HEADER AD

HEADER AD

RC MTAKA : GEN - Z WANA WAJIBU WA KULINDA AMANI YA TANZANIA

Na Mwandishi wetu, Njombe 

MKUU wa mkoa wa Njombe, Antony Mtaka amesema vijana wa kizazi kipya maarufu (Gen -Z ) wana wajibu wa kulinda amani ya Tanzania kwani ndio kizazi kinachobeba matumaini na sura ya Taifa .

Ameyasema hayo juzi katika ibada ya kanisa la Waadventista Wasabato Njombe mjini.

Amesema kwamba amani ni tunda la haki na wajibu . Ni msingi thabiti wa maendeleo kama jamii na kama taifa, na kwamba ni wajibu wa kuilinda amani ya nchi  kwa wivu mkubwa.

" Ni jukumu letu vijana wa leo, kuitunza amani yetu kwa faida ya vizazi vilivyopo na vijavyo waikute Tanzania iliyo moja" amesema RC Mtaka.

Ameongeza kuwa, mkoa wa Njombe upo salama, hauna matishio ya kihalifu, huku akiwaomba wana Njombe kuendelea kujenga mazingira thabiti ya ulinzi wa watu na mali, ili kutoa fursa kwa wananchi kuendelea kufanya shughuli zao za uzalishaji mali na mahangaiko yao ya kujipatia kipato cha siku. 

"Usalama wa mkoa wetu, utatuongezea imani kwa wawekezaji wetu mbalimbali kuendelea kuamini kwamba Njombe ni mahala sahihi pa wao kuweka mitaji yao.

" Wana Njombe tushikamane kuhakikisha tunaziepuka aina zozote za chokochoko zitakazoashiria uhalibifu wa mali, uwekezaji, miradi ya umma na binafsi, au uharibifu wa uhai wa wananchi" amesema.

Ameongeza kusema " Wananchi wenzangu, mkiona au kuhisi dalili yoyote hata ndogo inayoashiria uvunjifu wa amani au kuhatarisha usalama wa eneo lenu au maisha ya mtu, basi mtoe au utoe taarifa mapema. Ulinzi shirikishi huanza na wanajamii mmoja mmoja kwa kutoa taarifa kwa wakati.” amesema RC Mtaka .

No comments