruka mbele, hapo hawezi simama,

Maisha piga hatua, kama nyumbu Serengeti.

Akili unazo tele, ili kukwepa kukwama,

Ni vema ujitawale, ili usije kuzama,

Taratibu songa mbele, mbele nyama utachoma,

Maisha piga hatua, kama nyumbu Serengeti.

Kumbuka wazee wale, likufanya ukasoma,

Wewe pita mle mle, watoto wapate soma,

Wasifike pale pale, lipokufikisha mama,

Maisha piga hatua, kama nyumbu Serengeti.

Kimuona yuko vile, maisha amesimama,

Sidhani yake ni lele, na yako ukiyapima,

Jua amesota yule, penginepo ungezima,

Maisha piga hatua, kama nyumbu Serengeti.

Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com 0767223602

No comments