MFUMO WA TOA TAARIFA UTAKAVYOSAIDIA UFUATILIAJI WA BARABARA
Na Baltazar Mashaka, Mwanza
MIUNDOMBINU ya barabara ni kiungo na nyenzo muhimu katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi kutokana na mchango mkubwa katika kujenga uchumi wa taifa lolote.
Pia imekuwa na mchango mkubwa kwa taifa kutokana na kutumika kusafirisha bidhaa mbalimbli za viwandani na shambani kwenda katika masoko.
Hivi karibuni Bodi ya Mfuko wa Barabara nchini (RBF) ilizindua mfumo wa kisasa wa kielektroniki wa ufutiliaji na utoaji wa taarifa barabarani pindi zinapotokea dharura,kero za muda mrefu zinazotokea barabarani na kusababisha usumbufu kwa wananchi na watumiaji wengine wa barabara.
Mfumo wa Kielektroniki wa Ufuatiliaji wa Hali ya Barabara nchini (e-Monitoring App)utakaotumiwa na wananchi kutoa taarifa za uharibifu na matengenezo mabovu ya barabara,ulizinduliwa na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (sekta ya ujenzi) Mhandisi Godfrey Kasekenya.
Uzinduzi wa mfumo huo wa ‘TOA TAARIFA BARABARANI’ ulifanyika jijini Mwanza katika Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania (BOT) sambamba na kikao kazi cha kujadili namna ya kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi katika miundombinu ya barabara.
Mhandisi Kasekenya anasema sekta ya barabara ni nyenzo muhimu kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi,hivyo bila usafiri wa uhakika wa barabara ni vigumu wananchi kunufaika na huduma za kijamii na kiuchumi zinatolewa na kuwezeshwa na serikali ikiwemo elimu,afya na upatikanaji wa masoko.
“Kuzinduliwa kwa mfumo huu ni tukio muhimu katika maendeleo ya sekta ya barabara nchini na yenye mchango mkubwa kijamii na kiuchumi,utawezesha wananchi kutoa taarifa za hali ya barabara kwa wakati.”
Anasema kama taifa ni muhimu kuhakikisha miundombinu ya barabara inatunzwa ili kulinda thamani yake na kuendelea kutoa mchango katika kuleta maendeleo ya nchi.
Naibu Waziri huyo anasema taarifa za hali ya barabara kupatikana kwa wakati ni moja ya njia muhimu za kutunza miundombinu hiyo, anaishukuru bodi kwa kubuni mfumo wa kielektroniki utakaotumiwa na wananchi na watumiaji wengine barabara kufuatilia na kutoa taarifa kwa wahusika kuhusu hali ya barabara katika maeneo yao.
"Nimefurahi kusikia mfumo huu umetayarishwa na wataalamu wa ndani na kuokoa takribani Tsh.Milioni 300 za Kitanzania,nawapongeza wote na nitoe wito kwa taasisi zote za umma zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, kuwatambua wataalamu wa ndani pale walipo, kuwaamini, kuwapa nafasi na kuwajengea uwezo," anasema.
Mhandisi Kasekenya anaeleza kwamba serikali imewekeza fedha nyingi kwenye miundombinu ya barabara lakini inakabiliwa na hatari kubwa ya kuharibika kutokana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi ambapo kiasi cha Tsh.Bilioni 209.7 kilitumika kwa matengenezo ya dharura kati ya mwaka 2015 na 2020.
Anasema matarajio yake uhamasishaji na utoaji elimu juu ya mfumo huo utakuwa miongoni mwa vipaumbele vya Bodi na Menejimenti ya Mfuko kwa sababu serikali imewekeza fedha nyingi kwenye miundombinu ya barabara ambapo inakabiliwa na hatari kubwa ya kuharibika kutokana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi.
“Kwa kutambua athari za mabadiliko ya tabianchi, Serikali iliandaa Mkakati wa Kitaifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi kunzia 2021 hadi 2026 (National Climate Change Response Strategy 2021-2026) ikilenga kujumuisha masuala ya mabadiliko ya tabianchi kwenye mipango na bajeti za kisekta na kuwezesha upatikanaji endelevu wa fedha na teknolojia ili kukabiliana na madhara hayo,”anaeleza Naibu Waziri.
Ameuelekeza Mfuko wa Barabara kuhakikisha unatenga fedha kila mwaka kugharamia shughuli za utafiti utakaojikita kuleta teknolojia ya ujenzi au matengenezo ya barabara zitakazostahimili athari za mabadiliko ya tabianchi.
Pia utafiti huo ulenge kuongeza matumizi ya malighafi inayopatikana hapa nchini, hususan kwenye maeneo ya mradi kama mawe,vifusi na changarawe ili kukabiliana na upungufu wa fedha za matengenezo serikali itaendelea kuongeza vyanzo vya mapata ya mfuko inapowezekana.Anasema ni wajibu wa viongozi wa Serikali za Mitaa kusimamia ulinzi wa miundombinu ya barabara kwenye maeneo yao kudhibiti,athari zinazotokana na wizi wa samani za barabara, matengenezo ya magari barabarani na mifugo kutembea barabarani zitapungua na mwisho kutoweka kabisa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara,Joseph Haule anasema sekta ya barabara ni nyenzo muhimu kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika kurahisisha usafiri wa uhakika wa barabara.
Anasema mfumo huo wa kisasa wa kielektroniki utawarahisishia TANROADS na TARURA utekelezaji wa majukumu yao,watatengeneza kwa wakati barabara pindi uharibifu unapotokea baada ya kupokea taarifa,pia utasaidia kufanyika kwa matengezo ya kawaida ili kudhibiti uharibifu mkubwa usiendelee.
“Kupitia mfumo huu kutakuwa na mikataba ya muda mrefu ya matengenezo ya kawaida ya barabara,itasaidia wananchi kwani wamekuwa wakishuhudia mashimo hatarishi barabarani,yakikaa muda mrefu bila kuzibwa,mitaro kuziba bila kuzibuliwa ama matengenezo duni kufanyika kutokana na kukosekana kwa taarifa kwa wakati na hivyo kusababisha ajali,”anasema Haule.
Anasema kuwa mfumo huo utatumiwa na wananchi kutoa taarifa za hali ya barabara na utawasaidia sana wataalamu kuchukua hatua kwani hapo awali wananchi walipata changamoto ya kutuma na kutoa taarifa,wakati mwingine waliwatumia watu wasio sahihi na kusababisha mchakato wa matengenezo kuchukua muda mrefu.
“Bodi kwa kuunda mfumo huu wa ufuatiliaji wa hali ya barabara,utasaidia kuboresha miundombinu nchini na wakala wa barabara kuandaa utratibu endelevu wa kutuma taarifa kwa namna watakavyoshauriwa, ikiwemo matumizi na miongozo mbalimbali na taarifa zilizoandaliwa, zinazosaidia na kuwezesha nchi nyingi kukabiliana na mbadiliko ya tabianchi,”anasema
Hata hivyo anaeleza kuwa miundombinu ya barabara inakabiliwa na changamoto zinazosababishwa na mabadaliko ya tabia ya nchi changamoto ambazo zinahitaji mikakati ya pamoja na wadau namna ya kukabiliana nazo.
“Miundombinu hiyo ya barabara inakabiliwa na changamoto zinazosababishwa na mabadiliko ya tabia ya nchi katika nchi mbalimbali duniani kama mvua kubwa,joto kali,upepo mkali pamoja na kuzidishwa kwa uzito wa magari barabarani,”anasema Haule.
Anasema barabara ni rasilimali kubwa kiuchumi kutokana na serikali kuwekeza fedha nyingi na takwimu za mwaka 2020 zinaonesha thamani ya mtandao wa barabara zilizorasimishwa ni Tsh.Trilioni 21 sawa na asilimia 16 nchini,hivyo ni vyema kuhusisha taasisi zilizo chini ya wizara katika kusanifu na kujenga miundombinu ya barabara.
"Ni muhimu kwani mbinu za kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya tabia ya nchi kwenye miundombinu ya barabara ni mtambuka,zinahitaji mchango wa wadau mbalimbali kuweza kufanikiwa kwa sababu zina mchango mkubwa wa kutimiza adhima ya Raisa Samia Suluhu katika kuhamasisha na kuvutia wawekezaji,hivyo tunahitaji kuwa na barabara zenye ubora.
“Licha ya mafanikio kuna changamoto za barabara za udongo na changarawe pamoja na uzito mkubwa wa magari,utatuzi wake unahitaji ushirikiano wa wadau wa barabara.Bodi imeunda mfumo huo utumike kutoa taarifa za athari na madhara ya barabara, siku za usoni mabadiliko ya tabianchi yanaweza kuleta madhara makubwa katika miundombinu ya barabara na kuigharimu serikali fedha nyingi,”anasema Haule.
Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Barabara anawaasa wananchi kuutumia mfumo huo kutoa taarifa sahihi na kwa wakati ili zifanyiwe kazi kwa wakati na kufanya hivyo kutaondoa malalamiko na upendeleo wa ukarabati wa barabara kwa viongozi.
Meneja wa Mfuko wa Barabara nchini, Eliud Nyauhenga anasema bodi imeamua kutumia mfumo wa ufuatiliaji wa hali ya barabara ili kuwawezesha wananchi na watumiaji wengine wa barabara kutoa taarifa za uharibifu wa miundombinu hiyo.
“Mfumo huu umeandaliwa na watalaamu wazawa,wananchi na watumiaji wengine wa barabara watautumia kutoa taarifa za uharibifu wa barabara,ujenzi mbovu,mashimo na kuziba kwa mitaro kupitia simu zao za mikononi,hakuna mwananchi atashindwa kuutumia,”anasema Nyauhenga.
Anasema mfumo huo umeokoa Tsh. Milioni 300 na endapo ungeandaliwa nje ya nchi ungeigharimu serikali kiasi hicho cha fedha na kwamba wataendelea kuhamasisha na kuelimisha wananchi na jamii kutumia mfumo huo bila malipo.
Pia mfumo huo utasaidia na utawawezesha wananchi na watumiaji wengine wa barabara kutuma taarifa za kero za barabarani,yakiwemo mashimo hatarishi,kuziba kwa mitaro, ujenzi mbovu na maeneo mengine yanayosababisha adha kubwa kwa wananchi na hivyo kuwezesha kushughulikiwa kwa wakati.
Nyauhenga anafafanua kuwa mfumo huo unamruhusu mwananchi yeyote mwenye simu ya mkononi aina ya batani maarufu kitochi na simu janja, kutuma taarifa ya uharibifu,ubovu wa barabara na kero nyingine kwa kupakua kisimbuzi cha BARABARA mtandaoni kutoa taaifa.
“Lengo la kuanzisha mfumo huo ni kuwawezesha wananchi kutoa taarifa za kero za barabarani kwa mamlaka husika(TANROADS na TARURA) kwa kutumia mfumo huo ili kuokoa maisha ya watu na kutunza miundombinu hiyo muhimu ya usafirishaji,”anasema .
Meneja huyo wa Mfuko wa Barabara nchini, anasema mfumo huo unalenga kuondoa kero na changamoto zinazotokea barabarani,yakiwemo mashimo hataraishi kwa usalama wa wananchi na adha nyingine zinazokwamisha safari za wananchi katika maeneo ya miundombinu ya barabara.
Anasema utaongeza hamasa kwa TARURA na TANROADS ambao ni wanahusika na usalama wa barabara kwa sababu zitaunganishwa katika mfumo huo,polisi wa usalama barabarani na bodi ya mfuko,utawezesha mamlaka hizo kuingia mikataba ya muda mrefu na wazabuni na kushughulikia kwa wakati kero na matengenezo."Serikali inatumia fedha nyingi kujenga na kukarabati barabara,kazi ya Mfuko wa Barabara ni kusimamia na kuhakikisha zinajengwa kwa ubora unaozingatia viwango,zinakuwa katika mazingira ya kuwaruhusu wananchi kuzitumia na kuendelea na shughuli zao bila usumbufu.
Mmoja wa wataalamu wa mfumo huo, Emmanuel Mwakajinga,anasema umeandaliwa na wataalamu wazawa wakishirikiana na wataalamu elekezi kupitia mipango iliyowekwa, hivyo utaongeza wigo wa ufuatiliaji wa miundombinu ya barabara,matatizo ya ujenzi na matengenezo ya barabara.
Anasema progarmu hiyo itapatikana katika simu zote, ina uwezo wa kuchukua taarifa bila mtandao wa internet na kuzituma moja kwa moja baada ya mtandao kurejea,ina uwezo wa kupiga picha za mnato ambapo mwananchi atapata mrejesho wa taarifa aliyotuma kupitia simu yake muda mfupi.
Mwakajinga anasema wananchi watatuma taarifa zao za uharibifu wa barabara,mashimo makubwa yanayoweza kusababisha ajali,matengenezo duni na kero nyingine bila kuingia gharama za vifurushi kupitia *152*00# na watumiaji wa simu janja watapakua kisimbuzi cha BARABARA mtandaoni kutoa taarifa.
Post a Comment