HEADER AD

HEADER AD

TARURA : TARATIBU HIZI ZIFUATWE KABLA YA KUJENGA NYUMBA KARIBU NA BARABARA


Na Dinna Maningo, Tarime

MENEJA Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) wilaya ya Tarime mkoani Mara, Mhandisi Charles Marwa  amewasisitiza wananchi wanaonunua viwanja kuomba ushauri pindi wanapotaka kujenga nyumba ili kuepuka kujenga katika hifadhi ya barabara.

Akizungumza na DIMA Online Mhandisi Charles amesema baadhi ya wananchi ununua maeneo kwenye hifadhi za barabara na kujenga nyumba kitendo ambacho ni kinyume cha sheria ya barabara na hivyo Serikali kulazimika kubomoa.

Meneja Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) wilaya ya Tarime mkoani Mara, Mhandisi Charles Marwa

"Kama uwanja wako upo karibu na hifadhi ya barabara tunashauri usijenge kwanza fika TARURA uombe ushauri sisi tutafika hadi kwenye uwanja wako tutakupimia na kukuelekeza jenga kuanzia hapa.

"Maeneo ya hifadhi ya barabara ni muhimu tunapotaka kupeleka huduma za kijamii kama kupanua barabara, umeme, maji, minara humo ndio tunapitisha sasa wakijenga nyumba hizo huduma zitapitishwa wapi? lazima utabomolewa"amesema Mhandisi Charles.

Meneja huyo amesema  mtu mwenye uwanja karibu na barabara  kabla ya kujenga nyumba anatakiwa kuzingatia haya ; 

"Hifadhi ya Barabara unatakiwa kuacha mita 40 yaani mita 20 kutoka katikati ya barabara upande wa kushoto na mita 20 kutoka katikati ya barabara upande wa kulia kwa barabara za wilaya.

"Barabara za jamii mita 30 ambapo kila upande kutoka katikati ya barabara ni mita 15, kwa barabara za TANROAD ni mita 60 kutoka katikati ya barabara ni mita 30 kwa upande wa kulia na kushoto." amesema 

Amesema ni muhimu mwananchi kupata maelekezo kabla ya kujenga " Hata ukijenga ukakaa miaka mingi tutakubomolea bila kukupa fidia kwasababu tunaamini  Serikali inaanzia pale alipo.


" Kuna Balozi, Mwenyekiti wa Kitongoji, Kijiji na Mtaa, kuna Mtendaji wa Kijiji, Mitaa na Kata na Diwani, wote hawa  wanajua taratibu na sheria maana huwa wanaelimishwa, ni jukumu lao kuwaelimisha wananchi na kuwaelekeza. 

"Kwahiyo tunategemea anapotaka kujenga atafute ushauri aulize nataka kujenga hapa wamwambie nenda Halmashauri wataalam waje wakuongoze, akija Halmashauri ataelekezwa utaratibu hapo ndio atakua amepata usahihi kuwa anatakiwa afanye nini" amesema.

Meneja huyo ameongeza " Halmashauri itamuelekeza Sheria ya Ardhi na Mipango miji lakini kwenye barabara watamshauri nenda TARURA kama kiwanja kimepakana na barabara.

" Akija kwetu sisi tutakwenda hiyo ni huduma inatolewa bure hachangii chochote tutampimia. Kutojua Sheria haina maana kuwa inakuepusha kutenda kosa" amesema Mhandisi Charles.

Akizungumza kuhusu shughuli za wajasiriamali zinazofanywa kandokando mwa barabara amesema ni kosa kuweka magenge, soko katika maeneo ya hifadhi ya barabara.

"Kufanya biashara barabarani ni kosa, wananchi wanatengeneza mazoea na kuonesha ni lazima. Kwa hapa Tarime mjini tulikua na changamoto ya Masoko baada ya soko kuu kubomolewa kwaaji ya ujenzi wa soko jipya.

" Tuliruhusu wananchi wajibanze kwenye hizi barabara wakati masoko yanaboreshwa, yakishakamilika wale waliopo pembeni ya barabara tutawaondoa ili wakafanye biashara zao sokoni, tunawavumilia tu kwa muda kwasababu sio maeneo rasmi ya kufanya biashara" amesema.

Meneja huyo ameongeza kuwa barabara ni kwaajili ya matumizi ya vyombo vya moto na watembea kwa miguu" Hata mimi huwa inanikera lakini hatuwezi kuwavuruga wakati hatujawapa maeneo rasmi ya kufanyia biashara zao kwahiyo tulikubaliana tuwaache kwanza"amesema.


Wakati huohuo, Meneja huyo ameitaka Halmashauri ya Mji Tarime na Halmashauri ya wilaya ya Tarime kushirikiana na Serikali za Vijiji na Mitaa kuweka vibao vya vivuko vya mifugo barabarani na sio mifugo kuvuka kila mahali.

"Halmashauri kwa kushirikiana na Serikali za Vijiji na Mitaa ni jukumu lao kupanga maeneo kwa ajili ya mifugo kuvuka barabara lakini hazijatengwa.

" Tulishaongea na halmashauri watoe maelekezo wapitishe azimio maeneo yatengwe lakini hakuna.

Pia amewataka wakulima kutoharibu barabara " Kuna wale wanaoenda shambani jembe linakokotwa na ng' ombe wanapita barabarani na kuharibu barabara nikiwaona nawachukulia hatua.

Amesema kuwa huwa wanatoa elimu pia kupitia vyombo vya habari, vikao na kwamba kuna adhabu za kisheria.

Ameongeza kuwa wafugaji wamekuwa ni changamoto kwakuwa mifugo yao kama ng'ombe uharibu barabara ambazo hujengwa lakini siku chache uharibiwa na ng'ombe ambao huchimbua kupitia kwato zao.

>>>Barabara ni muhimu katika kuhakikisha inamrahisishia usafiri mwananchi ili kumwezesha kufika mahali popote anapokuwa akitekeleza majukumu yake katika kupata huduma mbalimbali zikiwemo za kijamii,kiuchumi na kiafya .

Barabara ikitumika vibaya inaweza kuwa adha na kero kwa mwananchi na kushindwa kutimiza ndoto zake kwakuwa atakwama katika shughuli zinazomradhimu kutumia usafiri wa barabara.

Mwaka 2007 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga sheria ya barabara ya mwaka 2007( The road Act,2007) namba 13 ya 2007 na sheria hii ilitiwa saini na aliyekuwa Rais Jakaya Kikwete mnamo tarehe 28, Agost, 2007.

Sheria hiyo ilianza kutumika rasmi Desemba,2007 inayozungumiza utunzaji wa barabara na miundombinu ya barabara zikiwemo hifadhi za barabara.

Katika sheria hiyo kifungu namba 50 kifungu kidogo cha 2 (i) kinaruhusu mtu anayevunja sheria ya barabara na hifadhi ya barabara kupigwa faini ya Tsh. laki tatu au kifungo kisichozidi mwaka mmoja jela au vyote kwa pamoja.

No comments