HEADER AD

HEADER AD

DIWANI KATA YA TUMBI APATA UMEYA,AWATAKA WATENDAJI KUACHA KUFANYA KAZI KWA MAZOEA

Na Gustaphu Haule, Pwani

BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha limemchagua diwani wa Kata ya Tumbi kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt.Mawazo Nickas kuwa Meya wa kwanza wa Manispaa hiyo.

Nickas amechaguliwa katika uchaguzi uliofanyika Desemba 4/2025 katika ukumbi wa Manispaa hiyo ambapo Nickas aliibuka kidedea baada ya kupata kura 19 za madiwani walioshiriki uchaguzi huo.

Katika uchaguzi huo pia madiwani hao walimchagua Aziza Mruma diwani wa viti maalum (CCM)kuwa Naibu Meya wa Manispaa hiyo kwa kupata kura 19 za ndiyo sawa na idadi ambayo Meya wa Manispaa hiyo alizipata.

Akitangaza matokeo hayo Mwenyekiti wa uchaguzi huo ambaye ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Kibaha Moses Magongwa , amesema kuwa Baraza hilo linajumla ya madiwani 20 lakini diwani mmoja hakushiriki kutokana na sababu zilizonje ya uwezo wake.

      Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Mawazo Nickas.

Awali kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo , mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa amesema kuwa Manispaa ilipokea majina ya wagombea baada ya mchakato wa uchaguzi wa vyama vya Siasa kukamilika.

Amesema majina aliyopokea ni mawili likiwemo jina la diwani wa Kata ya Tumbi Dkt.Mawazo Nickas pamoja na jina la Aziza Mruma diwani wa Vitimaalum ambao wote wanatokana na Chama Cha Mapinduzi ( CCM).

Amesema Manispaa ya Kibaha imepata Meya wa kwanza kwa mujibu wa Sheria kwakuwa Kibaha ilipitishwa rasmi kuwa Manispaa Juni 2025  na Dkt .Nickas ndiye anayefungua njia ya U-meya .

Akizungumza wakati akifunga Baraza la kwanza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Meya wa Manispaa hiyo Dkt. Mawazo Nickas amewataka watendaji kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake wajikite kwenye kazi za kuwasaidia wananchi.

Amesema kama kuna mtendaji alikuwa anafanya kazi kwa mazoea kuanzia sasa aache maramoja kwakuwa yeye hataki mazoea ili kitu ambacho kitamtambulisha mtendaji ni kufanyakazi ambayo inaleta manufaa kwa Wananchi.

Amesema wananchi wanatarajia mambo makubwa kutoka kwa madiwani kwahiyo wao watafanyakazi kwa ajili ya maslahi ya Wananchi na kwakuwa walikubali kuwa madiwani basi wategemee kupata maendeleo makubwa.

        Diwani wa Kata ya Tangini kupitia CCM Anthony Milao (Kulia) akila kiapo katika mkutano wa Baraza la madiwani uliofanyika Disemba 4/2025 katika Manispaa ya Kibaha.

" Mimi sitaki rushwa,wala sitopokea rushwa ila ninachotaka kazi ifanyike kwa kuhakikisha tunasimamia vizuri miradi ya maendeleo pamoja na kuzitatua kero za wananchi ili na wao wapate kujivunia upatikanaji wa Manispaa yao",amesema Nickas.

"Wananchi wategemee maendeleo kwa kasi na kicheko, Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan anatoa fedha nyingi na anataka kuiona nchi ikibadilika kwa kasi na katika hili hatutavumilia mtendaji anayechelewesha maendeleo,"amesema.

Amewataka watendaji wa Manispaa ya Kibaha kujitathmini kwakuwa  baraza hilo linakwenda kusimamia matumizi ya fedha za wananchi kwa kutekeleza miradi ya maendeleo ili kusudi waweze kupunguza vilio vya changamoto na kero za Wananchi.

Nickas amewaomba  wananchi wenye kero kufika ofisini kwake na atawasikiliza na kuzitafutia utatuzi kwa haraka kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo na wakuu wa idara.

Hata hivyo, katika mkutano huo wa kwanza wa Baraza la madiwani kulifanyika shughuli mbalimbali ikiwemo kuapisha madiwani, kufanya uchaguzi wa Meya, kiapo cha maadili, kuunda kamati za madiwani pamoja na uwasilishaji wa taarifa mbalimbali za maendeleo.

      Mhariri wa Makala kutoka kampuni ya Uhuru Publication Selina Wilson (Kulia)ambaye pia ni diwani wa Vitimaalum ( CCM)akila kiapo katika baraza la madiwani la Manispaa ya Kibaha  lililofanyika Disemba 4/2025.


No comments