HEADER AD

HEADER AD

WAOMBA ELIMU ITOLEWE KUEPUSHA WANANCHI KUJENGA NDANI YA HIFADHI YA BARABARA

Na Dinna Maningo, Tarime

UKOSEFU wa Elimu ya Hifadhi ya Barabara ni changamoto inayowakumba wananchi walio wengi, huku wengine wakiwa hawafamu ni mita ngapi zinazotakiwa kuachwa kwa ajili ya matumizi ya barabara.
 
Imeelezwa kuwa wananchi kutopewa elimu ya hifadhi ya barabara ni chanzo cha baadhi yao kufanya shughuli na  kujenga nyumba kwenye hifadhi ya barabara kwakuwa hawafahamu sheria ya barabara na taratibu za kufuatwa.

Wananchi wilayani Tarime mkoani Mara wameiomba Serikali kutoa elimu ya hifadhi ya barabara kama njia ya kuwaepusha kununua viwanja au kujenga nyumba kwenye hifadhi ya barabara na kusababisha kubomolewa nyumba zao.


Mwandishi wa Habari wa DIMA Online amefanya mazungumzo kwa nyakati tofauti na baadhi ya wananchi mjini Tarime kufahamu kama wana elimu ya Hifadhi ya Barabara nao walikuwa na haya ya kusema;

Ghati Chacha Mkazi wa Rebu shuleni amesema" Mimi sijui hifadhi ya barabara ni nini nafahamu tu kuna hifadhi ya Wanyama ya Serengeti, sifahamu kama huwa kuna hifadhi ya barabara zaidi tu ya kuona barabara tunazozitumia tunapotembea kwahiyo mimi sijui hifadhi ya barabara". Amesema Ghati.

Zakayo Chacha Wangwe mkazi wa mjini Tarime amesema elimu ya hifadhi ya barabara haijawafikia wananchi wote jambo linalosababisha waendelee kujenga na kufanya shughuli mbalimbali ndani ya hifadhi ya barabara.

    Zakayo Wangwe mkazi wa mjini Tarime

" Elimu itolewe iwe endelevu kuanzia viongozi wa vitongoji, baadhi yao hawana elimu ya upangaji wa matumizi bora ya ardhi, wala mipaka ya hifadhi ya barabara, wengine wanachaguliwa hasa hawa wa Serikali za Mitaa na Vijiji wanafanya kazi bila kuwa na elimu ya matumizi bora ya ardhi kama hifadhi za barabara, mito, vyanzo vya maji.

Ametaja sababu nyingine ya watu kujenga kwenye hifadhi ya barabara ni tamaa ya fedha kwa baadhi ya viongozi ambao uandikisha viwanja wakijua vipo kwenye hifadhi ya barabara.

"Unakuta kiongozi anafahamu kabisa ili eneo ni la hifadhi lakini anakubali kumwandikishia muuzaji na mnunuzi kwasababu ya tamaa zao binafsi wanauza maeneo ya hifadhi ya barabara bila kufuata utaratibu.

"Elimu ya hifadhi ya barabara itolewe pia kwa wananchi, TARURA na TANROAD watoe elimu maana watu hawajui kuwa unatakiwa kuacha mita ngapi kutoka barabarani.

"Mfano sisi tulibomolewa nyumba na TANROAD tulikuwa hatujui kama kuna sheria ya mwaka 1932 ya hiyo hifadhi ya barabara ya Tarime- Nyamwaga kuwa unatakiwa kuacha mita 22.5 kutoka katikati ya barabara kila upande.

"Hatukuwa na hiyo elimu baada ya zoezi la ubomoaji kufika ndiyo tukaambiwa. Tunaomba wahusika wawe wanatoa elimu mapema, wangekuwa wanatoa elimu mapema watu wasingekuwa wanajenga kwenye hifadhi ya barabara." Amesema Zakayo.

Zakayo ameomba kuwepo na Mawasiliano kati ya Serikali za Mitaa, Vijiji, Idara za ardhi katika Halmashauri, TARURA na TANROAD pindi kunapofanyika zoezi la upimaji wa ardhi hususani viwanja vya wananchi.


"Kuwepo na mawasiliano ya karibu, mfano unakuta Idara ya ardhi ya Halmashauri wanakwenda kupima viwanja watu wanapewa hati lakini unakuta hayo maeneo ni hifadhi ya barabara.

" Mfano mzuri ni vile viwanja kama kwa Nyaronyo na Rebu watu wana Hati zao lakini wakaambiwa ni hifadhi ya barabara hii ni kwasababu hapakuwa na mawasiliano yakutosha au tamaa za fedha kwa wahusika wa ardhi.

"Wanapimia watu ardhi na kuwapa hati wakijua ni maeneo ya hifadhi ya barabara alafu baadae watu wanabomolewa. wakati wa upimaji wa viwanja watu wa ardhi na wakala wa barabara wawepo ili wananchi wasiingie kwenye tabu ya kubomolewa nyumba ilihali wana hatimiliki walizopewa baada ya kupimiwa viwanja" amesema Zakayo.

Mariam Tura mwenye ulemavu wa viungo mkazi wa Mtaa wa Mkuyuni amesema watu hujenga karibu na barabara kwakuwa hawana elimu ya hifadhi ya barabara na barabara nyingi hazina alama za mipaka ya barabara.


"Barabara nyingi hazina alama ambazo zingekuwa rahisi mwananchi kutambua mipaka ya barabara, unakuta watu wameuziwa viwanja kwa kutojua kama vipo hifadhi ya barabara siku barabara ikipita anabomolewa nyumba.

"Sehemu za barabara ziwekewe vielelezo, kama vigingi kwamba hapa ni eneo la barabara, au eneo la wazi, eneo la mto ili mtu anapoenda kununua uwanja au kujenga awe anajua hili ni eneo la hifadhi." Amesema Mariam.

Ameongeza kusema" Na mimi nilitaka kushikishwa eneo ambalo kesi ilikuwa mahakamani, Mwenyekiti wangu wa mtaa ndiye alinisaidia akanijulisha kuwa ni eneo lenye mgogoro na kesi ipo mahakamani nikaacha kulinunua. Hivi karibuni eneo hilo limebomolewa, ningekuwa nimelinunua nyumba yangu ingebomolewa". Amesema Mariam.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Kogete Halmashauri ya Mji Tarime Alphaxad Maginga Keroma amesema wananchi wengi hawafahamu kuhusu hifadhi ya barabara.

"Wananchi wengi hawafahamu kabisa, elimu haipo ni wachache wenye hiyo elimu. Viongozi wao wanafahamu mfano mtaa wangu wa Kogete tuna mambo ya upimaji wa viwanja kwahiyo huwa tunakaa na watu wa upimaji.

"Wanatuambia hii barabara labda tutaipa mita 10, labda ni ndogo tuipe mita 8, kwahiyo na sisi unakuta tunafahamu ,inapofika hatua ya urasimishaji makazi ya watu unakuta tupo nao na tunakuwa na ramani pale ofisini.

"Mtu anapotaka kununua uwanja tunamuuliza unataka kununua uwanja kwa nani au jirani na nani atasema kwa fulani, tunaenda kwenye ramani tunaangalia huyo fulani labda ana viwanja vitatu je kati ya hivyo ni kipi anachouza anatueleza" amesema. 

Mwenyekiti huyo amesema "Tatizo ni kwamba mtu anapokuwa amenunua uwanja hashirikishi viongozi wakati wa kujenga, kiongozi unakuja kujua nyumba tayari ipo kwenye lenta au usawa wa madirisha imejengwa kwenye hifadhi ya barabara na alijenga bila kibali cha ujenzi" amesema.

Maginga ameongeza " Ukimpa elimu anakwambia unakwamisha maendeleo yake ni changamoto tunayokutana nayo, lakini kwenye maeno yote ambayo sisi tumepima tumehakikisha kila kiwanja kinafikiwa na njia sema ni kwa sababu hazijafunguliwa zikaonekana rasmi.

" Mimi nikimkuta mtu anajenga eneo fulani lazima nimuekeleze kuacha kichochoro hizo ni njia za Serikali maana nyumba inaweza kuungua hivyo gari lazima lipite kwenye hivyo vichochoro kwa ajili ya kuokoa .

" Kwahiyo tulishapima sasa kwakuwa ni wagumu kuelewa ndio hao ikifika wakati wa kujenga barabara nyumba zao zinabomolewa alafu wanaanza kulalamika kuwa Serikali imewabomolea nyumba".Amesema Mwenyekiti huyo.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Kokehogoma Musa Nehemia amesema tangu kufanyika zoezi la upimaji shirikishi wa ardhi limesaidia kupata elimu ya hifadhi ya barabara ambayo imewawezesha viongozi wa Serikali ya mtaa kuitoa kwa wananchi kupitia mikutano na pindi mtu anaponunua uwanja.

    Mwenyekiti wa Mtaa wa Kokehogoma Musa Nehemia

"Upimaji shirikishi umetupa elimu kamati ya ardhi ilielimishwa ikiwemo ujenzi holela, tunatoa elimu ila baadhi ya wananchi akishanunua uwanja anaamini yeye ndio mwenye maamuzi ya matumizi anajenga hadi barabarani.

" Kiwanja kikishawekewa kigingi unatakiwa kuacha mita 1.5 kurudi nyuma ndio ujenge nyumba hili hata barabara ikipita uwe na sehemu ya kuingia nyumbani kwako au kwa ajili ya kichochoro, mita 8 za barabara zikishapimwa na wewe unatakiwa kuacha mita 1.5 kuingia kwako" amesema Musa.

Amewaomba wananchi kufuata maelekezo ya viongozi wao ili kuepuka kero na usumbufu pindi inapobainika viwanja vyao na nyumba kuwa ndani ya hifadhi ya barabara.

No comments