>> Yaibuka mengi Kliniki ya kusikiliza malalamiko ya wananchi
>> Rushwa ,chuki, visasi, huduma mbovu vyatawala
>> Serikali yaombwa kufanya uchunguzi utoaji huduma kituo cha afya Nyangoto
Na Mwandishi Wetu , Nyamongo
HAKI za Afya ni pamoja na haki ya kupata huduma za afya, haki ya kutobaguliwa, haki ya kupata taarifa za afya, haki ya faragha na usiri, haki ya huduma salama na zenye ubora, haki ya kulalamika na kupata haki, haki ya mazingira bora ya afya na haki ya kupata dawa na vifaa muhimu.
Katika Kituo cha afya Nyangoto kilichopo Nyamongo , maafuru hospitali ya Sungusungu katika wilaya ya Tarime , mkoa wa Mara, upatikanaji wa haki za afya imekuwa ni changamoto kubwa inayowakabili wagonjwa wanaofika kupata huduma ya afya .
Baadhi ya watoa huduma wanalalamikiwa kwa kutowathamini na kuwajali wagonjwa huku wengine wakisota kwa muda mrefu mapokezi bila kupewa huduma.
Wagonjwa wanaofika kupata huduma wanalalamika kuombwa gharama kubwa za fedha zisizoeleweka ndipo wahudumiwe haraka . Wasio na fedha wakiisotea huduma kwa saa kadhaa.
Wagonjwa wengine hulazimika kwenda kupata huduma hospitali ya Nyamwaga mwendo wa takribani km 12 kutoka stendi ya Nyamongo baada ya kukosa huduma stahiki kituo cha afya Nyangoto.
Jambo hilo limeendelea kujenga chuki baina ya wananchi na serikali kutokana na malalamiko ya mara kwa mara yanayoelekezwa kwa watoa huduma vikiwemo vitendo vya rushwa vinavyowakosesha haki ya afya lakini hakuna utatuzi .
Tarehe 26, Mei, 2026 mkuu wa wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele alizindua Kamati (Kliniki ) ya kusikiliza na kushughulikia malalamiko vijiji 11vinavyozunguka mgodi wa Barrick North Mara .
Mkuu wa wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele akizungumza na wananchi wa Nyamongo baada ya kuzindua kliniki ya kusikiliza malalamiko, Mei, 26, 2026.
Kliniki hiyo imeundwa na mgodi wa Barrick North Mara , uzinduzi uliofanyika viunga vya stendi ya Nyamongo huku kamati ya kusikiliza malalamiko akiwahimiza wananchi kujitokeza kutoa malalamiko yao ili yaweze kutatuliwa .
Kamati hiyo imehusisha wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa serikali za vijiji, Kata, wataalam kutoka wilaya ya Tarime, mkoa wa Mara na watu wa kutetea haki za Binadamu na utawala bora itakayozunguka vijiji 11 vinavyozunguka mgodi wa North Mara.
Vijiji hivyo ni Kijiji cha Nyangoto, Mjini Kati, Matongo, Nyabichune, Kewanja Kerende, Msege, Nyakunguru , Nyamichere, Genkuru, na Nyamwaga.
Meneja mkuu wa idara ya mahusiano mgodi wa Barrick North Mara, Francis Uhadi anaeleza kwamba kliniki hiyo ni jukwaa la pamoja la kusikiliza na kutatua changamoto ambapo serikali na mgodi hukutana na wananchi kusikiliza na kutatua malalamiko, kutoa ufafanuzi na kutafuta suluhu kwa pamoja na uwazi .
Meneja mkuu wa idara ya mahusiano mgodi wa Barrick North Mara, Francis Uhadi , akizungumza wakati wa unzinduzi wa kamati ya malalamiko Mei, 26, 2026 Nyamongo.
Anaongeza kuwa, lengo la kamati hiyo ni kuhakikisha kama kuna malalamiko yoyote yanayohusu upande wa serikali , mgodi kamati hiyo itaweza kusikiliza na kuyatafutia ufumbuzi.
Wananchi wakatoa malalamiko yao mbele ya kamati ya kusikiliza malalamiko ikiongozwa na aliyekuwa Kaimu Mwenyekiti wa kamati Matha Omahe kutoka ofisi ya mkuu wa wilaya ya Tarime.
Kaimu Mwenyekiti wa kamati ya kusikiliza malalamiko , Matha Omahe ( aliyevaa tisheti nyeupe akiwa na afisa maendeleo ya jamii Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, wakisikiliza malalamiko ya watu wenye ulemavu wakati wa unzinduzi wa kamati ya malalamiko Mei, 26, 2026 Nyamongo.
Gharama , ucheleweshaji huduma
Mkazi wa Kijiji cha mjini kati Juma Shaban Salehe anatoa malalamiko yake kwamba wagonjwa wanachelewa kupata huduma kwani wauguzi hawajali hasa wa mapokezi lakini pia gharama ni kubwa jambo linalosababisha wagonjwa wenye hali mbaya kupoteza maisha.
" Hospitali ya Sungusungu hakuna huduma nzuri , juzi kidogo nimpoteze rafiki yangu aliyechomwa kisu. Tulipofika Sungusungu wakampokea aliyempokea akamtelekeza na kuondoka zake .
" Alimuacha akivuja damu kidogo apoteze uhai . Ndugu zake na mimi tukamtoa pale mapokezi ili tumpeleke hospitali binafsi, ile tunafika nje akaja muuguzi akatuuliza mnaenda wapi ? tukasema ndugu yetu anataka kufa hatuoni huduma yoyote ile.
" Ndugu zangu hospitali ya Sungusungu huduma ni hafifu kibaya zaidi gharama ziko juu wanawake wakifika kujifungua wanaombwa pesa madaktari na wauguzi wanaamini Nyamongo ni sehemu ya madini kila mtu ana pesa wakati kuna wengine wanaganga njaa kama mimi" anasema. Juma.
Anaongeza " Unakuta mwanamke ametoka Kijiji cha mbali kuja kujifungua anaombwa 70,000 hadi 100,000 , unakuta mfukoni ana 20,000 au 30,000 bila kukamilisha pesa wanayoitaka hawezi kuhudumiwa .
" Inabidi uanze kupigia ndugu zako simu ili wakupatie fedha . Ninao ushahidi kuna mwanamke mmoja wakati niko pale Sungusungu yule mama alikuwa analalamika kwamba amemleta mkamwana wake kujifungua kaombwa 100,000.
" Akasema amekosa laki moja ikabidi akaombeombe mtaani akapata pesa akapeleka mkamwana wake akahudumiwa " amesema Juma .
Mkazi wa Kijiji cha Matongo, Samwel Marwa yeye akailalamikia Zahanati ya Matongo na Kegonga " Watoto wetu wanapougua tunapata changamoto kubwa zinazotukabili hatupokelewi kwa wakati kwa muda mwafaka.
" Ukienda kutafuta madaktari ama wauguzi hawapo . Mtoto hatibiwi mpaka awe na cheti cha kuzaliwa na vile vile uwe na kadi ya kliniki .
" Unalazimika uchukue pikipiki sh. 3000-5000 ukimbie mjini kati upewe barua ili uweze kupokelewa mtoto wako ndio atibiwe , je hapo Serikali inatuokoa au inatuangamiza ? . Kero hizo zinasababisha tunaumia na watoto wetu , inasababisha tukimbilie zahanati binafsi " anasema Samwel.
Sheria ya Mtoto
Sheria Na. 21 ya mwaka 2009. Inatoa haki ya afya kwa mtoto, kifungu cha 8(1)(d) kinamtambua mtoto kuwa na haki ya kupata huduma za afya na matibabu, ikiwemo chanjo (medical care including immunisation).
Kifungu cha 8(2) kinakataza mtu kumnyima mtoto huduma za afya, matibabu au mahitaji mengine muhimu kwa maendeleo yake. Inalinda afya, ustawi na haki za watoto, ikiwemo masuala yanayohusiana na afya ya uzazi kwa watoto na vijana.
Majibu ofisi ya DMO
Kaimu Mganga mkuu Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, ambaye pia ni muuguzi msaidizi Kituo cha afya Nyangoto, Silvery Sabin Sabas anazipokea changamoto hizo na kusema kwamba hakuna gharama zozote kwa mjamzito na watoto chini ya miaka 5.
" Nikiri kusema huduma ya mzazi au mjamzito kwa mwongozo wa serikali yetu tukufu ya Mama Samia Suluhu Hassan hatuna gharama zozote ambazo mzazi au mjamzito anatozwa.
" Kama hii changamoto ipo mimi kama Patron nikiri ofisini kwangu bado sijapokea na kama kuna mwananchi katendewa kama Juma Shaban naomba tupeane ushirikiano" anasema Sabin.
Anaongeza " Sikatai kama hilo halipo naomba nilifikishe kwa wenzangu maana siko peke yangu . Watumishi ni sawa na watoto tulionao majumbani kwetu , tunapotoa maelekezo asilimia chache hawawezi kushika hayo maelekezo .
" Huwenda miongoni mwetu sisi watoa huduma tunao watu wa namna hii lakini niwahakikishie tupeni ushirikiano kama sisi viongozi. Na mara nyingi changamoto kama hizi zinapotokea tunaziwasilisha kwa DMO tunapata ufumbuzi lengo na kusudi ni kuhakikisha kila mwananchi afurahie huduma katika Taifa lake.
Sabin anawasisitiza wananchi waliotendewa vitendo vya ukiukwaji wa haki za afya kujitokeza kuwataja ili watu hao wachukuliwe hatua kali ikiwemo kuwaondoa kwenye nafasi zao za utumishi.
" Kama umetendewa kitendo na mtu unamfahamu ofisi zetu ziko wazi , tupeni ushirikiano hao watu tuwaondoe kwasababu ni watu wachache ndio wanatuchafulia sifa za huduma ya afya.
" Hiyo ni kashfa kwa serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hatutakubali, na niwahakikishie hata wewe Juma Salehe hata leo hii ukija ukatoa ushuhuda wenye ushahidi tutakupatia majibu yako na mtumishi aliyefanya hivyo na yuko wapi " anasema.
Akizungumzia mtu aliyechomwa kisu na kukosa huduma anasema " Changamoto hii ya mtu kuchomwa kisu hatujaipokea ofisini kwetu . Kama hakupata matibabu au alicheleweshewa huduma mimi nipo masaa 24 changamoto hii sijaipokea .
" Tuna taratibu tulizozihuisha hivi karibuni , awali tulikuwa na msimamo mmoja . Taratibu zetu zilikuwa akija mtu amejeruhiwa lazima akachukue PF3 hiyo tumeshaiondoa . Ukishafika kituoni upate kwanza huduma , na mara nyingi tuna mawasiliano na Jeshi la Polisi tunawapatia taarifa huku tukiendelea kutoa huduma, PF3 itafuata baadae .
Mtaalam huyo wa afya anaongeza kusema " Bado narudi pale pale tupo wengi tunaotoa huduma , kila mtu ana tabia yake kwahiyo tusaidiane tupatieni majina ya hao watu bahati nzuri tunafahamika tuleteeni taarifa tutashughulika nae .
" Wananchi nanyi mnatuangusha pale mnapokosa kutupa ushirikiano tunaomba mtupe ushirikiano, saa zingine sisi viongozi tunashughulikia mambo lakini ikifika sehemu unasema haaa mimi nilimpa ya soda sh . 5,000 kumbe hata ulitozwa sh. 20,000. Mimi hii inanipunguzia molari ya kushughulika na hawa watu tupeni ushirikiano.
Anasema kwamba kuanzia tarehe 01/06/2026 kutakuwa na mfumo mpa wa malipo kwa kulipa kwa kutumia namba ya malipo, mteja hatoweza kutoa pesa taslimu atalipa kwa njia ya kidigitali.
" Huu mfumo nina uhakika asilimia 80 au 90 malipo ya pesa yako hayatashikwa na mtoa huduma yeyote na huu ndio mwarobaini pekee , pesa zote utafanya malipo kwa control number" anasema .
Amewaomba wananchi kuupokea mfumo huo kwani utasaidia kupunguza changamoto zinazojitokeza za kutoza gharama ambazo kwa mwongozo wa serikali haziruhusu kufanya hivyo.
Hata hivyo baadhi ya wananchi waliokuwa wameketi kwenye viti ikasikika minong'ono wakisema kwamba changamoto kituo cha afya ni nyingi na hawawezi kuzisema hadharani kwakuwa hawajui waliopo kwenye mkutano huo wa malalamiko wana mahusiano gani na watoa huduma kituo cha afya Nyangoto .
" Mwandishi changamoto ni nyingi tatizo unaweza mtaja mtu alafu hatua zisichukuliwe mwisho wa siku wanakuchukia. Ukienda hospitali wanaweza kumdunga mgonjwa wako hata sindano ya sumu kwasababu uliwataja hadharani .
" Rais aliwahi kusema kila mtu ale kwa urefu wa kamba yake kwahiyo nao wanakula kwa urefu wa kamba zao , mimi ni nani niwazuie ? hata ukiwachongea hakuna mabadiliko yoyote , wanawahamisha lakini matatizo yanabaki vile vile hayaishi" anasema mwananchi mmoja.
Rushwa yakosesha huduma
Kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
Na. 11 ya Mwaka 2007 Sura ya 329 (Toleo Lililofanyiwa Marejeo la 2022 – R.E. 2022) ni kosa kuomba, kutoa au kupokea Rushwa.
Kifungu cha 15 cha sheria hiyo ya TAKUKURU kinakataza kuomba rushwa
, Kupokea rushwa, kutoa rushwa,
Kukubali faida yoyote ili kushawishi utekelezaji wa kazi.
Kifungu cha 16 kinazuia matumizi mabaya ya mamlaka. Kifungu cha 17 kinazuia wizi au matumizi mabaya ya mali ya umma ikiwemo kuiba dawa hospitalini, kuuza vifaa vya hospitali
Kutumia mali ya hospitali kwa maslahi binafsi.
Kifungu cha 31 kinazungumzia matumizi mabaya ya nafasi ya kazi . Sheria hiyo imetoa adhabu mtu atakayepatikana na hatia anaweza kuadhibiwa kwa mujibu wa kifungu cha 15(2), kifungo cha miaka 3 hadi 5 jela, au faini isiyopungua shilingi 500,000 na isiyozidi shilingi 1,000,000, au adhabu zote mbili kwa pamoja, pamoja na uwezekano wa kutaifishwa au kurejeshwa kwa mali iliyopatikana kupitia rushwa.
Licha ya kuwepo kwa sheria hiyo na adhabu bado vitendo vya rushwa havikomi vinaendelea katika Zahanati, vituo vya afya na hospitali mbalimbali nchini , jambo linalojenga chuki baina ya wananchi, watoa huduma na serikali kwa ujumla .
Mwandishi wa DIMA Online amezugumza na wananchi mmoja kwa mmoja kwa nyakati tofauti kufahamu hali ya utoaji wa huduma ya afya katika Kituo cha afya Nyangoto . Wananchi wanazungumza kwa sharti la kutotajwa majina yao kwa usalama wa afya zao.
" Unaweza ukawa kwenye mazingira yasiyo ya nyumbani ukauguliwa mtoto ukifika hospitali hauna kadi ya kliniki wanakulipisha hela sh. 5,000 kwa ajili ya kuonana na daktari.
" Na kwa mjamzito ni hivyo hivyo kama hauna kadi ya kliniki unalipa sh. 5000 ndio unapata huduma. Wanasema huduma kwa mjamzito na mtoto ni bure huo ni uongo wajawazito wanaojifungua kawaida wanalipa 50,000 - 80, 000 wa upasuaji hadi 300,000 " anasema mwananchi mmoja .
Mkazi mwingine anasema " Bila kutoa Rushwa hupati huduma ukifika watakuangalia na kukuacha hapo. Kwakuwa una shida inabidi uwape tu hela sasa utafanyeke maana ukiwachongea wanakujengea chuki wanakuwa na kisasi na wewe.
" Wana kamsemo wanasema kwamba " Hapa ni mtakuja " wanajua utakuja na siku ukirudi wanakutelekeza hawakupi huduma kwasababu hukuwapa pesa au uliwachongea .
Bhoke Chacha mkazi wa Kijiji cha Nyangoto anasema waliofanyiwa upasuaji nje ya kituo hicho wakienda kutolewa nyuzi wanawanyanyapaa.
" Ukifanyiwa upasuaji hospitali nyingine siku ukienda kutoa nyuzi wanakunyanyapaa mara wakwambie si uende huko ulikofanyiwa upasuaji ,akikubali kukupa huduma anakupatia kwa shingo upande yaani anakuvuta kwa uchungu . Yaani ili upate huduma nzuri mpaka utoe pesa .
" Hata malipo yakifanyika kwa njia ya mtandao bado rushwa haitaisha, utalipa pesa kupitia mfumo lakini kule wodini hautopewa huduma mpaka umshikishe pesa. Kuna wauguzi wawili wanawake yaani wanapenda Rushwa hatari anaweza kumwangalia mgonjwa wako anakata roho kisa tu hujampatia pesa" .
Marwa Mwita mkazi wa Kijiji cha Nyangoto anasema huduma ya wazee nayo ni changamoto " Mzee anafika mapokezi anaambiwa apange foleni na hali yake sio nzuri, matibabu yenyewe mpaka alipie fedha kwakweli wazee tunateseka sana, serikali itusaidie sisi wazee .
Mkazi mwingine anasema " Dawa za watoto hazipo kituo cha afya , wauguzi karibu wote wana maduka yao binafsi ya dawa wanakwambia dawa hakuna ila anakuelekeza ukanunue kwenye duka lake binafsi .
" Wakati mwingine ukienda hospitali kupata huduma muuguzi anakwambia hapa utachelewa kupata huduma anakuelekeza uende kwenye duka lake la dawa unaenda pale unapata dawa kama ni vipimo unapimwa kwenye maabara zao binafsi na kukupa tiba kama ni sindano atakuchoma ukiwa kwenye duka lake la dawa au maabara yake ya vipimo. " anasema.
Wauguzi hawakai kituoni
Mkazi wa mtaa wa mjini kati anasema " Pale Sungusungu kuna wakati ukienda hupati huduma kwasababu baadhi ya wauguzi wanakuwa hawapo kituoni wanakuwa kwenye maduka yao na maabara zao binafsi wakitoa huduma.
" Kuna chumba namba 1 kile chumba hakinaga mganga ni chumba ambacho wauguzi wamekigeuza chumba cha kupigiamo stori yaani hatumjui mganga mkuu ni nani au mganga mfawidhi kwenye hiki kituo " anasema mwananchi mmoja.
Mwingine anaongeza " Watoa huduma wanafanya kazi kwa kujisikia kwa muda wanaotaka wao, akienda kunywa chai au kula chakula atamaliza huko hata masaa mawili ndio unamuona .
" Unaenda hakuna nesi wa kukuhudumia ,ukiwafuata wanakuja kwa kuchelewa . Ukimwambia ukweli kuwa unavyofanya sio vizuri anakujengea chuki na visasi kana kwamba umemkosea .
" Wanataka hata kama wamefanya vibaya unyamaze, watoto wanakufa hasa wakati wa kuzaliwa hadi tunaogopa kwenda kujifungulia Sungusungu kwasababu hata kumpata nesi aje amwekee mtoto dawa ni shida wanakuja kwa kujisikia ukiwapa pesa huduma ni fasta " anasema .
Anaongeza " Wazazi wanaogopa kusema ukweli kwasababu wanajua bado utarudi tu kwenye hiyo hospitali utawakuta inabidi ukae nayo moyoni japo yanaumiza sana.
" Tena wale wa shfti ya usiku wodi ya wazazi na watoto ni shida wana lugha mbaya matusi kama yote wakati unajifungua wanakupiga kweli tena makofi " anasema.
Sheria ya afya
Sheria ya Afya ya Tanzania, Na. 21 ya Mwaka 2017 (Health Act, 2017), inasisitiza haki ya kupata huduma za afya. Kifungu cha 22(1) Mgonjwa ana haki ya kupata huduma za afya zinazofaa bila ubaguzi kwa misingi ya jinsia, dini, kabila, hali ya kijamii au sababu nyingine zisizokubalika kisheria
Mapokezi shida
Mkazi wa Kijiji cha Nyangoto anasema " Yaan pale mapokezi panachosha sana utakaa sana mpaka utakoma hata kama umezidiwa wao hawajali . Ukiwa na hela unachomolewa kwenye foleni fasta unapata huduma msio na pesa utasota sana kuja upate huduma cha moto umekipata.
" Ili upate huduma ya haraka pale mapokezi mpaka uwashikishe fedha au uwe na mtu anayefahamiana nao akusaidie uhudumiwe . Ukiona kero na una pesa unawapa ili upate huduma au unaondoka kwenda kupata huduma hospitali binafsi. Kama una pesa unaona bora ukapate huduma hospitali binafsi zenye gharama kubwa pesa ambayo ungefanyia mambo mengine ".
Hata hivyo, pamoja na malalamiko kwa watoa huduma kituo cha afya Nyangoto kulalamikia huduma mbovu , wapo watoa huduma wanaofanya kazi kwa kuzingatia maadili ya kazi na huduma bora kwa wateja na wagonjwa .
Wananchi wanasema wapo watumishi Kituo cha afya Nyangoto wanatoa huduma nzuri kwa wagonjwa hawana manyanyaso. Watumishi hao waliotajwa kwa jina moja ni Sabini , Habson na Revinata kwamba wao mgonjwa akifika anashughulikiwa ipasavyo lakini wasipokuwepo ni tabu na huzuni kwa wagonjwa.
Wananchi wanaiomba serikali kupeleka wachunguzi wa siri kufuatilia hali ya huduma ya afya inavyotolewa na watoa huduma wa kituo hicho cha afya Nyangoto na Zahanati ya Matongo kwa kile kilichoelezwa kuwa watoa huduma wanakiuka haki za afya.
Haki ya afya inamhakikishia mtu kupata huduma za afya zinazopatikana, zinazofikika, zenye ubora na zinazotolewa bila ubaguzi. Nchini Tanzania, haki ya afya inapatikana kupitia Katiba, sheria mbalimbali, sera za afya, miongozo ya huduma za afya na mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania imeiridhia.
Katiba ya Jamhuri
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ibara ya 14 inasisitiza kwamba kila mtu ana haki ya kuishi na kupata hifadhi ya maisha yake kwa mujibu wa sheria .
Sera ya Afya
Kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya afya ya mwaka 2007 inalenga kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma za afya zinazofikika , zenye ubora na zinazotolewa kwa usawa bila ubaguzi wa aina yoyote.
Mwongozo
Mwongozo wa haki na wajibu wa mteja /mgonjwa ( Client Service Character) wa mwaka 2013 , utaoa haki kwa mgonjwa kupata huduma za afya zinazokidhi viwango vinavyokubalika vya ubora.
Pia unatoa haki kwa wazee, wajawazito, watoto chini ya miaka mitano na watu wenye ulemavu wanapaswa kupewa kipaumbele katika kupata huduma.
Mgonjwa ana haki ya kupewa taarifa kuhusu huduma zinazopatikana, gharama za huduma na malipo anayopaswa kufanya.
Mikataba ya Kimataifa
Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiuchumi, Kijamii na Kitamaduni (ICESCR) wa mwaka 1966 – Ibara ya 12, unatambua haki ya kila mtu kufurahia kiwango cha juu kabisa cha afya ya mwili na akili kinachowezekana.
Huu ndiyo mkataba mkuu wa kimataifa unaotambua haki ya afya kama haki ya binadamu.
Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu la mwaka 1948 (UDHR) Ibara ya 25(1)linasisitiza kuwa kila mtu ana haki ya kiwango cha maisha kinachotosha kwa afya na ustawi wake, ikiwemo huduma za matibabu.
Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu wa mwaka 1981, Ibara ya 16 (1), unaeleza kuwa kila mtu ana haki ya kufurahia hali bora ya afya ya mwili na akili . Pia Ibara ya16 (2) inasisitiza Nchi wanachama zinapaswa kuchukua hatua za kulinda afya za wananchi wao.
Post a Comment