HEADER AD

HEADER AD

UKOSEFU WA MALISHO TISHIO KWA VIJIJI VINAVYOPAKANA NA HIFADHI - 2

Na Dinna Maningo, Tarime

SERA ya Taifa ya Mifugo ya mwaka 2006 inaeleza kuwa, sekta ya mifugo hutoa mazao mengi ya mifugo yanayotumika nchini na hivyo kupunguza uagizaji wa mazao hayo kutoka nje ya nchi.

Pamoja na mchango wa sekta ya mifugo kwenye uchumi wa Taifa, pia huchagia katika kuzalisha chakula, chanzo cha mapato na ajira kwa wananchi hususani wa vijijini.

Sera hiyo inaeleza kuwa,vikwazo vinavyokabili maendeleo katika sekta ya mifugo ni tatizo kubwa katika mfumo wa umilikaji wa ardhi, rasilimali za maji na malisho ni kutokuwa na utaratibu wa kutenga na kumilikisha ardhi kulingana na taratibu za sheria au kimila.

Matatizo mengine ni kupanuka kwa shughuli za kilimo katika maeneo yaliyokuwa yanatumika kwa kufuga na kuchungia, kupanuliwa kwa mbuga za Wanyamapori na kuhamahama kwa wafugaji kunakozuia kuendelezwa kwa maeneo hayo.

Licha ya mifugo kuwa hitaji kubwa kwa Taifa na Jamii hususani wananchi waishio vijijini bado mifugo katika vijiji vinavyopakana na Hifadhi za Taifa (TANAPA ) vinakabiliwa na ukosefu wa maeneo ya malisho, hali hiyo inasababisha baadhi ya wafugaji kuchunga mifugo ndani ya hifadhi ili ipate malisho.

Kitendo cha wafugaji kuingiza mifugo ndani ya hifadhi kimekuwa kikizua migogoro na uvunjifu wa mahusiano mema baina ya wafugaji na askari wanaolinda hifadhi za taifa kwakuwa wakiingia hifadhini hukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria, pamoja na kutaifishwa mifugo yao.

Wilaya ya Tarime mkoa wa Mara, baadhi ya vijiji vinakabiliwa na ukosefu/uhaba wa malisho vikiwemo vijiji 8 vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (SENAPA), jambo ambalo limesababisha migogoro baina ya wafugaji na hifadhi pindi wanapokamatwa, mifugo hukamatwa na kutaifishwa ,huku kukiwa na malalamiko ya baadhi yao kuuliwa na askari wa hifadhi na wengine kupotea katika mazingira ya kutatanisha ndani ya hifadhi.

Wegesa Marwa mkazi wa Kijiji cha Nyandage anasema wananchi walio wengi hawafahamu mpaka unaotenganisha hifadhi  na vijiji, jambo linalosababisha waendelee kulisha mifugo ndani ya hifadhi wakiamini ni ardhi ya Kijiji.

        Moja ya eneo lenye mgogoro

" Serikali kupitia Hifadhi ya Serengeti ilituchimbia kisima cha maji kama ujirani mwema tumekitumia kisima hicho muda mrefu lakini siku zilivyokwenda wakatuzuia kuwa kisima kipo hifadhini hatutakiwi kuingia, kama walijua eneo ni la hifadhi kwanini wachimbe kisima eneo wanalojua siyo la kijiji?, huu ni uonevu tu watu wa vijijini tunaonewa sana kwasababu wanajua hatukusoma "anasema Wegesa.

Jastine Marwa anasema ukosefu wa malisho ulisababisha mifugo yake kuuwawa kwa kupigwa risasi na askari wa hifadhi ya Serengeti wakiwa malishoni eneo la mlimani.



" Ilikuwa mwaka 2014 Ng'ombe wangu 4, mbuzi 11 na kondo 8 wakiwa wanachunga kwenye kingo za mlima walipigwa risasi wote wakafa mimi nilibahatika kukimbia " anasema .

Chacha Tugara anasema" kuna mfugaji mmoja wa kata ya Gorong'a alikamatiwa mifugo yake wanachi wakamchangia fedha ili akaikomboe, alifika hifadhini akapigwa faini kila mfugo 150,000 wakapiga gharama zote akalipa lakini hakupewa zaidi ya kupelekwa mahakamani na pesa kalipa za faini,ana deni la fedha alizochangiwa na mifugo hakupewa. 

"Ukifika pale kuna sehemu ambayo wanakuweka na mifugo yako unapigwa picha ukiwa umesimama kwenye kundi lako la ng'ombe wakimaliza wanakwambia ingia kwenye gari mnapelekwa mahakamani na vielelezo vya picha hizo walizokupiga nakusema ulikamatwa ndani ya hifadhi ukiwa unachunga mifugo " anasema Chacha.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ngoche Matinde Marwa anasema kuuwawa kwa vijana na wengine kupotea kwa mazingira ya kutatanisha  kuna poteza nguvu kazi na kuongezeka kwa wajane na yatima.

"Asilimia 80 ya watu wanaokufa kwa kupigwa risasi wanaowauwa ni askari wa Kenya wa hifadhi ya Masai Mara iliyopakana na hifadhi ya Serengeti, sasa tunajiuliza hivi Tanzania haina walinzi wa kutosha hadi iazime askari wa Kenya kuja kutukamata na kututesa?  " anahoji.

Marwa Mwita anasema alijeruhiwa kwa risasi akiwa anachunga mlimani, anasema eneo hilo wanalitumia kwa miaka yote kulisha mifugo kwakuwa hakuna eneo lingine.





Clement Rafael mkazi wa kijiji cha Masurura anasema ," Tarehe 9,11,2021 tulikuwa njiani tukitoka kunywesha maji mifugo eneo ambalo ni la malisho tuliona askari wa hifadhi, tukaendelea kutembea tukijua hatuna hatia .

" Askari wakatufuata tulipokua wakaanza kuambiana kusanyeni ng'ombe, mweye uwezo wa kukimbia alikimbia wasio na uwezo wakakamatwa na ng'ombe zikataifishwa, ukienda serikalini hakuna utetezi tumebaki kuwa watumwa kweye nchi yetu" anasema.

Juma Mniko mkazi wa kitongoji cha Nyatare  anasema "Vitendo vya unyanyasaji unaofanywa na watu wa hifadhi havijaanza leo ni vya miaka mingi, mwaka 1997 mwezi wa 9 tulikuwa watu 19 tukichunga askari walikuja kutukamata,wachungaji 10 wakafanikiwa kukimbia 9 tukakamatwa tukapelekwa kichakani eneo la tindiga tukalazwa chini kwa kupangwa mistari.

"Mstari mmoja ulikuwa na watu 4 na msati wa pili ulikuwa na watu 5 kisha tukachapwa sana wakainua bunduki zao na kuanza kutumiminia risasi tukiwa tumelazwa chini kwa mistari,wakajua tumekufa wote mimi sikufa ila wenzangu wanane walikufa.

"Nilipigwa risasi usawa wa sikio kushoto ikatokezea chini ya koromeo ,nikapigwa rungu nikapoteza fahamu wakaondoka wakijua nimekufa walikuwa askari wanne ,nilitibiwa leo hii bado nipo mzima " anasema Juma.

Wambura Marwa ni Mzee wa Mila anasema migogoro wa mipaka kati ya vijiji  na hifadhi  ni wa muda mrefu ," chakusikitisha tumekua tukiililia serikali lakini haijwahi kutusikiliza zaidi ya kuamini kuwa wanaoingia hifadhini wanakwenda kufanya ujangiri kitendo hiki kimesababisha mifugo ikose haki ya malisho, wakiona mifugo wanaiswaga kuipeleka hifadhini hata kama wameikuta ikila nyasi nje ya hifadhi.
Wazee wa Mila

Marwa Ryoba Anaongeza " Sisi ni wazee wa miaka mingi tunajua mpaka, huo wanosema wao sio mpaka sahihi wanatuonea kwasababu sisi ni wakurya na wanawachukulia wakurya ni watu wakorofi, wawindaji na kushindwa kutatua kero zetu.

"Wanajali wanyamapori kuliko mifugo ya kufugwa lakini nyama na maziwa wao ndiyo wa kwanza kula iwe kweye arusi,sikukuu,vikao na mikutano, majumbani,kwanini wasile hao wanyama wa hifadhini kama wao wanathamani sana kuliko mifugo ya kufugwa?" anauliza.

Diwani wa Kata ya Gorong'a Ayubu Marwa anasema vijiji vilivyopakana na hifadhi vinaonewa kwakuwa ardhi hiyo miaka ya nyuma ilikuwa na mipaka ya hifadhi ambayo baadae ilibadilishwa.

" Hili eneo kabla ya kuwekwa bikoni lilikuwa eneo la malisho na eneo lingine waliishi watu hata makabuli yapo na ushahidi mzuri ni barabara iliyopita kwenye hilo eneo ambalo hifadhi inalikatalia, barabara hiyo ilikuwa ya kijiji ilitumiwa na wananchi ilikuwa inatoka Nyanungu inapita maeneo ya pori kunakodaiwa ni kwao.

" Ilikuwa inapita hadi Tindiga ya Gorong'a kwenye maji ya chumvi ambapo wazee kwa wakati huo waliitumia barabara hiyo iiliyopita eneo wanalolikatalia, wakati huo kata ikiwa inaitwa Gorong'a iliyozaa kata ya Nyarokoba na Kwihancha.

" Kwa wakati huo ilikuwepo mipaka ya vibao vilivyobandikwa kwenye miti mikubwa iliyokuwepo ilikuwa inatambulika TNP , wananchi walichunga na kuviheshimu hivyo vibao, baadae serikali ikabadili na kuongeza eneo la mpaka wakachukua hadi eneo la chumvichumvi ambalo tulilitumia kwa mifugo " anasema Ayubu. 

Anaongeza " Eneo la chumvichumvi wanakokamatiwa watu ndiko kuna maji yenye madini ya chumvichumvi ambayo yanaimarisha afya ya mifugo, ni tiba ya minyoo wafugaji wanaonywesha pale hawana shida ya tiba ya mifugo maji yale ni tiba tosha. " anasema Diwani.

Diwani wa kata ya Kwihancha Ragita Mato anaipongeza serikali kupitia timu ya wataalamu wa ardhi iliyofika Katani Aprili,2022 na kuonesha mipaka kati ya vijiji na hifadhi ambayo imesaidia kupunguza migogoro ya mpaka uliokuwepo.

"Kuna vijiji kwenye kata yangu vimepakana na hifadhi watu walikuwa wanasumbuliwa na hifadhi ,serikali ilikuja ikafanya uhakiki ile ramani ambayo sisi ndiyo tunaifahamu wataalamu waliifuata hiyohiyo jambo ambalo limesaidia kupunguza migogoro.

"Wataalamu waliifuata tangazo la serikali lilivyoeleza kwa kutekeleza tangazo la 1968  lililotangaza hiyo mipaka, na ndiyo iliyofuatwa kwahiyo kwa sasa mgogoro wa mpaka haupo na hakuna malalamiko " anasema Ragita.

Kauli  ya Afisa Mifugo

Afisa Mifugo Halmshauri ya wilaya ya Tarime Joseph Marwa anasema tatizo linalochangia ukosefu/uhaba wa malisho ni ukame hasa msimu wa kiangazi mwezi wa 6-8, japo anasema ukame sio kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na maeneo mengine nje ya Tarime yaliyo na changamoto kubwa ya ukame.

"Ardhi ya Tarime ni nzuri kuna vijiji ambavyo vina maeneo ya malisho kama Kijiji cha Gibaso, Matongo, Kemambo na maeneo mengine na kuna vijiji vingine havijatenga maeneo ya malisho,jamii yenyewe ndio inatakiwa itenge maeneo maana kuna jamii hazifugi ng'ombe.

"Kijiji cha Surubu wao walitenga eneo la malisho, sehemu nyingine imekuwa vigumu kutenga maeneo ukitenga mtu anaona umekata eneo lake na vijiji vingine havina ardhi za kutenga maeneo ya malisho.Tarime hakuna migogoro ya wakulima na wafugaji kwasababu mtu ni mfugaji huyohuyo ni mkulima"anasema Joseph. 

......Itaendelea





No comments