WATOTO WANNE WAPOTEZA MAISHA BAADA YA NYUMBA KUANGUKIWA NA UKUTA WA HOTELI YA PAFECT BUKOBA
Na Alodia Dominick, Bukoba
WATOTO wanne wa familia mbili tofauti katika mtaa wa Anyama kata ya Kibeta manispaa ya Bukoba mkoani Kagera , wamepoteza maisha baada ya nyumba walizokuwa wamelala kuangukiwa na ukuta wa hotel ya Pafect wakati mvua kubwa ikiendelea kunyesha majira ya alfajiri.
Tukio hilo limetokea April 17 mwaka huu majira ya saa 11:00 alfajiri wakati watoto hao wakiwa wamelala majumbani mwao, mvua kubwa ikiendelea kunyesha ukuta wa hotel ya Pafect uliangukia nyumba walizokuwa wamelala watoto hao na kusababisha vifo vyao.
.jpg)
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Bukoba Mkoa wa Kagera, Dkt Charles Kaigi amesema, wamepokea vifo vya watoto wanne, watatu wakiwa wa kike na mmoja wa kiume.
"Tumepokea vifo vya watoto wanne kutoka katika familia mbili tofauti, Familia ya Mikdadi Ally waloofariki ni Maniath Mikdadi (4) na Nunihan Mikdadi (10), familia ya Edimond Matungwa waliofariki ni Elizaberth Edimond (12) na Edwin Edimond (10)" amesema Dkt. Kaigi.
Amesema miili ya watoto hao baada ya kufanyiwa uchunguzi imebainika kuwa baada ya kufunikwa na kifusi walijaa mchanga puani na mdomoni hivyo kukosa hewa na kupoteza maisha.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la zimamoto na uokoaji mkoa wa Kagera Joseph Ngonyani amesema jeshi hilo limepata taarifa ya kuwepo ajali ya watoto kuangukiwa na ukuta katika mtaa wa Anyama kata ya Kibeta Manispaa ya Bukoba.
Amesema baada ya kufika eneo la tukio walikuta wananchi wakiendelea kufanya maokozi na jeshi hilo likaungana nao na kutoa miili ya watoto hao waliokuwa wameangukiwa na ukuta na miili yao kupelekwa hospital ya Rufaa Bukoba, mkoa wa Kagera.
Kamanda Ngonyani amewatak wananchi kuchukua tahadhari zaidi hasa katika kipindi hiki cha mvua kubwa, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha majengo yao yako imara ili kuepusha madhara kama hayo.

Mashuhuda wa tukio hilo wamesema ajali hiyo ilitokea majira ya saa kumi na moja alfajiri, wakati mvua ikiwa bado inaendelea kunyesha, hali iliyosababisha ukuta Perfect Hotel kuporomoka na kuwafunika watoto hao ambao walikuwa nyumba Jirani.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo Anitha Jacob mkazi wa Anyama kata ya Kibeta ameeleza kuwa, ilikuwa asubuhi na mapema ndipo alisikia kelele za majirani kuomba msaada alipofika ndipo aliona kifusi cha ukuta wa hotel ya Pefect ukiwa umeangukia nyumba mbili zilizopo jirani huku wananchi wakiendelea kuondoa kifusi hicho.


Post a Comment