HEADER AD

HEADER AD

GATI MOJA LA MAJI LINAHUDUMIA WATU 2,000

Mwenyekiti wa mtaa wa Kigote Maungo Malima akifungua Gati ambao maji yamekuwa yakitoka kwa kusuasua

 

  • Ni lile lililopo mtaa wa Kigote na Lugezi
  • Wananchi wanalazimika kuchota maji usiku 

Na Dinna Maningo, Mwanza

UHABA wa maji bado ni tatizo linalosababisha kusuasua kwa utekelezaji wa Sera ya maji ya Taifa kwakuwa baadhi ya maeneo hapa nchini wananchi hawapati huduma ya maji  safi na salama,hivyo kulazimika kutembea umbali mrefu huku na kule kuyasaka maji,maeneo yaliyo na maji nayo bado hayatoshelezi kukidhi mahitaji ya watumiaji.

Pia vituo vinavyotoa maji ni vichache havikidhi mahitaji ya wananchi hivyo kusababisha mrundikano wa watu kwenye kituo kimoja kinachotoa maji (GATI) yanayotoka kwa muda mfupi,kaya zenye maji majumbani nazo zinapata kwa kusuasua . 

SERA ya Maji ya Taifa ya mwaka 2002 ambayo imetokana na mapitio ya Sera ya mwaka 1991 inaelekeza vituo vya maji viwe umbali usiozidi mita 400 na kila kituo kihudumie watu 250.

Mtaa wa Kigote na Lugezi Kata ya Bugogwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza,inakabiliwa na uhaba wa maji kutokana na kuwepo kituo kimoja kinachotoa maji katika mitaa hiyo.

Licha ya kuwepo Gati moja la maji  mtaa wa Kigote limekuwa likitoa maji kuanzia muda wa saa moja usiku hadi saa 12 asubuhi , hali inayowalazimu wananchi kufuata maji  yasio safi na salama mwendo wa Takribani km moja katika Ziwa Victoria.

Maungo Malima ni Mwenyekiti wa mtaa wa Kigote anasema kuwa mtaa una kaya 800 una Gati moja la maji  ambalo halitoshelezi mahitaji ya wananchi na ahadi ya kuongezewa Gati nyingine imekuwa ikitolewa lakini hakuna utekelezaji .

 "Mtaa wa Kigote ni mtaa mkubwa una Kaya 800 lakini una Gati moja la maji linalohudumia watu zaidi ya 2,000 linatoa maji kuanzia saa moja usiku hadi saa 12 asubuhi yanakatika,asubuhi hakuna maji mchana hadi jioni hakuna maji, watu waliovutiwa maji majumbani hawafiki 100 nao maji ni hivyohivyo yanatoka kwa shida.

"Tulifuatilia tukabadilishiwa mtandao wa maji lakini tatizo la upatikanaji wa maji bado ni lile lile,wataalamu wanasema huku eneo la chini watu wengi walivutiwa maji,uhitaji unakua mkubwa na kusababisha maeneo mengine yakose maji kwahiyo inapofika muda wa usiku uhitaji wa maji unapungua ndio yanatoka kwenye Gati,wataalamu wa maji walituahidi kutuletea Magati sita  ya maji lakini hawajaleta na kadri siku zinavyokwenda wananchi wanazidi kuongezeka.

Maungo anasema kuwa zipo kaya zinazohitaji kuvutiwa maji "Diwani na Mbunge walishayazungumzia kwenye vikao lakini wataalam hawatekelezi wangekuwa wanatekeleza maji yangekuwepo ya kutosha, wataalamu wa halmshauri wanapuuza maelekezo ya viongozi tunaomba Serikali ituongezee Gati ili wananchi wasihangaike kutafuta maji na yatoke kwa wakati bila kusuasua" anasema Maungo.

Lucy James anasema kuwa uhaba wa maji unawatesa wanawake"maji ni ya shida yakikatika kuyapata ni baada ya siku moja au zaidi na yakitoka ni usiku,una watoto wanatakiwa kuogo bado ufue nguo,inabidi tuyafuate ziwani ambayo sio safi na salama.

Eneo kulikokuwa kumewekwa Gati na kisha kuhamishwa baada ya kutotoa maji


Uhaba wa maji upo pia mtaa wa Lugezi katika kata hiyo, licha ya kwamba  tenki la maji limejengwa kwenye mtaa huo lakini wananchi waliovutiwa maji majumbani ni wachache huku kukiwa na Gati moja la maji linalohudumia watu zaidi ya elfu 2,000 na maji hutoka kwa kusuasua.

Mwenyekiti wa mtaa wa Lugezi Alex Mkama anasema "Mtaa una Kaya 700  kati ya hizo zilizovutiwa maji majumbani hazifiki hata kaya kumi japo tenki lipo hapahapa mtaani lakini maji ni ya shida hata hayo yaliyopo yanatoka kwa kusuasua mara yapo mara hayapo,kutoka hapa mtaani hadi kufika ziwani unatumia dakika sita lakini watu hawana maji ya bomba ambayo ndio safi na salama kwakuwa yanakuwa tayali yametibiwa na dawa.

"Mtaa mzima unatumia Gati moja linalohudumia watu zaidi ya elfu 2,000 , wananchi wanataka maji ya bomba nilishafuatilia sana mamlaka ya maji ukiuliza unaambiwa tupo kwenye mchakato mara unaambiwa tatizo ni vifaa,mara kuna kifaa kiliungua eti kimeagizwa Afrika kusini.

Anaongeza " Mara unaambiwa kuwa maji yakikatika ni kwasababu umeme hauna nguvu ya kutosha kusukuma maji yaani unaenda kutafuta ufumbuzi unaowafuata wakusaidie nao wanakueleza changamoto sasa sijui nani wakumsaidia mwingine,watuwekee mtandao wa maji watu wavute maji tunahitaji maji safi na salama yatakayolinda afya zetu"anasema Alex. 

Alphonce Atanasi anayeishi mtaa huo wa Lugezi  anasema kuwa kwenye maeneo yenye vituo vya kutoa maji bado ni haba hayatoshelezi mahitaji "Leo maji yapo kesho hakuna au unakaa hata siku tatu hakuna maji na una bomba la maji nyumbani, Gati ni moja watu ni wengi halitoshi waongeze mengine,maji ni uhai ukikosa maji unajiongezea magonjwa.

 Ester Elias anaongeza " Tatizo ni wataalamu hawatimizi majukumu yao ipasavyo ,anapokuja kiongozi mkubwa maji yanatoka akiondoka maji yanakosa sasa unajiuliza inakuwaje tukose maji ? lakini siku akija kiongozi maji hayoo yanatoka! ile kauli mbiu ya kumtua mama ndoo kichwani bado haijatusaidia sisi wanawake wa Lugezi ni wimbo tu,akina mama wanahangaika na maji wanachelewa kupikia watoto wanachelewa biashara zao kisa maji alafu mnatuambia mmemtua mama ndoo kichwani wakati kila kukicha tunatembea kutafuta maji tumejitwisha weee maji vichwani hadi vinauma "anasema Ester.

Diwani wa kata ya Bugogwa William Mashamba anasema kuwa tenki linalosambaza maji mitaani limezidiwa ni dogo halitoshelezi mahitaji na kwamba Serikali inatarajia kujenga Tenki lingine ili kuwezesha uwezo wa maji ambalo litasaidia  kupunguza changamoto ya mahitaji ya maji.

Kaimu Meneja Mahusiano wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) Oscar Twakazi anasema kuwa mamlaka ya maji inatambua wajibu wa kutekeleza sera ya maji ambayo inatekelezwa kwa kuzingatia Sheria ya maji na Sheria nyingine na kwamba Mamlaka inaendelea kuweka mipango ya kuboresha huduma katika maeneo hayo na mengine hatua kwa hatua kulingana na uwezo wa fedha utakaokuwepo  kwakushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya maji.

"Maeneo ya pembezoni ya Mwanza yalikuwa yanasimamiwa na Wizara ya Maji kupitia Idara za maji Mikoa lakini kwa miaka michache iliyopita ikaundwa RUWASA ili kutoa huduma ya maji maeneo ya Vijijini kabla ya RUWASA miradi yote ilikuwa inasimamiwa na halmashauri za maeneo husika walikuwa wanadizaini wenyewe wanatumiwa fedha kujenga kulingana na wanavyoona mazingira yao yamekaaje " anasema Oscar.

Anaongeza kusema " Miradi yote unayoizungumzia kwa maana ya wilaya ya Ilemela ilikuwa inajengwa na halmashauri na ilikuwa imesuasua sana baadae ilikabidhiwa RUWASA na sasa inasimamiwa na MWAUWASA.Tulipokabidhiwa tuliikamilisha kwa jinsi ilivyokuwa imedizainiwa na kwa fedha zilizokuwepo.

"Mfano kama mradi halmshauri ilitumia Milioni 500 zikabaki Milioni 250 tuliendelea kukamilisha kukamilisha kwa fedha hizo hizo, huwezi kubadili au kufanya chochote tofauti na ulivyopewa kwahiyo tunachangamoto kubwa ya maeneo hayo ile miradi ni ya muda mrefu  na ilidizainiwa kabla ya 2010 na 2013 ikajengwa " anasema.

Oscar anasema kuwa Serikali ina nia njema na wananchi wake,imekuwa ikijitahidi kutatua changamoto za maji ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama,bado inaendelea kutekeleza miradi ya maji ili kuwasogezea wananchi huduma  ya maji safi na salama kama Sera ya Taifa inavyosisitiza.

"Kuna fedha imetengwa ambayo itaboresha utoaji wa huduma katika maeneo hayo, Bugogwa maji hayatoshelezi na sio huko tu bado na maeneo mengine maji ni pungufu. Mradi wa Butimba ukikamilika utasaidi kupunguza changamoto ya maji,ongezeko la idadi ya watu na shughuli za maendeleo yanayohitaji maji imechangia kuwepo mgao wa maji jijni Mwanza.

"Makadirio ya mwaka jana mahitaji ya maji Jiji la Mwanza yalikuwa ni lita Milioni 160 lakini chanzo cha Capripoint kinazalisha lita Milioni 90,upungufu unaosababisha mgao wa maji hivyo mradi wa Butimba utakuwa suluhisho la changamoto ya maji katika maeneo mbalimbali na utaongeza uzalishaji wa lita takribani Milioni 140"anasema Oscar.

Hotuba ya Waziri wa Maji Jumaa Aweso (MB) aliyoiwasilisha Bungeni  ya Makadilio ya Mapato na Matumizi ya fedha za Wizara ya Maji kwa mwaka 2022/2023, imeainisha vipaumbele na mpango wa utekelezaji kwa mwaka huo wa fedha.

Bajeti hiyo inaonesha miradi 175 ya maji safi na usafi wa mazingira mijini itatekelezwa kwa mwaka 2022/2023 ambapo Mwanza Jiji utafanyika upanuzi wa mtandao wa maji safi katika maeneo ya pembezoni mwa mji wa Mwanza, Kayenze, Igombe,Shibula, Lwanhima na Sangabuye ambapo fedha za Serikalini kupitia mfuko wa maji wa Taifa (NWF) kiasi cha Tsh. 350,000,000 zitatumika.

Ilani ya uchaguzi ya Chama Tawala cha Mapinduzi (CCM) ya 2020 -2025 inaielekeza Serikali kutekeleza yale yaliyomo kwenye Ilani ikiwemo Ibara ya 9 inayosema kuwa Chama kitaielekeza Serikali kuimarisha upatikanaji wa huduma bora ya Afya, Elimu, Maji, Umeme na makazi Vijijini na Mjini.

Pia kuongeza kasi ya usambazaji maji safi na salama ili kutosheleza mahitaji kwa zaidi ya asilimia 85 Vijijini  na zaidi ya asilimia 95 kwa mjini kwa upande wa Tanzania Bara ifikapo mwaka 2025 imeeleza Ilani ya CCM.

Ilani hiyo Ibara ya 10 inasema kuwa CCM itahakikisha Serikalini yake inatekeleza mambo yote yaliyoahidiwa katika ilani.



No comments