RC PWANI AELEZA WALIVYOJIPANGA MAPOKEZI YA MBIO ZA MWENGE WA UHURU
Na Gustaphu Haule, Pwani
MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema maandalizi ya mapokezi ya mbio za Mwenge wa Uhuru kutoka Jijini Dar es Salaam yamekamilika.
Amesema Mwenge wa Uhuru mwaka huu kwa Mkoa wa Pwani utapokelewa Aprili 18 katika viwanja vya shule ya msingi Mtambani iliyopo Kata ya Mapinga Wilayani Bagamoyo.
Kunenge ametoa kauli hiyo wakati akizungumza katika mkutano wake na Waandishi wa habari uliofanyika , Aprili 16, 2026 ofisini kwake kuhusu namna walivyojipanga kupokea Mwenge huo.
Amesema Mwenge wa Uhuru utatokea katika Jijini la Dar es Salaam ambapo Aprili 18 utaingia rasmi Mkoa wa Pwani na mapokezi yake yatafanyika Mapinga Wilayani Bagamoyo.
Kunenge amewaomba Wananchi wa Wilaya ya Bagamoyo pamoja na mkoa wa Pwani kiujumla kujitokeza kwa wingi kuulaki Mwenge huo kwakuwa Mwenge huo ni ishara ya heshima ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Amesema Mwenge wa Uhuru ukiwa katika mkoa wa Pwani utakimbizwa katika Halmashauri zote tisa ikiwemo Halmashauri ya Bagamoyo, Chalinze, Kibaha Vijijini,Kibaha Mjini ,Kisarawe,Mkuranga ,Kibiti ,Rufiji na Mafia.
.
Baadhi ya Waandishi wa habari wakiwa katika kikao na Mkuu wa mkoa wa Pwani kilichofanyika Aprili 16/2026 .
Amesema mbio za Mwenge wa Uhuru ni kichocheo kikubwa cha maendeleo ambapo ukiwa Mkoa wa Pwani utaweka mawe ya msingi na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo yenye lengo la kuboresha maisha ya Wananchi.
"Kauli mbiu ya Mwenge wa Uhuru mwaka huu inasema: “Tanzania ni yetu sote, Tushikamane kwa pamoja kuleta Maendeleo" kwahiyo niwaombe Wananchi wajitokeze kwa wingi siku ya mapokezi, " amesema .
Kunenge ameongeza kuwa kauli mbiu hiyo inahimiza ushirikiano, kudumisha amani na kufanya kazi kwa bidii ili kufanikisha maendeleo endelevu ya Taifa.
Hata hivyo amesema kuwa msimu wa mwaka 2025 Mkoa wa Pwani ulikuwa wa kwanza Kitaifa na mwaka huu Mkoa umejipanga vizuri kutetea nafasi hiyo.


Post a Comment