MBUNGE BUKOBA MJINI AWAHIMIZA WAANDISHI WA HABARI KUITANGAZA MIRADI YA MAENDELEO

Na Alodia Dominick, Bukoba
MBUNGE wa jimbo la Bukoba mjini mkoani Kagera, Mhandisi Jonhston Mutasingwa amewaomba waandishi wa habari kutoa ushirikiano kwa viongozi walioko madarakani na kuitangaza miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa kwa kuandika habari za mwendelezo katika manispaa hiyo.
Mutasingwa ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari aliposhiriki chakula cha mchana na waandishi hao na kutaja umuhimu wao kuwa, ni kuhakikisha kuwa habari zinazotolewa zinasaidia jamii kupata taarifa sahihi na za kina kuhusu miradi mbalimbali inayotekelezwa.
"Endapo zitaandikwa habari za kuchochea miradi ya maendeleo zitachangia vyombo vyetu vya habari na waandishi kuongeza kipato kwa sababu ikiwa ni gazeti wananchi watahakikisha wananunua magazeti ili wasome kinachoendelea.
" Mitandaoni lazima watafungua, watasikiliza radio na kuangalia Televisheni hivyo zitaongeza watazamaji" amesema Mhandisi Mutasingwa.
Ameeleza kuwa, wanataluma ya habari watumie kalamu zao kuibua habari zenye kuvutia wasomaji na watazamaji, wawe na mwendelezo wa habari wanazoziandika, alitolea mfano wa miradi mbalimbali ikiwemo ya barabara kwamba waandishi waandike kila hatua ya mradi huo mpaka utakapokamilika.
"Mfano, umeandika habari inayohusu ujenzi wa barabara ya njia nne fuatilia kila hatua hadi utakapokamilika ili wasomaji wapende kusoma, kusikiliza na kuangalia maana habari yenye mwendelezo inashawishi mtu aendelee kuifuatilia"ameeleza Mutasingwa.
Amesema itakaporipotiwa kila hatua jamii itatambua miradi hiyo imefikia hatua gani na faida zake ni zipi kwa sababu, inatekekezwa kutokana na kodi za wananchi.
Mhandisi Mutasingwa amesisitiza waandishi wa habari kutumia kalamu zao kuandika habari zenye kuchochea amani kwa sababu bila amani maendeleo hayawezi kupatikana.
Wakati huo huo , Mhandisi Mutasingwa,amewashauri waandishi hao wa habari kuibua habari za uchambuzi juu ya changamoto zinazowakabili wananchi ili zijulikane na kutafutiwa ufumbuzi wa kina na mamlaka husika.
Amani Kajuna mkazi wa mkoa wa Kagera ambaye pia alikuwa kampeni meneja wa mbunge huyo amesema, waandishi wa habari ni kioo cha jamii, ni macho ya viongozi na wananchi, ni sauti ya jamii nzima ya Taifa la Tanzania hivyo, ni vyema viongozi wakashirikiana na waandishi kwani safari ya siasa inalenga maendeleo na inahitaji ukaribu wa pamoja.
Nao baadhi ya waandishi wa habari wamesema kuwa, viongozi wakubali kuzungumza pale watakapohitajika kutolea ufafanuzi jambo fulani kwani wapo baadhi ya viongozi wakitafutwa huwa hawakubali kuzungumza na wengine wanatoa masharti ya mwandishi aandikeje, jambo ambalo ni kinyume na maadili ya uandishi wa habari.
Diana Deus ni mwandishi wa habari wa gazeti la serikali la Habari Leo amewaomba viongozi kuwa tayari kupokea changamoto zilizopo Bukoba mjini ili kuzitafutia ufumbuzi.
Aidha mhandisi Mutasingwa alikuwa ameambatana na meya wa manispaa ya Bukoba Acton Rwankomezi.



Post a Comment