HEADER AD

HEADER AD

MKE WA MTU SUMU

MKE wa mtu ni sumu, ni sumu inayoua,

Nakuasa mheshimu, usijifanye wajua,

Usije kujilaumu, na kisha ukajutia,

Mke wa mtu ni sumu usiweke mazoea.


Kaolewa kwa mahari, na ndoa ikafanyika,

Wala haikuwa siri, watu walikusanyika,

Nakupatia hadhari, yasije yakakufika,

Mke wa mtu ni sumu usiweke mazoea.


Wala usimrubuni, kwa khanga na visabuni,

Siku nikikubaini, utajuta maishani,

Sitaki uje nyumbani, mimi ndoa nathamini,

Mke wa mtu ni sumu usiweke mazoea.


Mme ninahudumia, uwezo ninao pia,

Nyama namnunulia, huduma nampatia,

Kwangu ameshatulia, usiingilie ndoa,

Mke wa mtu ni sumu usiweke mazoea.


Mahari nimelipia, nikafungiwa na ndoa,

Gharama niliingia, mpaka nikamuoa,

Siyataki mazoea, nadhani umesikia,

Mke wa mtu ni sumu usiweke mazoea.


Siutaki ushirika, na mke wangu jamani,

Nakukataza hakika, uwe nalo akilini,

Usije ukaumbuka, ukachekwa kijiweni,

Mke wa mtu ni sumu usiweke mazoea.

No comments