DED KIBAHA AWAKOSHA WALIMU , DC ATIA NENO
>>Ni baada ya changamoto ya Walimu ya upandishwaji Madaraja, Madeni kutatuliwa
Na Gustaphu Haule, Pwani
MKURUGENZI wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa ameibua shangwe kwa walimu wa Shule za Msingi na Sekondari waliopo katika Halmashauri hiyo baada kusema kuwa changamoto ya fedha za likizo na kupandishwa madaraja sasa limekwisha.
Dkt.Shemwelekwa ameibua shangwe hizo katika hafla ya kuwapongeza Walimu wa Shule za msingi na Sekondari waliofanya vizuri katika mitihani ya Kitaifa ya Mwaka 2025 hafla ambayo ilifanyika kwenye ukumbi wa Kibaha Shopping Mall Aprili 16/2026.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa akizungumza katika hafla ya kuwapongeza walimu wa Shule za Msingi na Sekondari waliofanya vizuri katika mitihani ya Kitaifa ya Mwaka 2025.Akizungumza katika hafla hiyo Shemwelekwa amesema kuwa wakati alipoteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha aliikuta changamoto kubwa za walimu ambazo ni kupandishwa madaraja pamoja na malimbikizo ya madeni hususani fedha za likizo.
Dkt.Shemwelekwa amesema kuwa changamoto hizo tayari amezifanyiakazi kama ambavyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan alivyotoa maelekezo na sasa madeni hayo yameanza kulipwa na yataendelea kulipwa.
Amesema kuwa walimu waliopangwa kwenda likizo Desemba 2025 walimu wote walilipwa na amehakikisha kuwa wale ambao watakwenda likizo Juni 2026 fedha zao zitaanza kulipwa Aprili 17/2026 na kwamba makusudio yake walimu wanapokwenda likizo hakuna atakayedai fedha zake.
"Fedha za walimu wanaokwenda likizo kwasasa si changamoto tena kwa Manispaa ya Kibaha kwakuwa limefanyiwa kazi na walimu wanapata haki yao kwa wakati na hata wale wanaoenda likizo Juni fedha zao zipo tayari na ifikapo Aprili 17/2026 zitaanza kuingia katika akaunti zao," amesema Shemwelekwa
Shemwelekwa amesema kuwa kinachoendelea kufanyiwa kazi sasa ni fedha za malimbikizo ambalo muda si mrefu litakwisha na kwamba amewaomba walimu kuendelea kufanyakazi kwa bidii kwakuwa changamoto zote zinafanyiwa kazi na kila Mwalimu atapata haki yake.
Amesema walimu ni watu muhimu na wamekuwa wakifanyakazi kubwa kwa faida ya Taifa la Tanzania na kwa kutambua umuhimu huo wameona ni vyema wakawapongeza walimu hao kwa kazi nzuri waliyoifanya mwaka 2025 kwa kuwapa zawadi mbalimbali ikiwemo vyeti,tuzo na fedha taslimu.
Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson Saimon ( kushoto) akimkabidhi mmoja wa walimu wa Manispaa ya Kibaha cheti cha pongezi kwa kufanya vizuri katika mitihani ya Mwaka 2025 na anayeshuhudia wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa.Kutokana na kauli alizotoa Mkurugenzi huyo,walimu wa Shule za msingi na Sekondari waliofurika katika ukumbi huo waliibuka na shangwe kubwa kwa ajili ya kumshangilia Mkurugenzi wao kutokana na kutatua changamoto zilizokuwa zinawakabili kwa muda mrefu.
Hatua hiyo ilipelekea walimu wakuu na wakuu wa Shule kwa niaba ya walimu wenzao kumpongeza Mkurugenzi huyo kwa kumpa zawadi mbalimbali ikiwemo zawadi ya cheti maalum cha pongezi .
Mmoja wa walimu hao kutoka Shule ya Msingi Tangini Jasmin Msuya amesema kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha amekuwa akifanyakazi nzuri kwani tangu amefika Kibaha wameona mafanikio makubwa katika sekta ya elimu.
Msuya amesema kubwa katika yote ni juu ya fedha za likizo kwa walimu ambapo mwaka 2025 aliyalipa lakini mwaka 2025 aliweza kutengeneza madawati 4000 na kugawa katika Shule mbalimbali lakini pia mwaka 2026 amefanikiwa kugawa tena madawati mengine 4000.
"Sisi walimu wa Manispaa ya Kibaha tunampongeza Mkurugenzi Dkt.Rogers Shemwelekwa kwa kazi nzuri na kwa hakika tumefurahi sana kwa namna ambavyo anagusa sekta ya elimu kwa upande wa kurekebisna miundombinu pamoja na kutatua changamoto za walimu ,"amesema Msuya.
Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson Saimon ametoa wito kwa walimu kuongeza bidii ya ufundisha ili kuweza kuzalisha wataalam wengi ambao watalisaidia Taifa kwa miaka ya baadae.
Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Kibaha Nickson Saimon katika hafla ya kuwapongeza walimu.Amesema kuwa walimu wavunje hofu kwa wanafunzi wanapokuja Shuleni na ikiwezekana wawajengee imani ya kuwa kila mwanafunzi anaweza kufanya vizuri kwakuwa sio kila mwanafunzi anatokea katika mazingira mazuri.
Amesema anawapongeza walimu kwa kazi nzuri na mafanikio yanayopatikana ndio maono ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye anapenda kuona Taifa linasongambele kimafanikio.
Saimon amesema kuwa wanaposherehekea mafanikio hayo ni safari mpya ya kuendea katika mafanikio mengine mapya na mafanikio hayo yanatakiwa kuwa makubwa zaidi na kwamba walimu wakipata tuzo sio kwamba wao ni bora kuliko wenzao bali ni sehemu ya kupeana chachu ya kufanyakazi.
Mwenyekiti wa hafla hiyo ambaye pia ni afisa elimu wa Manispaa ya Kibaha Theresia Kyara,amesema kuwa anamshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha miradi WA Boost unaosaidia masuala ya elimu .
Kyara amesema tangu kuanzisha kwa mradi huo, sekta ya elimu imefanikiwa kwa kujenga miundombinu mbalimbali ya madarasa ambayo inawasaidia wanafunzi kusoma katika mazingira mazuri.
Hatahivyo,amesema uwepo wa miundombinu hiyo ndiyo imesaidia wanafunzi wengi wa Shule za msingi na Sekondari na katika mwaka 2025 kufanya vizuri huku akisema mwaka 2026 mafanikio ya elimu yatakuwa makubwa zaidi.




Post a Comment