UKOSEFU WA MALISHO TISHIO KWA VIJIJI VINAVYOPAKANA NA HIFADHI - 3
Na Dinna Maningo, Tarime
ILANI ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM ) ya mwaka 2020-2025, Ibara ya 38 inaeleza kuwa sekta ya mifugo ni miongoni mwa sekta muhimu katika ukuaji wa uchumi, kutokana na umuhimu huo ni dhahiri kuwa ipo haja kuendelea kuimarisha ufugaji wa kisasa na kuchakata bidhaa za mifugo kwa ajili ya mahitaji ya ndani, ikiwemo ya lishe bora, na usafirishaji nje ya nchi.
Ibara ya 40 ya Ilani hiyo inasema katika kipindi cha miaka mitano CCM itaielekeza Serikali kuendelea kuleta mabadiliko makubwa na ya kisayansi katika ufugaji kwa kuhimiza ufugaji wa kisasa wenye kuzingatia kinga, tiba na utafiti wa mifugo ili kuzalisha ajira nyingi zaidi hasa kwa vijana na kuinua mchango wa sekta katika pato la Taifa na kuleta ustawi wa wananchi.
Rais Samia Suluhu akiwa ameshika kitabu cha Ilani ya CCM
Kuimarisha utambuzi na usajili wa mifugo nchini ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wafugaji na mifugo yao, kurekebisha maeneo ya wafugaji kwa kuyapatia huduma muhimu.
Huduma hizo ni maji, afya na elimu kwa ajili ya kusaidia jamii kutulia sehemu moja na hivyo kuepuka kuhamahama kufuata huduma hizo na kuimarisha huduma za maji, malisho na vyakula vya mifugo ikiwa ni pamoja na kubaini na kutenga maeneo ya ufugaji kwa kuyatambua, kuyapima, kuyasajili na kuyamilikisha ili kuongeza maeneo yaliyotengwa kutoka Hekta 2,788,901.17 hadi Hekta 6,000,000.
Pia yamekuwepo malalamiko ya wafugaji wakieleza kuwepo kwa vitendo vya unyanyasaji wa Binadamu na mifugo unaotendwa na Askari wa Hifadhi hiyo pindi mifugo inapochunga ndani ya hifadhi jambo ambalo limesababisha mahusiano mabaya baina ya wafugaji na hifadhi.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji
" 2019 nilikamatiwa mifugo yangu wakasema wanataka watoe mfano walikamata mbuzi 61 wakakamata na mifugo ya wafugaji wengine , wakataifisha na walinifanyia hivyo kwasababu mimi ni kiongozi wa wafugaji. Hakimu alipelekwa porini ndani ya hifadhi akaoneshwa eneo kuwa mifugo ilikuwa ikichunga wakati si kweli haikuwe kwenye eneo hilo.
" Ng'ombe zikauzwa kambini upande wa Kenya na zingine Kambini upande wa Tanzania, tumepata hasara watu wanauwawa wengine wanapotelea hifadhini ,faini yenyewe kubwa , huku kwetu ng'ombe ndio kila kitu ukitaka kusomesha utauza ng'ombe, Afya, kuoa, Chakula tegemeo ni ng'ombe, Serikali itatue hili la maeneo ya malisho yakipatikana hakuna atakayeingia ndani ya hifadhi ," anasema Muhere.
Muhere anasema matukio ya mifugo kupigwa risasi na wahifadhi yalianza mwaka 2009 , ambapo mwaka 2013 baadhi ya nyumba za wananchi ziliteketezwa kwa kuchomwa moto kwamba zipo ndani ya hifadhi huku Operesheni tokomeza ujangiri ikilalamikiwa kuuwa mifugo na kujeruhi wafugaji.
" Operesheni tokomeza ujangiri iliuwa mifugo mingi ikiwa inatoka kwenye chumvichumvi, wafugaji wakakamatwa hao watu walipofika vijijini waliuwa ng'ombe 90, mbuzi 103 , Punda 4 na kujeruhi wafugaji 11 , viongozi wa Chama walifika wakashuhudia ilikua mwaka 2013, Kamati ya Bunge ilifika ikashuhudia ng'ombe zilizouwawa wakazipiga na picha wakasema suala hilo watalipeleka bungeni.
"Haohao tokomeza ujangiri mwaka huohuo wakauwa tena mifugo zaidi ya 470 ,mbwa 93 , punda 24, kondoo 75, iliuliwa hadharani watu walikuwepo wakishuhudia, kwakweli wafugaji na mifugo katika vijiji vilivyopakana na hifadhi ni shida, kwenye mifugo hakuna haki isipokuwa haki ipo tu kwa wanyamapori.
" Hili jambo la malisho bila kutatuliwa vijiji vitakuwa maskini wa kutupwa, askari wa hifadhi wametufirisi haitoshi Tembo nao wanakula mazao na kujeruhi watu lakini wao wapo wanapeta tu hatujaona wakiuwawa kwa risasi kwa kosa la kuingia kwenye makazi ya watu na fidia hakuna ," anasema Muhere.
Operesheni tokomeza ujangiri iliibuliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa lengo jema na kupambana na ujangili unaotishia urithi wa wanyamapori iliyoanza Oktoba, 4 2013 na ilistishwa Novemba,1,2013 kupisha malalamiko yaliyojitokeza wakati wa operesheni tokomeza.
Tarehe 1,Mwezi Oktoba,2014 aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Serikali ya awamu ya nne Dkt. Jakaya Kikwete aliunda Tume ya kuchunguza kuhusu malalamiko yaliyojitokeza na utekelezaji wa Operesheni tokomeza iliyofanya kazi siku 265 na kutembelea wilaya 38 katika mikoa 25 na kuhoji jumla ya mashahidi 259.
Mikoa iliyohusika katika Operesheni Tokomeza ujangiri ni Kigoma, Katavi, Rukwa, Mbeya, Kagera, Geita, Shinyanga, Simiyu, Mara, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Iringa, Morogoro, Pwani, Tabora, Singida, Manyara, Arusha na Tanga.
Ripoti ya Tume hiyo ilieleza kuwa watuhumiwa 1,030 wa makosa mbalimbali ya ujangiri na uvunaji haramu wa misitu walikamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya Sheria na bunduki za kijeshi 18 , bunduki za kiraia 1,579 zilikamatiwa.
Tume ilibaini kuwa katika utekelezaji wa Operesheni kulikuwa na matukio ya ukiukwaji wa sheria, Kanuni, Taratibu, ukiukwaji uliosababisha madhara mbalimbali ikiwemo vifo, askari wengi kuingia kwenye nyumba kwa wakati mmoja, tuhuma za wizi, upotevu, na uporaji wa mali, kuchoma nyumba moto kwa madai ya nyumba hizo kujengwa kwenye hifadhi, wanakijiji kupoteza vyakula na mali zao.
Kauli ya Mtafiti wa Mifugo
Patrick Rukiko ni Mtafiti katika Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Kanda ya Ziwa kituo cha Mabuki kilichopo wilaya ya Misungwi mkoa wa Mwanza, anasema uzalishaji wa wanyama umekuwa ni mdogo kutokana na changamoto mbalimbali katika uzalishaji mifugo unaochangiwa na ukosefu/uhaba wa malisho, hupatikana kwa vipindi, ubora mdogo ambapo upatikanaji ni asilimia 26 ya mahitaji yote.
Mtafiti wa Mifugo (kushoto) Patrick Rukiko
Patrick anasema kuwa malisho ni chakula kikuu cha wanyama wanaocheua wakiwemo, mbuzi, ng'ombe, kondoo na wanyama wa porini wenye sifa kama hiyo, malisho huchukua zaidi ya asilimia 60 ya mahitaji yote ya chakula.
"Malisho huchukua asilimia 70 ya gharama zote za ufugaji wa ng'ombe wa maziwa, ni chanzo cha mapato kwa wauzaji na wazalishaji na hutunza ardhi/kuzuia mmomonyoko.
Mtafiti huyo anasema kama hakuna malisho bora kwa wanyama, uzalishaji utapungua, mifugo na bidhaa zake bei kuongezeka, pato la mwananchi na Taifa kushuka, vifo, ukosefu wa bidhaa bora, kupotea kwa ajira, migogoro ya wafugaji na wakulima.
Utafiti wa TAWILI
Kwa mujibu wa Kijarida sera cha Julai, 2021 cha kusambaza matokeo ya utafiti kilichoandaliwa na Dkt. Cecilia Leweri na Jerome Kimaro kutoka Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) na kuwasilishwa katika Tume ya Taifa ya Sayansi,Teknolojia na Ubunifu (COSTECH) inaelezwa;
Tafiti za TAWIRI zinasema kuwa jumla ya migogoro 41,404 imeripotiwa kwa kipindi cha mwaka 2012-2019 na kati ya hiyo migogoro 29,798 imeripotiwa katika maeneo ya shoroba zilizo katika hifadhi za Taifa kati ya 2017-2020, huku vifo vya Binadamu 2012-2020 ni 1,173.
Majeraha ya kudumu kwa Binadamu 2012-2020 ni 204, Majeraha ya muda kwa Binadamu 2012-2020 ni 514, vifo vya wanyama kwa mwaka 2012-2020 ni 1,146, Uharibifu wa mazao 2012-2020 ni ekari 51,330
Tafiti za TAWIRI zinaonesha kuwa nchini Tanzania migogoro hiyo imekuwa suala kubwa katika jamii ikichochewa zaidi na ongezeko kubwa la idadi ya watu iliyosababisha kuongezeka kwa mahitaji ya matumizi ya maliasili na kusabisha hasara za kijamii, kiuchumi, kibioanuwi na hivyo kuathiri uhifadhi wa wanyamapori.
Hali hiyo inaelezwa kusababisha kupanuka kwa miji na shughuli za Binadamu kama kilimo, ufugaji, uwindaji wa wanyamapori katika maeneo ya makazi ya wanyamapori hususani shoroba, maeneo ya mtawanyiko na maeneo ya kingo (Bafa).
Tafiti zinaeleza kuwa kuingiliwa kwa makazi ya wanyamapori pamoja na shoroba kunatishia uhusiano wa kiikolojia wa maeneo yaliyohifadhiwa (PAs) na kwamba ushahidi wa kiutafiti unaonyesha kuwa, kuna shoroba za wanyamapori ambazo bado zinafaa kwa matumizi ya wanyamapori.
Utafiti huo umebaini kuwa kuwepo kwa migogoro kati ya Binadamu na wanyamapori ikiwemo ya ardhi imechangia kutokea kwa vifo kati ya watu na wanyamapori na uharibifu wa mazao.
Moja ya eneo lenye mgogoro wa malisho Vijiji vilivyopakana na Hifadhi
Utafiti wa TAWIRI unaonesha kuwa vifo vya wanyama kwa mwaka 2012/2013 ni 46, 2013/2014 vifo 93,2014/2015 ni 107,2015/2016 vifo 64,2016/2017 ni 130,2017/2018 ni 149, 2018/2019 ni vifo 203, 2019/2020 vifo 354.
Vifo vya Binadamu kwa mwaka 2012/2013 ni 69, 2013/2014 ni 61, 2014/2015 vifo 59, 2015/2016 ni 102, 2016/2017 ni 132, 2017/2018 vifo 380, 2018/2019 ni 266 na 2019/2020 vifo ni 104.
Utafiti unaonyesha kuwa majeraha ya kudumu kwa Binadamu mwaka 2012/2013 ni 23, 2013/2014 majeraha 31, 2014/2015 ni 20, 2015/2016 ni 20, 2016/2017 ni 30, 2017/2018 ni 20, 2018/2019 walikuwa 60 na 2019/2020 ni 0 hakukuwa na binadamu mwenye majeraha ya kudumu.
Majeraha ya muda kwa Binadamu 2012/2013 ni 38,2013/2014 ni 49, 2014/2015 majeraha 41, 2015/2016 ni 78, 2016/2017 ni 54, 2017/2018 majeraha 29, 2018/2019 ni 149, 2019/2020 waliokuwa 76.
Utafuti huo unaonesha kuwa migogoro kati ya Binadamu na wanyamapori imesababisha uharibifu wa mazao ambapo 2012/2013 ekari 1,518 ziliharibiwa,2013/2014 ekari 4,046, 2014/2015 ni 6,786, 2015/2016 ni 8,924, 2016/2017 ekari 4,567, 2017/2018 ni 5,016, 2018/2019 ekari 10,547 na 2019/2020 zilikuwa ekari 9,926.
Kwa mujibu wa taasisi hiyo ya utafiti imependekeza kuoanisha sera za sekta zinazohusika na matumizi ya ardhi kama vile Sera ya ardhi, wanyamapori, misitu, maji,kilimo, mifugo, na mazingira, pamoja na kuhakikisha kuwa shoroba za wanyamapori zinajumuishwa katika mipango ya matumizi ya ardhi ya Vijiji, Wilaya, Mkoa na Taifa.
Pendekezo lingine ni kurasimisha shughuli mbadala za kiuchumi zinazoendana na uhifadhi wa wanyamapori mbali na shughuli za kilimo, shughuli hizo ndiyo ziwe pekee zitakazofanyika katika maeneo yaliyo karibu na makazi ama mapitio ya wanyamapori ambazo ni pamoja na ufugaji wa nyuki na utalii wa maeneo ya asili na utalii wa kitamaduni.
Ufugaji wa Nyuki
Pia kuwawezesha wananchi kushiriki katika shughuli za uhifadhi, kuwashirikisha wataalamu wa afya kufahamu takwimu za majeraha yaliyosababishwa na wanyamapori, watunga sera, na wadau mbalimbali wawe mstari wa mbele kuunga mkono utekelezaji wa mkakati wa kitaifa na kupunguza migogoro kati ya Binadamu na wanyamapori na urejeshaji wa shoroba.
Post a Comment