HEADER AD

HEADER AD

MIRADI IKIKAMILIKA CHANGAMOTO YA MAJI ITAPUNGUA MWANZA

Na Baltazar Mashaka,Mwanza

UHABA wa maji umekuwa ni changamoto katika maeneo mbalimbali nchini, hali hiyo imekuwa ikizua malalamiko kwa baadhi ya wananchi kutopata huduma stahiki ya maji kwakuwa maji ni hitaji muhimu katika maisha ya Binadamu pamoja na shughuli za uzalishaji.

Ili kupunguza tatizo la uhaba wa maji, Serikali imekuwa ikijitahidi kutatua changamoto hiyo ya maji kwa kutoa fedha kujenga miradi ya maji ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma kukidhi mahitaji yao.

Mkoa wa Mwanza ni miongoni mwa mikoa uliopata fedha za kutekeleza miradi ya maji katika Bajeti  ya mwaka wa fedha 2022/2023 ambapo Serikali imetoa kiasi cha fedha Tsh.Bilioni 174  kutekeleza miradi 47 ambayo itasaidia kupunguza changamoto ya maji.

Mkuu wa mkoa wa Mwanza Adam Malima anasema kuwa mahitaji ya maji yanakadiriwa kuwa lita Milioni 160 kwa wakazi wa Jiji la Mwanza lenye idadi ya watu  Takribani Milioni 4 lakini maji yanayozalishwa  ni lita Milioni 90,hivyo kusababisha upungufu wa lita Milioni 70 za maji.

"Serikali ya awamu ya sita katika kukabiliana na upungufu wa maji mkoani Mwanza,imewekeza sh. Bilioni 174.8 katika sekta ya maji kwa kutoa fedha za miradi 47 kati ya hiyo 45 ya Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) na miwili ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jiji la Mwanza (MWAUWASA) " anasema Malima.

Anasema kuwa ongezeko la idadi ya watu na shughuli za maendeleo yanayohitaji maji limesababisha mgawo wa bidhaa hiyo jijini Mwanza,mradi wa maji Butimba utakuwa suluhisho na utaongeza uzalishaji wa maji takribani lita 140 milioni,hivyo upungufu kubaki lita milioni 20.

“Mwaka 2021 makadirio ya mahitaji ya maji Jiji la Mwanza yalikuwa ni lita milioni 160 lakini chanzo cha Capripoint kinazalisha lita Milioni 90,upungufu unaosababisha mgawo wa maji maeneo ya miinuko na pembezoni,hivyo mradi wa Butimba utakuwa suluhisho la changamoto hiyo na utaongeza uzalishaji wa lita takribani milioni 140,”anasema.

Mkuu huyo wa mkoa anasema huduma ya maji mkoani humu inatolewa na taasisi tatu za MWAUWASA (Mwanza Jiji,Nansio,Magu na Ngudu),SEUWASA (Sengerema) na RUWASA inayohudumia maeneo ya vijijini,ambapo mjini wanapata maji kwa asilimia 78 na vijijini asilimia 38.

 “Tsh. Bilioni 38.3 mwaka 2020/21 zilitumika kutekeleza miradi 18 ya maji,kati ya hiyo mitatu ya MWAUWASA na 15 ya RUWASA ambapo vijiji 437 kati ya 544 vinapata maji na tunaendelea kusanifu miradi ya kufikisha maji maeneo hayo,mwaka huu tuna miradi 47 yenye thamani ya sh.bilioni 174.8 na kufanya jumla ya Tsh. Bilioni 213.1,”anasema Malima.

Anaishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu,kutenga fedha za miradi ya maji mkoani humu na kwamba ana kila sababu ya kuamini uboreshaji wa huduma ya maji unaofanywa utafikia malengo ya asilimia ya 85 inayotakiwa ifikapo 2025 itafikiwa kama ilivyoelekeza ilani ya uchaguzi ya CCM.

Kutokana na uwekezaji huo wa serikali katika sekta ya maji,anaahidi kushirikiana na Wizara ya Maji kusimamia kwa ufanisi na kukamilisha miradi hiyo ya maji.

Hivi karibuni  September,14,2022 Makamu wa Rais Dk.Philip Mpango aliweka Jiwe la Msingi katika chanzo kipya cha kusukuma maji na Kituo cha Tiba cha Maji Butimba,wilayani Nyamagana mkoani Mwanza,mradi utakaogharimu Tsh.Bilioni 69.3 unaojengwa na kampuni ya M/S Sogea Satom kutoka Ufaransa ambapo alielekeza mradi huo ukamilike Desemba 20202.

No comments